27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Sababu tano zilizoipa ubingwa Simba

SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM

LIGI Kuu Tanzania Bara inafikia tamati kesho, lakini tayari timu ya Simba imefanikiwa kutetea  ubingwa ilioutwaa pia msimu uliopita.

Simba ilifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida United na kufikisha pointi 91 ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine zinazoshiriki  ligi hiyo, ikiwemo mpinzani wake wa karibu Yanga ambayo ikifanikiwa kuifunga Azam  kesho, itafikisha pointi 89.

MTANZANIA linakuletea sababu tano zilizochangia Simba kufanya vizuri katika ligi hiyo na hatimaye kubeba taji hilo huku ligi ikiwa bado haijamalizika.

Falsafa ya Aussems

Wakati Aussems anakabidhiwa kikosi cha Simba, alikikuta kinatumia mfumo wa 3-5-4.

Mfumo huo ulikuwa unatumiwa na aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma.

Aussems alipoingia aliutosa mfumo wa Djuma wa 3-5-4 na kuingiza wa kwake ambao ni 4-3-3.

Mwanzo ulionekana kuwashinda wachezaji wa timu hiyo.

Kumbuka  kuhusu suluhu ya Simba dhidi ya Ndanda FC katika mchezo  wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Septemba 15, Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Manispaa ya Mtwara.

Wapo walioanza kutilia mashaka  uwezo wa Aussems baada ya suluhu  dhidi ya Ndanda.

Hata  hivyo, Mbelgiji huyo hakuyumbishwa na yale maneno  ya karaha ya  baadhi  ya mashabiki wa Simba waliokiri waziwazi kumkumbuka Djuma kama ndiye aliyekuwa anastahili  kukipika kikosi chao na kama kutimuliwa, basi alipaswa mzungu huo.

Mambo yalizidi kuwa magumu kwa  Aussems baada ya kikosi chake kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ndanda, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Septemba 20, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kipigo  ilichokipata Simba kilisababisha Aussems kutupiwa makopo ya maji pamoja na kutolewa maneno  ya kashfa na mashabiki wa timu hiyo.

Tukio hilo lilitokea wakati kocha huyo akielekea vyumba vya kubadilishia mavazi.

Lakini kadiri Wekundu hao walivyozidi kushuka dimbani, ubora wa kikosi cha timu hiyo ulizidi kuongezeka  kiasi cha kuwapa taabu wapinzani wake kwa kuibuka na ushindi mnono.

Okwi, Kagere, Bocco

Uwepo wa washambuliaji  hawa watatu wenye ubora wa juu ni   dhahiri ulichagiza kwa kiasi kikubwa timu ya Simba kutetea taji lake la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo.

Imekuwa vigumu kwa Emmanuel  Okwi, Meddie Kagere na John Bocco kuondoka uwanjani pasipo mmoja wao  kufunga bao.

Unaweza kuthibitisha  kwamba washambuliaji hao watatu si wa mchezo mchezo kwa kuangalia idadi ya mabao waliyopachika  kwa  pamoja ambayo yanafikia 54 na hiyo ni kabla ya mchezo wa mwisho wa timu yao dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa kesho Uwanja wa  Jamhuri, Morogoro.

Timu  nzima ya Simba imefunga mabao 77, lakini robo  tatu yamefungwa na washambuliaji hao  watatu pekee.

Ubora wa Kikosi

Hakuna  shaka kwamba Simba ndiyo timu iliyokuwa na kikosi imara zaidi miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Hili unaweza kuliona kwa kuangalia mchezaji mmoja mmoja  wa Simba na kulinganisha na wale wa timu nyingine.

Simba ilikuwa imekamilika kila  idara na jambo la maana zaidi lililofanywa na Kamati ya Usajili ya timu hiyo ni kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi ya mmoja  katika kila nafasi.

Hili liliifanya timu hiyo kutotetereka hata pale  mchezaji wake muhimu alipopata majeraha  yaliyomlazimisha kuwa nje ya uwanja kama ilivyotokea kwa beki Shomari Kapombe aliyeumia akiwa katika majukumu ya timu ya  Taifa, Taifa Stars.

Malengo ya Ubingwa, Ligi ya Mabingwa

Mapema kabisa uongozi  wa timu hiyo chini ya mwekezaji wake, Mohamed Dewji, aliweka wazi malengo yao katika Ligi Kuu Tanzania Bara  kuwa ni kutwaa ubingwa.

Ili kufikia malengo hayo, kila mdau katika klabu hiyo alipambana kutekeleza wajibu wake, hatua iliyosaidia timu hiyo kufanya vizuri dimbani.

Lakini pia kitendo cha Simba  kufikia na hatimaye kuvuka malengo ya  michuano ya  Ligi ya Mabingwa Afrika, kilichochea kufanya vizuri katika Ligi Kuu  Tanzania Bara.

Ikumbukwe kwamba, malengo ya Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa kufika hatua ya makundi, lakini  ilivuka na kufika robo fainali.

Hili liliwaongezea ujasiri wachezaji na kuona kama wameweza kuzifunga timu vigogo Afrika, zikiwemo TP Mazembe na Al Ahly kwanini washindwe kuifunga Yanga au Lipuli.

Motisha kwa wachezaji

Uongozi  wa Simba  umetengeneza utaratibu wa kutoa motisha kwa wachezaji wao pale wanapofanya vizuri kwa kupata ushindi katika michezo yao. Hili liliwaongezea sana hamasa wachezaji  na kuwafanya wajitume zaidi dimbani.

Umoja na mshikamano

Kama kuna kitu ambacho kimekuwa kikiathiri maendeleo ya klabu za Simba na Yanga ni migogoro. Migogoro hii ni ama uongozi na wachezaji, uongozi na mabenchi ya ufundi, viongozi kwa viongozi, wachezaji na mabenchi ya ufundi au uongozi na wanachama wao.

Kwa Simba hiki hakikuwepo safari hii na kama kilikuwepo, basi kilimalizwa kwa njia ya kistaarabu pasipo watu wasiohusika kufahamu. Utulivu ndani ya klabu ya Simba ulikuwa chachu ya kutetea ubingwa wake msimu huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles