ALLAN VICENT-TABORA
Kikundi cha Umoja wa wajasiriamali Mkoani Tabora kinatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha kukamua mafuta ya alizeti mwishoni mwa mwaka huu ili kuinua uchumi wa wanachama wake.
Akiongea na Mtanzania Katibu wa Umoja huo Ashura Shaban amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unatarajia kuanza Agosti mwaka huu na kitajengwa katika manispaa ya Tabora.
Amesema kuwa dhamira ya kujengwa kwa kiwanda hicho ni matokeo ya kiu kubwa ya maendeleo waliyo nayo wanachama wake ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano za kuwa nchi ya uchumi wa viwanda .
Aidha Ashura ameongeza kuwa ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kwa asilimia 100 serikali ya mkoa imewakopesha matrekta mawili ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kupata malighafi zinazohitajika kwa ajili ya kiwanda hicho.
‘Tumedhamiria kufanya mambo makubwa sana, kujengwa kwa kiwanda hicho kutawanufaisha sana wanachama, jamii na serikali kwa ujumla kwani tutalipa ushuru na kodi stahiki, tumeendelea kujiimarisha zaidi na hadi sasa tuna wanachama zaidi ya 200 na kila wilaya tuna wawakilishi’, amesema.