JUBA, SUDAN KUSINI
RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir, ametoa onyo kuwa serikali yake hataivumilia maandamano au mbinu zozote zisizokuwa za kisheria kumshinikiza kuondoka madarakani.
Wiki mbili zilizopita, vuguvugu linalojiita Red Card Movement, limeanzisha harakati za kumtaka Rais Kiir kuondoka madarakani. Kundi hilo linatumia maandishi kama #KiirMustGo na #SouthSudanUprising, ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kwenye mitandao ya kijamii, huku waandaaji wakiwa nje ya nchi hiyo.
Taarifa zinasema kuwa harakati hizo zinatarajiwa kufuata mfano wa hali ilivyokuwa katika nchi jirani ya Sudan, baada ya waandamanaji kuanzia mwezi Desemba mwaka 2018, kuanza kushinikiza kuondoka madarakani kwa rais wa zamani, Omar Al Bashir.
“Wale watakaojaribu kuharibu utulivu wa nchi watashughulikiwa. Namna ya kuimarisha udhabiti wa Sudan Kusini ni kupitia demokrasia na kupitia uchaguzi, na hili hatutaacha,” amesema rais Salva Kiir.
Sudan Kusini ilijikuta katika vita ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013, baada ya Rais Kiir kumshutumu Makamu wake wa rais, Riek Machar kutaka kumwondoa madarakani.
Kiir na Machar wametia saini mkataba wa amani kuunda serikali ya pamoja, lakini imedaiwa kuwa ni vigumu kutekeleza mkataba huo, huku Machar akiishi nje ya nchi hiyo.