24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Brexit kumng’oa madarakani Waziri Mkuu Theresa May

LONDON, UINGEREZA

CHAMA cha upinzani cha Labour nchini Uingereza kimevunja mazungumzo yaliyodumu kwa wiki sita sasa ya Brexit ya kupata mwafaka na Waziri Mkuu, Theresa May, na kulalamika kuwa mamlaka yake yanayeyuka na utawala wake unakaribia mwisho, hali ambayo inaelekea kuuzamisha uongozi wake kwenye mkondo unaohatarisha mwelekeo wa mpango huo.

Hayo yamefichuliwa kwenye barua ya kiongozi wa chama  cha Labour, Jeremy Corbyn  aliyomwandikia Waziri Mkuu Theresa May, ambapo amesema mpasuko kati ya chama chake na chama tawala cha Conservative hauwezi kuzibwa, na ile hali ya kujiamini na kuaminiana haipo tena,  kwamba mrithi wake  ataendelea na maridhiano yoyote yanayoweza  kupatikana. 

“Majadiliano yamekwenda  hadi yalipofikia. Ongezeko la  udhaifu na kutokuwa thabiti kwa serikali yako kuna maana  hakutakuwa na imani katika  kulinda chochote kinachoweza  kukubaliwa baina  yetu, kupitia mazungumzo tunayojaribu kufanya,” amesema Corbyn katika barua hiyo.

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa, chama chake cha Labour kitaendelea na msimamo wao wa kupinga makubaliano ya  talaka yaliyofikiwa na serikali  kama yalivyo hivi sasa.

Makubaliano yaliyofikiwa na Waziri May pamoja na Umoja  wa Ulaya na kumlazimisha kuchelewesha tarehe ya  Brexit yamekataliwa mara tatu na Bunge la Uingereza, hali ambayo inakinyooshea kidole chama cha Labour kuhusika kukwamisha mpango huo.

Muda mpya wa mwisho wa Brexit ni Oktoba 31, mwaka huu, lakini Bunge la Uingereza linatarajiwa kupiga kura kwa  mara ya nne mapema mwezi  Juni kuhusiana na masharti  ya nchi hiyo ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya.

Waziri May, ambaye ameonekana kuchoshwa na sakata hilo, alisema wabunge watakabiliwa na kile  alichosema kuwa ni chaguo gumu, kupiga kura  kukubaliana na Brexit, ama  kukataa tena.

Akizungumza katika tukio  mahsusi la kampeni kabla ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya, utakaofanyika nchini  Uingereza, maoni ya  wapiga kura yanaonesha chama chake cha Conservative  kinaweza kushika nafasi ya  tano.

Uingereza haikutaka kushiriki  katika uchaguzi huo, lakini  itafanya hivyo kwasababu ya  kuahirishwa mara kwa mara mpango wa Brexit. 

Kuvunjika kwa mazungumzo  hayo kumekuja siku moja  baada ya Waziri May kukubali kuweka muda maalumu kwa  ajili ya kuachia wadhifa wa  uwaziri mkuu, kufuatia kura  ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya bungeni, ambayo  itafanyika katika muda wa  wiki moja kuanzia Juni 3. 

Makubaliano hayo yamefikiwa  katika mkutano wa faragha pamoja na wanachama na  viongozi wa wabunge wa chama cha Conservative. Inafikiriwa kwamba May atazindua mpambano wa kuwania nafasi ya  uongozi mara muswada wa makubaliano ya kujitoa ama ukishindwa, kama inavyoonekana kuwa, ama utakamilishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles