25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Joto la uchaguzi ubunge2020 laanza kupanda

ARODIA PETER-DODOMA

Hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya baadhi ya wabunge wanaopata nafasi ya kuchangia mijadala ya bajeti za wizara kadhaa zilizowasilishwa bungeni kuelekeza moja kwa moja katika majimbo yao tofauti na vikao vilivyopita vya Bunge.

Baadhi ya wabunge wa kambi zote za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na upinzani, wameonyesha hofu kwamba kama baadhi ya miradi haitatekelezwa basi watapata wakati mgumu kujinadi kwa wapiga kura katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Huku mijadala ya kutupiana vijembe kati ya wabunge wa upinzani na CCM kama ilivyokuwa katika vikao vilivyopita imeanza kupungua na sasa wanajaribu kujenga hoja zenye ushawishi kwa mawaziri na Serikali ili miradi kadhaa katika majimbo yao iweze kukamilika.

Wiki hii Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, ziliwasilisha bajeti zake huku wabunge wakilalamikia upungufu wa fedha katika baadhi ya miradi wakiweka wazi kwamba utawakosesha kura katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, wabunge walikosoa mfumo na sera ya elimu ya mwaka 2014 wakidai ni kikwazo kwa maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Waliishauri Serikali kufanya mabadiliko katika mfumo mzima wa elimu vinginevyo taifa linatengeneza bomu la baadaye.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Jumanne Kishimba (CCM), alikosoa muda mrefu unaotumika kufundisha watoto hadi kuwa watu wazima kwamba unawafanya wengi kubaki wavivu hata wanapohitimu vyuo vikuu.

“Suala la mfumo wa elimu tunayoenda nayo ni bomu, elimu ya Tanzania ni kama kifungo cha maisha, kuanzia miaka 18 ya mtu kufanya kazi anakuwa shuleni hadi miaka 25 na akitoka huko na digrii yake, hapati kazi, hajui kulima wala kufuga na hiyo digrii hawezi kuweka bondi ya mkopo benki wala pharmacy (duka la dawa). “Hivi ni utafiti gani wa kisayansi unaosema ubongo wa binadamu kila mwaka usome darasa moja, kwanini tusifanye mwaka mmoja mtu asome madarasa matatu,” alihoji Kishimba.

Naye Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Suzan Lyimo, alitishia kuondoa shilingi katika mshahara wa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kama hataweka wazi ni lini madeni na malimbikizo ya walimu zaidi ya Sh bilioni 60 yatalipwa.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara, aliiponda akisema haina mashiko kwa sababu madeni hayo yataendelea kulipwa kadiri fedha inavyopatikana.

Licha ya kuombwa na wabunge kadhaa wa CCM arudishe shilingi, Suzan, aligoma huku akisisitiza wizara itoe muda maalumu lini madeni hayo yataanza kulipwa.

WIZARA YA MAJI

Katika mjadala wa Wizara ya Maji, wabunge wengi waliitaka Serikali kutekeleza azimio la Bunge lililotolewa kwa miaka mitatu mfululizo la kuongeza tozo katika kila lita moja ya petroli na dizeli.

Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge, aliitaka Serikali kuondoa kodi katika mitambo ya maji na kuruhusu sekta binafsi zishiriki kutatua kero ya maji nchini.

“Naomba wabunge tusimamie maamuzi yetu, maamuzi yetu tuyalinde kwa wivu, tunajenga nyumba moja tusigombane na Serikali.

“Hii tozo ya shilingi 50 tulikubaliana miaka mitatu iliyopita, kama Serikali haitaki basi ije na mbadala mwingine wa kupata fedha za maji, tutaondoa azimio hilo, hizi ndizo kura za uhakika,” alisema Chenge.

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Esther Bulaya, alimtetea Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, kwamba si kosa lake miradi ya maji kutokukamilika isipokuwa Serikali ndiyo inachelewesha fedha za bajeti.

