29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Watoto sita wenye ulemavu waokotwa wakiwa wametupwa na walezi wao

NA IBRAHIM YASSIN, ILEJE

WATOTO sita wenye ulemavu wilayani Ileje mkoani Songwe wameokotwa wakiwa wametupwa na wazazi pamoja na walezi wao.

Wilaya hiyo inatajwa kukithiri kwa vitendo vya kutupa watoto wanaozaliwa pindi wanapobainika kuwa na ulemavu.

Hatua hiyo imebainika baada ya jana wananchi wa kijiji na Kata ya Bupigu kumuokota mtoto mwenye ulemavu wa mkono huku akiwa na tatizo la akili anayekadiliwa kuwa na miaka 14.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti na gazeti hili,wakazi wa eneo hilo,walisema tatizo hilo limekuwa sugu hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati na kulimaliza.

Hakimu Mwanilu, mkazi wa Ileje, alisema matukio ya kuokotwa watoto wenye ulemavu ambao wamekuwa wakitupwa na wazazi wao limekuwa likijitokeza mara kwa mara na kwamba ili kukomesha hatua hiyo serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo iendeshe semina kwa wananchi.

Ericka Mtali muuguzi wa hospitali ya wilaya hiyo ambako mtoto huyo amehifadhiwa huko hadi sasa alisema, amekuwa akielewana na mtoto huyo kutokana na kuongea lugha ya Kisafa ambapo endapo kama hayupo inakuwa shida kuelewana na wahudumu wengine.

Tabitha Swila, Afisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, licha ya kukiri kuwepo kwa hali hiyo, alisema baadhi ya wazazi ama walezi wamekuwa na uelewa duni kuhusu kuwalea watoto wenye ulemavu hivyo ofisi yake imejipanga kuhakikisha inatoa elimu kwa umma ili kuepuka hali hiyo.

Enock Mwambalaswa mganga mkuu wilayani humo,alikiri kuwepo kwa matukio hayo na kusema kuwa hospitali hiyo imempokea mtoto huyo aliyeokotwa kwenye pori lililopo kijiji cha Bupigu na kwamba anaendelea kutibiwa na kutunzwa akiwa hospitalini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Haji Mnas alisema matukio hayo yamekuwa yakijitokeza na kujirudia rudia hali inayowapa mzigo mzito kitengo cha ustawi wa jamii kuwahudumia watoto hao.

Alisema kutokana na hali hiyo,ipo haja ya wananchi kujua umuhimu wa kuwatambua watoto walemavu kama watoto wengine na pia amewatahadharisha kuwa uongozi wa halmashauri utahakikisha unawachukulia hatua watakaobainika kutupa watoto.

Mkuu wa wilaya ya Ileje, Joseph Mkude,alisema kwa kushirikiana na ustawi wa jamii atafanya sensa ya kutambua idadi ya walemavu na kuwatunza katika vituo vya kulelea watoto katika taasisi mbalimbali ambapo serikali itaweka mkono wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles