32.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Nkwande akemea uchawi,utoaji mimba

Mwandishi Wetu-Mwanza

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Renatus Nkwande, amesema anasikitika kila anaposikia watu wanaongelea mambo ya uchawi na kusema huo ni ushamba wa elimu.

“Mtu akivimba tumbo unasema amelogwa, tena unamtaja na fulani ndiye mchawi. Huo ni ushamba wa elimu na tena huko ni kukosa imani na kushindwa kumuamini Mwenyezi Mungu,” amesema.

Alitoa kauli hiyo jana, wakati akitoa shukrani kwenye ibada ya kumsimika kuwa Askofu Mkuu wa jimbo hilo iliyofanyika kwenye viwanja vya Kawekamo jijini Mwanza.

“Watu wetu wana hofu mbalimbali ambazo zimewakamata tangu utoto wao. Tuwasaidie waumini hawa ili wamwamini Mungu kwamba anaokoa na anaweza kuwaponya madhila waliyonayo.

“Tuwasaidie watu wetu wajikomboe kielimu, wajiendeleze kwenye masomo ya fizikia, kemia na kadhalika,” amesema.

Alisema anashangaa tabia ya waafrika ya kupenda kuiga mambo ya ajabu kwa vile tu yameletwa na wazungu. “Sisi Waafrika ni watu wa ajabu tunaiga vitu visivyo na msingi. Wameleta ushoga, tunaiga! Wameleta utoaji mimba tunaiga. Leo hii kuna taasisi zinasambaza hata vifaa vya kutolea mimba, nasi tumekaa tunaangalia tu.

“Wazee wetu walipoona wamechoka ukoloni, walipigana ili kupata uhuru. Leo na sisi tupiganie uhuru kwa kukataa masuala ya ushoga na utoaji mimba.

“Huo ni uuaji, hiyo ni dhambi. Miongoni mwetu leo wapatikane watu wa kusimamia hayo ili ukoloni huu usiendelee kutawala akili za watu wetu,” alisema.

Aliwaomba Watanzania wamwombe Mungu awabariki, alibariki Taifa la Tanzania ili yanayofanyika yawasaidie kwenda mbinguni.

Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo na hatimaye kuwatoa kwenye umaskini. “Tunaamini yote anayofanya ni kwa manufaa ya Watanzania wote,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Magufuli na mamia ya waumini na viongozi waliohudhuria ibada hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema anatambua kuwaongoza watu kiroho na kimwili ni jambo lenye uzito mkubwa.

“Sisi viongozi na waumini kwa kutambua kazi nzuri uliyoifanya hadi kufikia kupata wadhifa huo tuna imani utaweza. Nakuomba upokee mzigo huo kwa matumaini na bila kusita kwani waumini wa kanisa hili wako pamoja nawe na viongozi wenzako wote tunategemea watatoa ushirikiano kwako. Tunachosema ni kwamba, jipe moyo kwa kuzingatia yaliyoandikwa katika Wafilipi 4:13 kwamba “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Jitwishe mzigo huo kwa imani na utaubeba bila kuchoka, sisi sote tuko pamoja nawe,” alisema.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kusisitiza suala la kutunza amani ya nchi na akawaataka viongozi wa dini na waumini kote nchini kuendeleza upendom hurma na kuwa na roho ya msamaha. “Tuhurumiane sasabu sisi si wakamilifu, kwa hiyo tuongeze msamaha miongoni mwetu,” amesisitiza.

“Nawaombeni wote, tuendelee kutumia nyumba zetu za ibada kuliombea Taifa hili ili tuendelee kuishi kwa amani, upendo na mshikamano. Tuepuke migogoro ya mara kwa mara katika nyumba zetu za ibada. Tuendelee kujenga waumini wetu wakue kiroho na kujenga dhana ya umoja na upendo katika Taifa letu. Watu wa Mungu ni watu wa upendo, watu wa Mungu ni watu wa amani, watu wa Mungu ni watu wa kiroho.”

Mapema, akitoa salamu za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Rais wa TEC, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga aliwataka waumini wa kanda ya ziwa wawe na mshikamano na wampe ushirikiano Askofu Mkuu Nkwande.

“Kuweni na upendo kama Bwana Yesu alivyofundisha na pia ombeeni utumishi mwema kwa viongozi wote wa Serikali na watumishi wote wenye jukumu la kuongoza watu.”

Askofu Nyaisonga aliishukuru Serikali kwa kulipa nafasi Kanisa Katoliki ya kushirikiana na Serikali kutoa huduma za jamii kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika sekta ya elimu na afya.

“TEC inapenda kuhimiza mshikamano baina ya Serikali na kanisa ili kuwe na ufanisi wa huduma tunazotoa za kumlinda mama na mtoto na kijana. Ufanisi huu utapatikana kwa kuimarisha miundombinu hasa katika ngazi za chini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles