23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mwili wa Mengi kuwasili Jumatatu

AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

MWILI wa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, aliyefariki dunia juzi Dubai, unatarajia kuwasili nchini keshokutwa. 

Akizungumza nyumbani kwa marehemu Dar es Salaam jana, Msemaji wa familia hiyo, Michael Ngalo, alisema mwili huo unatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8:30 mchana na ndege ya Shirika la Emirates kisha utapelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo wakati ukisubiri taratibu za kuagwa Jumanne ya wiki ijayo.

Ngalo ambaye ni Mwanasheria wa familia ya Mengi, pia alisema mwili huo utazikwa Alhamisi ya wiki ijayo nyumbani kwake Machame, Kilimanjaro.

“Jumanne mwili utaondolewa Lugalo utapelekwa Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kuagwa, baada ya kuagwa utarudishwa nyumbani na Jumatano asubuhi na mapema tarehe saba utachukuliwa  na kupelekwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kusafiri kwenda Moshi,” alisema.

Ngalo alisema baadaye mwili huo utashushwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kupelekwa nyumbani kwake Machame kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi asubuhi.

“Ibada ya mazishi itafanyika katika Kanisa la KKKT Kisereni na baada ya ibada mwili utarudishwa nyumbani kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika siku hiyo hiyo,” alisema.

Mbali na kutolewa kwa ratiba hiyo, viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali wameendelea kuwasili nyumbani kwa Mengi kwa ajili ya kuwafariji wafiwa miongoni mwao akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyewaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika msiba huo.

“Mengi ni mzee wetu alikuwa na roho nzuri na pia alishiriki katika maendeleo ya Dar es Salaam kwa kutoa ajira kwa watu wengi kupitia kampuni zake, wakazi wa Dar es Salaam naomba tumpe heshima yake kama alivyotuheshimu kwa kujitokeza kumsindikiza katika safari yake ya mwisho,” alisema Makonda.

Naye Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema ili kumuenzi Mengi, wananchi wanapaswa kuyaishi mambo aliyokuwa akiyafanya.

“Mema yake ya jana, leo na kesho yataishi, naomba Watanzania tutumie msiba huu kwa kutumia kauli ya Mengi ya kwamba maisha yapo katika ndimi zetu,” alisema Mbatia.

Viongozi wengine waliofika nyumbani kwa Mengi ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, aliyekuwa akilia kwa uchungu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles