25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lusinde awapa darasa wasomi chuo kikuu

Khamis Mkotya, Dar

MBUNGE wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), ametoa tafsiri pana kuhusu dhana ya uzalendo na namna inavyopaswa kutekelezwa, ili kulinda rasilimali za taifa.

Lusinde amesema uzalendo ni hali ya kupenda kuthamini, kuheshimu rasilimali za taifa ambao msingi wake unatokana na makuzi ya kijana, tofauti na wengi wanavyofikiri kuwa uzalendo ni kuipenda nchi tu.

Mbunge huyo pia alisisitiza uzalendo unaovuka mipaka na kuthamini heshima, haki na hadhi za watu, huku akiitaka jamii kujipamba na uzalendo unaovuka ubinafsi kwa faida ya wengine.

Lusinde alitoa somo hilo juzi, wakati akiwasilisha mada katika kongamano la wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) lililofanyika Ukumbi wa Nkrumah.

Kongamano hilo lililokuwa likihusu vyombo vya habari vya Kiswahili duniani liliandaliwa na Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere katika taaluma za Kiswahili.

Mbali ya Lusinde wabunge wengine walioalikwa katika kongamano hilo lakini hawakuhudhuria ni pamoja na Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM), Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM) na Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF).

Katika mada yake, Lusinde maarufu Kibajaji alisema ufisadi na wizi uliopo nchini hasa serikalini umesababishwa kwa kiasi kikubwa na wasomi wengi kupungukiwa maadili na kukosa misingi imara ya uzalendo.

Aidha mbunge huyo alitoa wito kwa bodi za kitaaluma kuanzisha kozi ya uzalendo mashuleni na vyuoni kama hatua ya kuwaandaa vijana kuwa wazalendo.

 “Kwa kukosa kuzalisha wazalendo tumejikuta tunazalisha mafisadi wengi, inabidi tuwafundishe vijana wetu uzalendo na kuhitimu shahada za uzalendo kama mnavyozalisha wanataaluma wengine.

“Kama hamfanyi hivyo inakuwaje watu wakiwa wakubwa tunataka ghafla wawe wazalendo kazini? Je kuna profesa yeyote hapa ambaye kawa profesa ghafla tu kwa kusema tu awe profesa? Tunafanya makosa makubwa kwa kutaka watu wawe wazalendo ghafla ukubwani.

“Ikumbukwe kuwa mtu anafundishwa kuwa daktari au uhandisi kwa faida ya jamii na siyo kwa faida ya tumbo lake, lakini mtu huyo akifundishwa udaktari au uhandisi tu pasipo kufundishwa uzalendo lazima ataishia kulisha tumbo lake na familia yake,” alisema.

Kuhusu uzalendo unaovuka mipaka, Lusinde aliitaka jamii kuiga mifano ya wapigania uhuru kama Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Kwame Nkrumah (Ghana) na mwanamapinduzi Ernesto Che Guevara ambao walivuka mipaka ya nchi zao kwa kupigania ukombozi wa bara la Afrika.

“Maana rahisi ya uzalendo imezoeleka kuwa ni kuipenda, kuona fahari ya nchi yako. Kwa bahati mbaya wengi tunadhani ukiipenda nchi yako inabidi uzichukie nchi nyingine, hapana huo si uzalendo,” alisema

Hata hivyo Lusinde alisema anashangaa kada ya wasomi imekumbwa na kitu gani, kwani Rais Dk. John Magufuli, amekuwa akiwalalamikia mara kwa mara kwamba wanamwangusha katika nafasi mbalimbali za uteuzi anazowapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles