25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Uchafu uliokithiri makazi ya Jangwani

Na TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

HOFU ya kuenea magonjwa ya mlipuko ikiwemo Dengue na Kipindupindu imetanda kwa wakazi wa mtaa wa Mtambani A Kata ya Jangwani Manispaa ya Ilala kutokana na kukithiri kwa uchafu katika mazingira ya eneo lao.

MTANZANIA JUMAPILI lilifika katika mtaa huo na kubaini kuwapo kwa uchafu uliokithiri ikiwamo maji yaliyotuama ndani na nje ya baadhi ya nyumba zao kwa muda mrefu.

Maji hayo ambayo wakazi hao wanasema yametuama kwa takribani miaka minne tangu kilipojengwa kituo cha mwendokasi yalionekana kubadilika rangi kutokana na kuchanganyika na yale yaliyotoka katika vyoo.

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya nyumba zikiwa  zimezingirwa na tope  hali iliyofanya watu wapite kwa tabu katika maeneo hayo.

Pamoja na nyumba nyingi za mtaa huo kuzungukwa na maji ambayo yanatoa harufu mbaya, pia maeneo yote ya  mtaa huo  yamezungukwa na uchafu ikiwamo mifuko chakavu ya plastiki maarufu.

Mwandishi wa gazeti hili alizungumza na mkazi wa eneo hilo liyejitambulisha kwa jina la Halima Said ambaye alionekana akitoka katika tope hilo na kuingia katika nyumba ambayo imejaa maji.

Mama huyo ambaye mtoto wake alilazwa katika Hospitali ya Amana kutokana na ugonjwa wa kuhara alisema nyumba iliyojaa maji ndio anayoishi kwa sasa.

“Humu ndani ndimo ninaishi na hali hii kwa sasa tumeizoea kwa kuwa imekuwa ya muda mrefu,” alisema Halima.

Alisema maji hayo yamekuwapo kwa muda mrefu ambapo awali walilazimika kukimbia makazi hayo kuepuka mafuriko lakini mvua zilipopungua waliamua kurejea.

“Tumerejea hapa ndio tumekutana na maradhi ya Dengue na Kipindupindu, tuliondoka kwa mafuriko tumerudi tumekuta maradhi,” alisema Halima.

Naye Mwenyekiti wa mtaa huo, Ally Mohamed alisema  hata ofisi ya serikali ya mtaa huo imejaa maji kwa takribani miaka minne jambo lililosababisha viongozi hao kufanya shughuli zao nje.

“Kama mlivyoona hapa tangu miundombinu ya maji ya eneo hili kuzibwa na maji kushindwa kuelekea baharini imekuwa mateso kwa wakazi wetu,” alisema Mohamed.

Wakati hali ikiwa hivyo katika eneo hilo Manispaa ya Ilala imeanza kupulizia dawa ya kuua viruirui na mbu wa Dengue na wadudu wanaosababisha Kipindupindu.

Wagonjwa wanane wa kipindupindu wameripotiwa katika eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles