NA HASSAN DAUDI
NI miaka 25 imepita tangu Afrika Kusini ilipojitoa katika minyororo ya sera ya ubaguzi wa rangi (Apartheid policy) chini ya Waholanzi, zikiwa ni juhudi kubwa za mwanasiasa mkongwe barani Afrika, marehemu Nelson Mandela. Wataalamu wa historia watakumbuka kuwa sera hiyo ilianzishwa mwaka 1948, lengo likiwa ni kuwaweka mbali wazawa wa taifa hilo na huduma zote muhimu kwa kigezo cha rangi nyeusi ya ngozi zao.
Ni katika sera hiyo ndipo kinapopatikana kisa maarufu cha Waafrika kutakiwa kupisha kiti pindi tu raia wa Kizungu anapoingia ndani ya basi. Hata ujenzi wa shule, hospitali au miundombinu mingine ulitegemea aina ya watu waliokuwa wakiishi eneo hilo, kwamba wale wenye ngozi nyeusi hawakustahili chochote kati ya hayo.
Hiyo iliwahi kuthibitishwa na moja kati ya ripoti za tafiti, ikionesha kwamba kufikia mwaka 1996, ni asilimia nane tu ya watu weusi waliokuwa wakishikilia nyadhifa za utendaji mkuu katika kampuni za ndani ya taifa hilo.
Hata hivyo, licha ya kwamba ni zaidi ya miongo miwili imepita, kwa macho ya wengi juu ya Afrika Kusini, bado haionekani kuwa kuna tofauti kubwa kati ya maisha ya wananchi wa taifa hilo tangu walipoachana na mateso ya ukoloni.
“Huwa inanikera sana kusikia watu wanasema kila kitu kipo sawa tangu sera ya ubaguzi ilipokwisha, kwamba watu weusi na weupe ni marafiki,” anasema mpiga picha wa jijini Cape Town, Alice Mann.
Labda matarajio ya walio wengi baada ya kuondoka kwa ukoloni ni kwamba wangepata fursa ya kumiliki ardhi, huduma bora za afya na elimu, ndoto ambayo imeendelea kusubiriwa bila mafanikio tangu walipopata uhuru wao mwaka 1994.
Kwa upande mwingine, unaweza kusema ni kutimia kwa kile alichowahi kutamka mzee Nelson Mandela, aliposema katika moja ya hotuba zake kuwa nchi hiyo haitakuwa huru endapo watu wengi wataishi bila chakula cha kutosha, mavazi ya kueleweka, huduma bora za afya na kazi za kujiingizia kipato.
Kwa kipindi chote cha utawala wa kidemokrasia, bado sehemu kubwa ya watu weusi imeendelea kuwa kwenye mkwamo, hasa katika nyanja ya kiuchumi, hali inayoakisi maisha ya mateso waliyoishi chini ya sera ya ubaguzi. Hayo yanafanyika licha ya ukweli kwamba watu weupe ni sehemu ndogo tu (8%) ya idadi ya Waafrika Kusini.
Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaanika wazi kuwa Afrika Kusini inabaki kuwa nchi yenye pengo kubwa kati ya walionacho na masikini. Kama ilivyokuwa chini ya sera ya ubaguzi wa rangi, kwa sasa watu weusi wameachwa mbali linapokuja suala la umiliki wa mali na wengi si wenye elimu kubwa.
“Ukiacha kuwa wanabaguliwa katika sekta ya ajira, bado hata wakipata nafasi wanalipwa ujira mdogo, mambo ambayo yalikuwa sugu wakati wa utawala wa Waholanzi nchini humo,” inaeleza ripoti ya mwaka huu ya WB.
Akitoa maoni yake juu ya hali hiyo, aliyekuwa mgombea urais kupitia Democratic Alliance (DA), ambaye alibwagwa na Rais Cyril Ramaphosa, Mmusi Maimane, alisema bado wananchi wenye ngozi nyeusi wanawekwa mbali na mfumo wa fursa za kiuchumi.
“Ukweli ni kwamba ukosefu wa ajira kwa Waafrika Kusini weusi ni asilimia 39, tofauti na weupe ambayo ni asilimia 8.3,” alisema mwanasiasa huyo aliyeambulia asilimia 21 ya kura za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, akikipiku Economic Freedom Fighters (EFF) cha mwanasiasa kijana, Julius Malema (11%).
Aidha, kwa upande wake, ripoti ya WB ilisisitiza: “Si kwamba unaweza kuponda juhudi za Serikali ya chama tawala, African National Congress (ANC), lakini ukweli ni kwamba huduma kama maji safi, umeme, elimu na afya zimekuwa zikiwafikia wachache.”
Imefikia hatua hata baadhi ya maeneo yanaeleweka wazi kuwa ni ya watu weupe, ambayo kwa kiasi kikubwa yanahakikishiwa huduma zote za kijamii. Mfano mzuri katika hilo ni Jiji la Cape Town, ambalo ni ngumu kuwakuta Waafrika Kusini weusi wakiinjoi maisha.
Kile kinachoendana na hicho ni kauli iliyowahi kuzua taharuki kubwa nchini humo ya aliyekuwa wakala wa mashamba, mwanamama Penny Sparrow, alipowafananisha Waafrika Kusini weusi na nyani.
Ikifafanua juu ya pengo lililopo kiuchumi, ripoti hiyo ya WB inaonesha kuwa familia yenye kipato kizuri, ambazo nyingi ni za wananchi weupe, inaweza kuizidi hata mara 10 ile masikini. “Ukitazama idadi ya wanaolala njaa itakushangaza,” inasisitiza ripoti ya WB.
Kwa upande wake, Murray Leibbrandt, profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Cape Town, ambaye alifanya utafiti uliohusisha wananchi 30,000 kuanzia mwaka 2008 hadi 2017, anasema: “Watu weupe ndiyo sehemu kubwa ya wasomi (hapa Afrika Kusini).”
Madai yake hayatofautiani na yale ya kuwapo kwa shule nyingi nchini humo, ambazo katika hali ya kusikitisha, wanafunzi hutengwa kutokana na rangi ya ngozi zao.
Kwingineko, yamekuwa yakiibuka malalamiko kuwa wanafunzi wenye rangi nyeupe wamekuwa wakiendelea na masomo hata wanaposhindwa kufikia ‘maksi’ zilizowekwa lakini huwezi kulikuta hilo kwa wenzao weusi, ambao hulazimika kubaki hapo hadi watakapofaulu.
Profesa Leibbrandt anaongeza kuwa si rahisi kwa nchi kutokuwa na pengo la aina hiyo lakini inaweza kujitamba kuwa inakwenda vizuri endapo tu itapambana kupunguza kwa kukuza watu wenye kipato cha kati.
“Kiwango cha kutokuwapo kwa usawa nchini Afrika Kusini kimekuwa kikirithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine, jambo ambalo ni hatari,” anasema msomi huyo.
Hivi karibuni, Rais Ramaphosa alionesha kurejea kwa namna nyingine kile alichokisema Mandela miaka mingi iliyopita. “Hatuwezi kuwa taifa la watu huru ikiwa wengi wao wanaishi katika dimbwi la umasikini,” alisema.
Kauli yake hiyo inaonesha kuwa hata viongozi wa juu serikalini wanakiri kuwa wananchi wao hawako huru kama walivyotarajia baada ya kuitokomeza sera ya ubaguzi.
Juu ya sababu ya kuwapo kwa hali hiyo ya ubaguzi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Mcebisi Jonas, aliwahi kusema lazima Serikali ya Afrika Kusini ilipe uzito suala hilo kwa kuwekeza katika elimu dhidi ya wale wenye vitendo vya ubaguzi.
“Hakuna anayezaliwa akiwa na chuki dhidi ya rangi ya ngozi ya mtu mwingine, hayo ni mafundisho ndiyo yanayoibua chuki. Ikiwa wanafundishwa hivyo, basi inawezekana wakafundishwa kupenda (wenzao),” alisema.