“Niwaombe wabunge, tusimshambulie Mbarawa tuibane Serikali ipeleke fedha katika miradi, kwa mfano Bunda kuna mradi una miaka 10 haujakamilika, Mamlaka ya Mji wa Bunda hawana ruzuku ya Serikali, watumishi wamebaki na msongo wa mawazo kwa sababu mishahara hamuwaongezei lakini vifaa vya kutekeleza miradi hamuwapi,” alisema Bulaya.

Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), alipinga ongezeko la tozo ya Sh 50 katika dizeli na petroli akisisitiza kuwa Serikali inakwamisha miradi kwa kutokutimiza wajibu wake wa kupeleka bajeti kama ilivyoidhinishwa na Bunge.

Alisema haoni sababu ya ongezeko hilo kwa sababu hata bajeti iliyopita ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 imetekelezwa kwa asilimia 51 huku fedha hizo zikitoka katika Mfuko wa Taifa wa Maji na wafadhili lakini Serikali haikutoa ruzuku kama ilivyotakiwa.

Naye Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje (CCM), aliilalamikia Wizara ya Maji na Umwagiliaji kutotekeleza miradi ya maji katika jimbo lake huku akihofia kunyimwa kura katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Alisema kutokamilika kwa miradi ya maji katika jimbo lake kunahatarisha kura zake.

Alisema maji ni siasa na kwamba Serikali ikishaahidi kuchimba kisima na mradi ukashindwa kutekelezwa hiyo ni siasa.

“Na uchaguzi ni mwaka kesho, tutapata shida. Naomba miradi hii itekelezwe ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.

“Katika jimbo langu maji yana chumvi lakini sina maana Profesa Mbarawa ayabadilishe yawe ya baridi bali atekeleze miradi ya maji waliyoahidi kuifanya.

“Mwaka 2008 nikiwa mbunge Serikali iliahidi kuchimba visima sita katika jimbo langu, lakini hakuna kilichofanyika,” alisema.

Mbunge huyo aliyezungumza kwa hisia alisema kuna miradi minne inaendelea hadi sasa ikiwa ni miaka mitatu tangu ianze kutekelezwa lakini haijakamilika.

Lubeleje alihoji kama Serikali haiwalipi wakandarasi miradi hiyo itakamilikaje?

Pia alisema kuwa wananchi wa vijiji vinavyotekelezwa miradi hiyo wanaendelea kupata shida ya maji na kuitaka Serikali kuwalipa wakandarasi ili miradi ikamilike.

“Nakuomba waziri ufike ueleze kwanini miradi hii haijakamilika hadi leo? Mimi nimeshaeleza nimechoka.

“Na siwezi kukosa kura katika vijiji hivyo kwa sababu miradi haikamiliki ufike wewe mwenyewe kuwaeleza wananchi kwanini haijakamilika,” alisema.

Pia alisema katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali iliahidi kuchimba visima jimboni kwake lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika ingawa mhandisi wa maji wa wilaya hiyo alishatoa orodha ya visima vitakavyochimbwa.

Alihoji Serikali fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo katika vijiji zaidi ya nane zilikwenda wapi.

Naye Mbunge wa Ulyankulu, John Kadutu (CCM), alitishia kufanya vurugu endapo Serikali haitaondoa kero ya maji katika jimbo lake.

Kadutu ambaye jimbo lake lipo Shinyanga, alisema kwa muda mrefu limekuwa halipewi kipaumbele ingawa lipo karibu na mradi wa maji kutoka Mto Malagalasi unaoelekezwa Kaliua na Urambo mkoani Tabora.

“Waziri na wataalamu mliopo hapa hebu fanyeni mnavyoweza, hivi sisi tutatengwa hadi lini? Sisi si wakimbizi kama hamtaki kutupa tawala za mikoa tupeni maji, wataalamu mnisikie tutaleta vurugu hata wao hawatakanyaga huko,” alisema Kadutu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles