25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

BAJETI 2019/2020: Wadau wameguswa

WAANDISHI WETU-DAR/DODOMA

SIKU moja baada ya Serikali kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20 ambayo ni Sh trilioni 33.1, baadhi ya wasomi na wadau mbalimbali wa maendeleo wameichambua bajeti hiyo katika mtazamo wa sura mbili.

Bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ambayo pamoja na mambo mengine Serikali imefuta tozo mbalimbali 54.

Tozo hizo ambazo wasomi na wadau wanaona zitachangia uwekezaji wa ndani kukua, ni pamoja na zile zilizokuwa zikitozwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na katika sekta ya mifugo.

Nyingine zilizofutwa ni pamoja na zile za ukaguzi wa maduka mapya ya bidhaa za chakula, ambayo ilikuwa Sh 50,000 kwa duka.

Hali kadhalika umeme unaouzwa Zanzibar umefutiwa kodi ya VAT ya asilimia 18, huku  watumiaji wa Tanzania bara wakiendelea kulipa asilimia 18 ya VAT.

Bajeti hiyo pia imeshuhudia TRA ikipigwa marufuku kufunga biashara kwa sababu ya madeni na kwamba uamuzi huo sasa utafanywa kwa kibali maalumu cha kamishna na si vinginevyo.

Tofauti na bajeti zilizopita, ambazo mara nyingi zilikuwa zikiongeza ushuru katika bia na sigara, hii haujaongezwa wala kupunguzwa.

Tozo zilizoongezwa katika bajeti ya sasa ni pamoja na ile ya leseni ya udereva ambayo  imepandishwa kutoka Sh 40,000 hadi 70,000, ada ya usajili wa magari Sh 10,000 – 50,000, Bajaji Sh 10,000 – 30,000 na pikipiki Sh 10,000 – 20,000.

Kufutwa msamaha wa kodi taulo za kike, pia nywele za bandia  kutoka nje kuingia kwa mara ya kwanza katika tozo ya asilimia 25, wachambuzi hao wanaona zimeifanya bajeti ya sasa kuwa na sura nyingine.

REPOA

Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (Repoa), Dk. Lucas Katera, katika uchambuzi wake, hasa uamuzi wa Serikali kuondoa tozo mbalimbali, alisema bajeti hiyo imegusa maisha ya Mtanzania wa kawaida.

“Mfano wakulima wadogo ambao wanafuga kuku na wavuvi wameondolewa tozo, wafanyabiashara wa kati wameondolewa tozo za kero kama za TBS, TFDA na Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema Dk. Katera.

Kutokana na hilo, mchumi huyo alisema wazalishaji wa ndani sasa wamewezeshwa kwa kodi za bidhaa za ndani kushuka wakati za nje zikiongezeka hali ambayo alisema itachangia uwekezaji wa ndani.

CWT

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, alisema wao wanaipongeza Serikali kwa kuongeza mishahara ya watumishi kutoka Sh trilioni 6 bajeti iliyopita hadi Sh trilioni 7.

Alisema kutokana na ongezeko hilo, wana imani sasa kilio cha walimu kimesikika.

 “Pia ulipaji wa madeni umeongezeka hadi Sh bilioni 600, hii kwetu ni furaha sana.

“Vilevile kwa upande wa vipaumbele vya Serikali, tumeona ni kuongeza nguvu katika elimu na afya, sasa hapa tuna imani ajira zitaongezeka kwa sababu huwezi kusema nguvu kazi bila ajira,” alisema Seif.

BODABODA

Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Michael Massawe, akizungumzia kuhusu kuongezwa kwa tozo za usajili wa bodaboda katika bajeti ya 2019/20, alisema wamepokea na kwamba hawana namna.

“Tumelipokea japo ni maumivu, lakini hatuna namna, tunajua mwanzo tutaumia ila baadaye tutazoea.

“Lakini pia tunaiomba Serikali pale inapochukua uamuzi wa namna hii, iangalie mahitaji yetu kwa sababu tunakuwa hatufikii malengo yetu,” alisema Massawe.

LHRC

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema bajeti hiyo ni kama inang’ata na kupuliza kwa sababu kuna mambo mazuri yanayofurahisha, mengine yanaumiza.

“Bajeti imeorodhesha mambo ambayo yalikuwa changamoto, mfano upotevu wa mapato, hasa bandari bubu, ugumu wa kukusanya kodi kwenye sekta zisizo rasmi.

“Sijaona mipango ya kuzuia upotevu wa fedha kwenye bandari bubu, ni vyema kungekuwa na ulinzi madhubuti na mpango maalumu kuhakikisha hizo bidhaa hazipotei.

“Kwa upande wa vipaumbele, ni viwanda, kilimo, maendeleo ya watu, miundombinu.

“Sasa kwa upande wa maendeleo ya watu, nikiangalia mafungu yaliyowekwa hapo sidhani kama yanakidhi sekta ya afya, elimu, maji ikapata vifaa vya kutosha,” alisema Henga.

Pia alisema kuna mambo mazuri, mfano kitendo cha Serikali kurudisha kodi katika taulo za kike.

“Hii itawasaidia watoto wa kike na wanawake, kwa sababu bajeti iliyopita pamoja na kodi kuondolewa, lakini bidhaa hizo ziliendelea kuuzwa kwa bei kubwa.

“Mwaka huu jambo zuri alilolielezea Dk. Mpango ni kupunguza kodi ya uzalishaji wa bidhaa hizo kwenye viwanda vya ndani kutoka asilimia 30 hadi 25, angalau itawasaidia watoto wa kike na wanawake.

“Kingine kupunguzwa kodi kutoka Sh 150,000 hadi 100,000 kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kitu ambacho ni kizuri, hivyo jambo hilo ni chanya kwa sababu wengi sasa wataingia kwenye ujasiriamali,” alisema.

DK. BASHIRU

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, naye amechambua bajeti hiyo akisema imeakisi mambo ya msingi yaliyowekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala.

“Ni mapendekezo mazuri yanayolenga shabaha zetu katika Ilani ya CCM. Tuliahidi kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, ajira, umasikini, rushwa ufisadi, amani na utulivu.

“Kama mlivyosikia, sekta zilizopewa kipaumbele kama viwanda, biashara, kilimo na kodi zimeonyesha matarajio makubwa, kwani miradi yetu mikubwa itatekelezwa vizuri,” alisema Dk. Bashiru.

Aliwaomba wabunge wa CCM na upinzani kujadili vizuri bajeti hiyo, lengo likiwa ni kuboresha mapendekezo hayo ya bajeti kuu.

PROF. SEMBOJA

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, alisema bajeti hiyo imeonesha utofauti kwa sababu haijaenda nje ya mategemeo na uwezo wa Serikali katika kutumia rasilimali zilizopo na kuwezesha wananchi kuwa wawekezaji katika ukuaji wa uchumi.

Alisema kwa kawaida bajeti hutafsiriwa katika mapato na matumizi ya Serikali na kwamba kazi ya Serikali inajulikana kuwa ni kushughulikia masuala ya sera, sekta zote za maendeleo, ulinzi na usalama.

“Ukiangalia katika bajeti hii, mimi ningesema ni bajeti moja nzuri, imekuwa ina ‘details’ (maelezo) zote bila kuwa na wasiwasi.

“Bajeti ya zamani ilikuwa wanaongeza na kupunguza basi, na hakukuwa na maelewano kati yao na sekta binafsi,” alisema.

Kuhusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupigwa marufuku kufunga biashara, alisema katika masuala ya kodi na utawala, ufungaji wa biashara huwa ni suala la mwisho na ambalo halimpendezi anayefunga wala anayefungiwa biashara, na hivyo kusisitiza ulazima wa ukusanyaji kodi kufanywa na mtu mwenye utaalamu.

 “Hili la kusema watu waende bandarini kuchukua mizigo yao hata zamani ilikuwa hivyo, suala la kutumia mawakala wa forodha ilikuwa ni kupunguza msongamano na baadhi ya watu kutoelewa taratibu,” alisema Profesa Semboja ambaye alikuwa akirejea kauli ya Serikali wakati ikiwasilisha bajeti yake kwamba wananchi sasa wataweza kutoa mizigo yao wenyewe bandarini.

Mtaalamu huyo wa uchumi, alisema kutokana na watu kutofahamu sheria na taratibu, kunaweza kusababisha wakashindwa kufanya vizuri badala ya kuvuna wakaliwa kutokana na kuwapo kwa mifumo inayoingiliana.

PROFESA MSOLA

Mhadhiri wa masuala ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Susan Msola, alisema hatua ya Serikali kutoa misamaha mbalimbali katika sekta ya kilimo na mifugo, kunaipa sekta hiyo hadhi inayostaahili.

“Nadhani hii ni kuipa tasnia ya kilimo hadhi yake ambayo ina washiriki wengi wa kati na wadogo. Pia itahamasisha uwekezaji mkubwa, utaendeleza vyema sera yetu ya viwanda.

“Lakini hatua hii inatakiwa pia iende sambaba na uboreshaji wa mazingira wa shughuli za ugani,” alisema.

ALI MFURUKI

Mwenyekiti wa Kampuni ya InfoTech Investment Group Ltd, Ali Mufuruki, ambaye alizungumza na kituo kimoja cha redio, alisema bajeti hiyo ni nzuri na imejibu maswali ya wafanyabiashara.

“Kwa kifupi ni bajeti nzuri ambayo inaonekana hasa kusapoti wafanyabiashara kwa kujibu maswali ambayo tulikuwa tukiuliza kwa muda mrefu, kuhusu usimamizi wa kodi ambao unatakiwa kuwa wa haki.

“Kwa mfano kurahisisha ulipaji wa kodi na kupunguza gharama za kufanya biashara hapa nchini, ikiwemo kupunguza kodi kwenye uingizwaji wa vifaa mbalimbali, hasa vya uzalishaji ambavyo naona katika bajeti hii Dk. Mpango amevipa kipaumbele.

“Matatizo halisi yaliyopo katika uchumi ambayo yamezungumzwa na sekta binafsi na watu wengine katika nchi hii, Serikali imeyatolea majibu,” alisema Mufuruki.

PROFESA NGOWI

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, alisema kimsingi bajeti hiyo iliyopendekezwa ni ya kawaida kama ya miaka iliyopita.

Alisema kama ilivyo katika bajeti zilizopita, hakuna jambo la kushangaza sana kwa kuwa vyanzo vya mapato ni vile vile na miradi inayotekelezwa ni ile ile.

“Mtu yeyote ambaye alishasoma bajeti miaka iliyopita na hii, hakuna ‘big surprise’ kivile, ingawa kuna ongezeko kidogo la asilimia 1.9 ukilinganisha na ya mwaka jana,” alisema.

Alisema katika bajeti ya mwaka jana kuna baadhi ya mambo mengi yalisemwa, lakini bado hayajatekelezwa kutokana na sababu mbalimbali, mapato hayakupatikana vya kutosha.

“Kwa hiyo kwa mimi ambaye nimefikiria bajeti kwa miaka 15, sijaona la kushangaza sana, ni bajeti ya kawaida.

“Ndio kuna maeneo yanamkuta mwananchi, mfano kuna uwekezaji katika elimu, afya, miundombinu kama  barabara, reli. Sasa kumgusa mwananchi inategemea utekelezaji wake, inaweza ikamgusa mwananchi au inaweza isimguse, ni vile inavyotekelezwa.

“Kama tunajenga SGR, Stiegler’s Gorge sasa mwananchi anashiriki vipi katika hayo, kwani bajeti inapanga tu, sasa mwananchi anashirikiana vipi, hilo ni jambo jingine,” alisema Profesa Ngowi.

Habari hii imeandaliwa na ELIZABETH HOMBO, LEONARD MANG’OHA, GRACE SHITUNDU (Dar) Na RAMADHANI HASSAN (Dodoma)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles