KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa makamu wa rais wa TFF, Michael Wambura imeendelea kupigwa kalenda kwa zaidi ya miezi mitatu sasa kutokana na upelelezi kutokamilika.
Wakili wa serikali Fatma Waziri, amedai hayo leo Alhamisi Mei 23 katika mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Kelvin Mhina wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.
Wakili Fatma amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi haujiamilika wakaomba tarehe nyingine ya kutajwa na kwamba upelelezi ukikamilika wataeleza.
Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni 4 kwa kutajwa na mshtakiwa anaendelea kusota gerezani kwasababu mashtaka yake hayana dhamana.
Wambura anakabiliwa na mashtaka 17, yakiwemo mawili ya kutakatisha jumla ya Sh. milioni 100.9.
Awali ilidaiwa mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka 17, yakiwemo 13 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, mawili ya kutakatisha fedha, moja la kughushi na moja la kuwasilisha nyaraka ya kughushi TFF.