Na Mwandishi Wetu, Dar
MBUNGE wa Mtera, Livingistone Lusinde (CCM), anatarajiwa kuhutubia kongamano la wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) litakalofanyika Mei 10 na Mei 11.
Kongamano hilo la vyombo vya habari vya Kiswahili duniani limeandaliwa na Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere katika taaluma za Kiswahili.
Barua ya mwaliko iliyosainiwa na Profesa Aldin Mutembei wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, imemtaja Lusinde kuwa ni miongoni mwa watoa mada katika kongamano hilo litakalohudhuriwa na wasomi mbalimbali.
Kwa mujibu wa barua hiyo, kongamano hilo ni la kwanza la kimataifa litakalokutanisha pamoja vyombo mbalimbali vya habari duniani vinavyojishughulisha na habari, matangazo na taarifa za Kiswahili.
“Kwa heshima, tunakukaribisha uwe pamoja nasi wakati wa kongamano hili litakalofunguliwa rasmi Mei 10, 2019 na kufungwa Mei 11, 2019.
“Tunaona fahari kubwa kwamba umekubali kuwa mmoja wa watoa mada katika kongamano hili. Tunatarajia mada yako itakuwa miongoni mwa zile zitakazotoa mjadala mzuri na wa kina miongoni mwa washiriki.
“Kwa hakika waandaaji, uongozi wa Chuo Kikuu na wanajumuia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanakusubiri kwa hamu kubwa,” ilisema barua hiyo ya Aprili 30, 2019.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu mwaliko huo Lusinde (Kibajaji), alisema ameupokea na kwamba kuitwa kwake kama mtoa mada ni kielelezo tosha kuwa wanataaluma sasa wanahitaji mawazo ya Watanzania wa kawaida badala ya yale ya kwenye vitabu.
“Kwa muda mrefu watoa mada kwenye makongamano wanakuwa wasomi wa viwango mbalimbali ambao mara nyingi huwasilisha mawazo ya kwenye vitabu akina Socrate, Aristotle na mawazo mengine ya wagiriki .
“Leo imefika mahala sasa wasomi wanahitaji kusikia mawazo ya Watanzania wa kawaida kama akina Lusinde na wengine wasiokuwa na elimu kubwa kwa mustakabali wa taifa hili,” alisema Lusinde.