Ramadhan Hassan,Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum,Amina Molel (CCM) ameomba mwongozo bungeni akihoji ni kwanini Nahodha wa timu ya Taifa na Mshambuliaji wa timu ya Genk ya Ubelgiji,Mbwana Samatta hapongezwi na Serikali.
Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu,Mbunge huyo alisimama na kuomba mwongozo kwa Spika wa Bunge Job Ndugai.
Katika mwongozo wake,Mollel amedai kwamba Samatta amefanya vizuri lakini Serikali ipo kimya.
“Mheshimiwa Spika Mtanzania mwenzetu Mbwana Samatta anayecheza Soka la kulipwa Nchini Ubelgiji ameiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa ameongoza Ligi hiyo kwa kufunga mabao 23.
“Kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Mtanzania mwenzetu na tumeona wenzake na hasa wenyeji wakishangilia kwa kutumia bendera ya Tanzania ni dhahiri kabisa ameitangaza vema Nchi yetu.
“Mheshimiwa Spika ninaomba kupata kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hilo ili kutoa motisha kwa watanzania wengine.
“Lakini kibaya zaidi kuna mtandao umeandika kwamba ni Mkenya ninaomba kauli ya Serikali ili wengine waache kudandia dandia,”amehoji Molel.
Akijibu,Spika Ndugai amesema jambo hilo ni jema na Serikali imemsikia na italifanyia kazi.
“Tutawasiliana na Serikali namna ya kushughulika na jambo hili wakati muafaka na serikali imekusikiliza ni jambo la msingi,”amesema Spika Ndugai