26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Kakolanya kutua Simba ni kujipoteza

Na ZAINAB IDDY

HIVI karibuni kumekuwa na tetesi juu ya mlinda mlango wa zamani wa Yanga, Beno Kakolanya kuwa katika mazungumzo na Simba kwa ajili ya kuingia kandarasi na kuwatumikia msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kakolanya anahusishwa na Simba, baada ya kumaliza mkataba katika klabu ya Yanga.

Mbali ya kufikia tamati kwa mkataba huo, kipa huyo alikuwa na mgogoro na klabu hiyo ambapo aliishutumu kutomlipa stahiki zake.

Sababu hiyo ilimfanya achukue uamuzi wa kujiondoka kikosini, lakini hata pale wadau wa klabu hiyo walipomtuliza na kutaka arejee kundini, kocha wake, Mwinyi Zahera alimtolea nje.

Zahera alitoa msimamo mkali, akisema hataki kumuona tena kipa huyo katika kikosi chake.

Kakolanya alisajiliwa na Wanajangwani hao kutoka kwa maafande wa Tanzania Prisons misimu minne iliyopita.

Vyanzo vilivyo karibu na nyanda huyo vinadai kuwa tayari kipa huyo amekutana na bilionea wa klabu hiyo ya Msimbazi, Mohamed Dewji, kwa lengo la kuzungumzia mkataba.

Kama kweli Kakolanya atamalizana na Simba, yapo maswali mengi ambayo wadau wa soka wanaweza kujiuliza kutokana na hali ilivyo ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wachezaji wengi walioondoka Yanga kwenda Simba kwa ushawishi wa fedha hawakuweza kudumu.

Mfano mzuri ni Hussen Sharif ‘Cassilas’ na Mohamed Said ‘Nduda,’ waliojiunga na Wekundu  hao wa dau zuri, lakini waliishia kusugua benchi na kula fedha za bure.

Wawili hao ni mfano tosha kwa Kakolanya, hivyo bila shaka kama anakwenda kwa ajili ya kupata nafasi ya kucheza imekula kwake, kwani ni vigumu kumuweka benchi Aishi Manula, aliye bora zaidi katika soka la Tanzania kwa sasa.

Tunakumbuka kile kilichotokea kwa Nduda, aliyekaa benchi kwa misimu miwili, baada ya kusajiliwa akitokea Mtibwa Sugar, huku Manula aking’ara ndani ya kikosi cha Simba. 

Msimu huu tangu aliposajiliwa Deogratius Munishi ‘Dida’, bado nyota ya Manula imeweza kung’ara, baada ya kuweza kuhimili mikiki mikiki ya mashindano iliyoshiriki timu yake, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika asilimia 90 ya michezo ambayo Simba imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Mapinduzi na Kombe la Shirikisho, maarufu kama Azam Federation Cup, Manula ndiye aliyesimama langoni, huku akipata nafasi mara chache tu.

Lakini pia ubora wa Manula umezungumzwa na makocha mbalimbali, akiwamo yule wa makipa wa Simba, Mohamed Mwarami, aliyeweka wazi kuwa kwa Tanzania hivi sasa hakuna mlinda mlango anayeweza kumuweka benchi Manula na kama ikitokea labda ni kutokana na matatizo ya kiafya.

Mbali na kocha huyo wa Simba, hata yule wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Emmanuel Amunike, pia ameunga mkono kauli ya Mwarami, baada ya kuweka wazi kuwa hajaona mlinda mlango mahiri Tanzania zaidi ya Manula.

Ni ukweli ulio mchungu kwa Kakolanya kuwa kama anakwenda Simba kwa lengo la kukuza kipaji chake kwa sasa si mahali
sahihi kwake, kwani ni bora hata angerejea Prisons, akaenda Ndanda, Lipuli au timu nyingine katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwenda Simba ni kutoa nafasi ya kuua kiwango chake ambacho kilishaanza kuimarika kiasi cha kuwa namba moja ndani ya Yanga.

Lakini kama Kakolanya anakwenda Simba kwa lengo la kuvuta fedha za tajiri Mo ni sawa, ila anapaswa kufikiria mara mbili katika hili kwa kuwa umri wake bado mdogo na anahitaji kupata sehemu atakayocheza na kukuza uwezo wake ili ayafikie yale aliyowahi kuyaweka wazi kuwa anahitaji kwenda kucheza soka la kulipwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles