25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA KULIAMSHA KWA NDANDA LEO

Na MOHAMED KASSARA

-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Wekundu wa Msimbazi, Simba, leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba inaongoza katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 85 baada ya kucheza michezo 34, ikishinda 27, sare nne na kupoteza mitatu.

Mabingwa hao watetezi watashuka  dimbani wakitoka kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho uliochezwa uwanja huo.

Ndanda wanayokutana nayo inashika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47 baada ya kucheza michezo 35, ikishinda 12, sare 11 na kupoteza 12.

Wana Kuchele hao watashuka dimbani wakijiamini baada ya kutoka kuvuna  ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya African Lyon katika mchezo wao wa mwisho uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba itaingia uwanjani kuikabili Ndanda  ikiwa na kumbukumbu  ya kulazimishwa suluhu katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Septemba 15, mwaka jana, kwenye  Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Hata hivyo, mchezo huo hautakuwa rahisi kwa wababe hao wa Msimbazi, kwani kikosi hicho kinahitaji ushindi pekee ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea taji lao hilo walilolitwaa msimu uliopita.

Kuelekea mchezo huo, Kocha wa Simba, Patrick Aussems, ataendelea kujivunia washambuliaji wake, Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi, ambao kwa pamoja wameifungia timu hiyo mabao 50 hadi sasa.

Wakati Aussems akitambia makali ya washambuliaji wake, Ndanda itapata pigo la kumkosa mpachika mabao wao hodari, Vitalis Mayanga, ambaye atakosekana kutokana na kukabiliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Aussems, alisema mipango yake ni kushinda mchezo huo ili kujipatia pointi tatu muhimu zitakazowafanya wazidi kujisafishia njia ya kutetea ubingwa wao.

 “Tunatakiwa kufanya kazi kubwa ili tupate pointi tatu, Ndanda moja ya timu ngumu sana, itatubidi kujitoa zaidi kushinda mchezo huo, kama unavyojua tulishindwa kupata pointi tatu katika mchezo wa kwanza, hata hapa haitakuwa rahisi kupata ushindi.

“Tunahitaji kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wetu, mbali na ubingwa pia tunahitaji kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi msimu huu, tumebakiza michezo minne na tunahitaji pointi tano, tutaanza kuzikusanya kwa Ndanda, kisha kumalizia kazi kwa Singida wiki ijayo,” alisema Aussems. 

Kwa upande wake Kocha wa Ndanda, Khalid Adam, alisema kikosi chake kinahitaji pointi mbili tu kujihakikishia kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao, hivyo hawatakuwa tayari kupoteza mchezo huo muhimu kwao.

“Mechi yetu na Simba si rahisi, tumejipanga kuona tunaondoka na pointi tatu muhimu, najua wapinzani nao wanasaka ushindi kuona wanatetea ubingwa wao msimu huu.

“Hatuhitaji kupoteza mchezo huo na wachezaji wote wako fiti kabisa bila shida, tunakwenda kupambana kwa ajili ya kusaka pointi, hata tukishindwa basi tupate moja, lakini si kutoka mikono mitupu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mwadui FC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles