LONDON, UINGEREZA
CHAMA cha upinzani cha Labour nchini Uingereza kimevunja mazungumzo yaliyodumu kwa wiki sita sasa ya Brexit ya kupata mwafaka na Waziri Mkuu, Theresa May, na kulalamika kuwa mamlaka yake yanayeyuka na utawala wake unakaribia mwisho, hali ambayo inaelekea kuuzamisha uongozi wake kwenye mkondo unaohatarisha mwelekeo wa mpango huo.
Hayo yamefichuliwa kwenye barua ya kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn aliyomwandikia Waziri Mkuu Theresa May, ambapo amesema mpasuko kati ya chama chake na chama tawala cha Conservative hauwezi kuzibwa, na ile hali ya kujiamini na kuaminiana haipo tena, kwamba mrithi wake ataendelea na maridhiano yoyote yanayoweza kupatikana.
“Majadiliano yamekwenda hadi yalipofikia. Ongezeko la udhaifu na kutokuwa thabiti kwa serikali yako kuna maana hakutakuwa na imani katika kulinda chochote kinachoweza kukubaliwa baina yetu, kupitia mazungumzo tunayojaribu kufanya,” amesema Corbyn katika barua hiyo.
Kiongozi huyo amesisitiza kuwa, chama chake cha Labour kitaendelea na msimamo wao wa kupinga makubaliano ya talaka yaliyofikiwa na serikali kama yalivyo hivi sasa.
Makubaliano yaliyofikiwa na Waziri May pamoja na Umoja wa Ulaya na kumlazimisha kuchelewesha tarehe ya Brexit yamekataliwa mara tatu na Bunge la Uingereza, hali ambayo inakinyooshea kidole chama cha Labour kuhusika kukwamisha mpango huo.
Muda mpya wa mwisho wa Brexit ni Oktoba 31, mwaka huu, lakini Bunge la Uingereza linatarajiwa kupiga kura kwa mara ya nne mapema mwezi Juni kuhusiana na masharti ya nchi hiyo ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.
Waziri May, ambaye ameonekana kuchoshwa na sakata hilo, alisema wabunge watakabiliwa na kile alichosema kuwa ni chaguo gumu, kupiga kura kukubaliana na Brexit, ama kukataa tena.
Akizungumza katika tukio mahsusi la kampeni kabla ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya, utakaofanyika nchini Uingereza, maoni ya wapiga kura yanaonesha chama chake cha Conservative kinaweza kushika nafasi ya tano.
Uingereza haikutaka kushiriki katika uchaguzi huo, lakini itafanya hivyo kwasababu ya kuahirishwa mara kwa mara mpango wa Brexit.
Kuvunjika kwa mazungumzo hayo kumekuja siku moja baada ya Waziri May kukubali kuweka muda maalumu kwa ajili ya kuachia wadhifa wa uwaziri mkuu, kufuatia kura ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya bungeni, ambayo itafanyika katika muda wa wiki moja kuanzia Juni 3.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mkutano wa faragha pamoja na wanachama na viongozi wa wabunge wa chama cha Conservative. Inafikiriwa kwamba May atazindua mpambano wa kuwania nafasi ya uongozi mara muswada wa makubaliano ya kujitoa ama ukishindwa, kama inavyoonekana kuwa, ama utakamilishwa.