26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Maofisa watendaji wamkera kiongozi wa CCM

Na OSCAR ASSENGA

MUHEZA

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga, Mohamed Moyo, amekerwa na tabia ya baadhi ya watendaji wapya wa kata wilayani humo, wasiotaka kushirikiana na madiwani waliopo kwenye maeneo yao.

Moyo alisema hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa kikao cha baraza la madiwani la wilaya hiyo, kilichokutana mjini hapa ili kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.

“Kuna malalamiko mengi kutoka kwa madiwani, kwamba baadhi ya maofisa watendaji wapya hawataki kushirikiana na madiwani.

“Jambo hilo linaweza kusababisha kuchangia kwa asilimia kubwa, kudorora kwa maendeleo, jambo ambalo hatuwezi kulikubali.

“Kwa hiyo, nawaomba waache tabia hiyo mara moja, kwa sababu tabia hiyo inarudisha nyuma maendeleo yetu na namuomba mkurugenzi akalifanyie kazi hilo, kwani viongozi hao pamoja na ugeni wao kazini, inaonekana hawataki kujifunza kutoka kwa wazoefu kazini,” alisema Moyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Nassib Mbaga, alisema watendaji hao wanatakiwa kuonana na madiwani ili kujadili maelekezo wanayopewa wilayani.

“Nawaambia haya kwa sababu mnaweza kwenda kwenye kata zao na kuwakuta madiwani hawashiriki kwenye mikutano yenu na mtakapoona hivyo, msiwalaumu hao madiwani.

“Pamoja na hayo, mtambue kwamba, mshikamano ni muhimu kwenye maendeleo, kwani siku zote tunaambiwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu,” alisema Mbaga.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu (CCM), alisema amefanikiwa kutatua kero nyingi za wananchi kutokana na ushirikiano anaopata kutoka kwa madiwani.

“Sidhani kama kuna diwani anaweza kusema hana mradi ambao ameusimamia na hana chochote cha kuzungumza mwakani wakati wa uchaguzi mkuu.

“Ila, kama kuna diwani ambaye anaamini hana cha kuzungumza mwakani wakati wa uchaguzi mkuu, aje tuonane ili tujue cha kufanya,” alisema Adadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles