30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania, DRC wakubaliana maeneo tisa nyeti

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

SERIKALI ya Tanzania na DR Congo zimekubaliana kushirikiana katika maeneo tisa yatakayowezesha uchumi wa nchi hizo kukua na kuimarisha uhusiano uliopo.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana baada ya mazungumzo baina ya Rais Dk. John Magufuli na Rais wa DRC, Felix Tshisekedi ambaye aliwasili nchini juzi kwa ziara ya siku mbili.

Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Rais Magufuli alisema ziara hiyo inatoa fursa kwa nchi hizo kuanza ushirikiano katika masuala mbalimbali.

Aliyataja mambo waliyokubaliana kuwa ni kukuza ushirikiano katika masuala ya kiuchumi, kushirikiana kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuwekeza sekta za viwanda, kilimo, uvuvi, utalii na nyingine.

Makubaliano mengine ni kuhimiza taasisi za fedha kufungua matawi katika nchi zote, kurahisisha kufanya biashara, kubadilishana uzoefu katika kutumia rasilimali zilizopo, kushirikiana katika ujenzi wa viwanda, kilimo, utalii, afya, ulinzi na usalama, utunzaji mazingira, sanaa, michezo na utamaduni na kutumia shoroba kukuza biashara na uwekezaji.

Mengine ni kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji na kuwahamasisha wananchi kutumia fursa zilizopo, kufufua Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambayo haijakutana tangu mwaka 2002 na kukubaliana ikutane kabla ya mwaka huu kuisha na kufanya vikao vya ujirani mwema na makongamano ya biashara.

“Licha ya kuwa na uhusiano wa muda mrefu, lakini ushirikiano wetu katika nyanja za kiuchumi si mkubwa sana, Congo ndio mahali pa kufanya biashara, ni ndugu zetu kwani hata baadhi ya makabila yako Congo, lakini yako pia Tanzania,” alisema.

Rais Magufuli alisema mwaka 2018 biashara kati ya Tanzania na DRC ilikuwa na thamani ya Sh bilioni 305,375 huku miradi ya uwekezaji kutoka nchi hiyo iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ipo nane yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.77.

Alisema miradi hiyo imetoa ajira kwa watu 418 tu na kwamba Watanzania wachache pia wamewekeza katika sekta ya usafirishaji na madini nchini DRC.

Rais Magufuli alisema mwaka jana DRC iliongoza kwa kusafirisha mizigo mingi katika Bandari ya Dar es Salaam – tani milioni 1.78 kutoka milioni 1.176 mwaka juzi.

“Kiwango hiki ni kidogo sana ukilinganisha na ukubwa wa nchi zetu na fursa zilizopo. DRC ni ya pili kwa ukubwa Afrika na sisi Tanzania ni wa 13, mpaka wetu unaanzia Kigoma hadi Katavi na Rukwa na urefu wa mpaka wa DRC na Tanzania ni takribani kilomita 554,” alisema.

Alisema nchi hizo zina idadi ya watu milioni 140 na kwamba zina kila kitu kama vile rasilimali za misitu, madini, gesi na nyingine, hivyo kuna umuhimu wa kufanya biashara kubwa kwa faida ya nchi zote.

Rais Magufuli alisema Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuboresha sekta ya uchukuzi na kwamba Bandari ya Dar es Salaam imeanza kutoa huduma za pamoja kwa saa 24 na siku saba za wiki.

Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kudhibiti vitendo vya wizi, kufanya upanuzi kuiwezesha kupokea shehena kubwa za mizigo na kuongeza muda wa kutunza mizigo ya DRC kutoka siku 24 hadi 30.

“Tumeondoa katazo la ufunguaji wa makontena na kufuta tozo ya Dola za Marekani 600 kuwawezesha maofisa TRA kusindikiza mizigo DRC.

“ TPA imefungua ofisi Lubumbashi kuwarahishia huduma wafanyabiashara wa DRC,” alisema Rais Magufuli.

RAIS TSHISEKEDI

Rais Tshisekedi alisema lengo la ziara yake ni kukuza uhusiano baina ya nchi hizo na kwamba wamekubaliana kuimarisha amani katika eneo la Maziwa Makuu ili watu wanaotaka kujihusisha katika shughuli za kiuchumi waweze kunufaika.

“Tumetambua kuna biashara kidogo sana baina ya nchi zetu na tumeona kwa haraka lazima ile tume ya pamoja ifanye kazi kuchambua kwa kina changamoto zilizosababisha hali hiyo.

“Kuna masuala ya miundombinu na kushughulikia changamoto za vizuizi vya biashara,” alisema Rais Tshisekedi.

Pia aliwasilisha ombi la nchi yake kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambalo lilikubaliwa na mwenyeji wake Rais Magufuli.

Alisema DR Congo na Tanzania zina mpaka wa pamoja wa zaidi ya kilomita 500, hivyo nchi hizo ni lazima zifanye kazi kwa pamoja kudumisha uhusiano.

Kabla ya makubaliano hayo, Rais Tshisekedi alikagua miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na shughuli zinazotolewa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Rais Magufuli pia alimwalika Rais Tshisekedi katika mkutano wa SADC unaotarajia kufanyika nchini Agosti mwaka huu na aliahidi kushiriki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles