COLOMBO, Sri Lanka
SERIKALI imesema idadi ya vifo vya watu katika mashambulio ya kujitoa muhanga yalitokea juzi kanisani na hoteli za fahali imeongezeka na kufikia 290.
Mbali na taarifa hiyo maofisa hao wa serikali walisema mashambulio hayo yaliratibiwa na mitandao ya ugaidi ya kimataifa.
Walilishutumu kundi dogo la wapiganaji wa Jihadi linaloitwa National Towheed Jamath kuhusika na mashambulio hayo yaliyosababisha pia watu 500 kujeruhiwa.
Mpaka mapema jana hakuna hata kikundi kimoja kilichojitokeza kudai kuhusika nayo na polisi wanawashikilia watu 24 .
“Hatuwezi kuamini mashambulio haya yamefanywa na kundi la watu waliopo nchini humu,” alisema msemaji wa Baraza la Mawaziri, Rajitha Senaratne.
“Kusingekuwapo na matandao wa kimataifa mashambulio haya yasingefanikiwa,”aliongeza msemaji huyo.
Kwa upande wake Rais wa nchi hii, Maithripala Sirisena, ameziomba jumuiya za kimataifa kusaidia kuwasaka waliopanga na kufanya mashambulio hayo.
“Taarifa za intelijensia zinaonyesha kuna mtandao wa ugaidi kutoka nje ya nchi ambao umeshirikiana na wa hapa. Hivyo rais anaomba ushirikiano na mataifa ya nje,”ilieleza taarifa ya ofisa ya rais.
Mapema juzi, Waziri Mkuu, Ranil Wickremesinghe, alieleza kuwa awali kulikuwapo na taarifa kwamba mashambulio hayo yangefanyika, lakini taarifa hizo hazikuchukuliwa kwa uzito.
Katika hatua nyingine, Rais Maithripala Sirisena ametangaza hali ya dharura kuanzia jana usiku hadi leo.
Taarifa ya Kitengo cha Habari cha Serikali ilieleza kuwa Serikali imeamua kutangaza sheria inayolenga kuzuia ugaidi ambayo itaanza kuheshimiwa kuanzia jana usiku.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa hatua hiyo itahusiana tu na shughuli za kuzuia ugaidi, na haitaingilia uhuru wa watu wa kutoa mawazo yao.
Msemaji wa serikali mjini hapa, Rajitha Senaratne alisema serikali ya Sri Lanka inaamini kundi lenye itikadi kali la lijulikanalo kama Nationa Thowheeth Jama’ath (NTJ) ndilo limefanya shambulio hilo na ameongeza kuwa uchunguzi ulikuwa ukifanyika kuangalia iwapo kundi hilo lilipata msaada kutoka nje ya nchi.
Nyaraka zilizoonwa na Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) zinaonyesha kuwa polisi ilitoa onyo Aprili 11 mwaka huu kwamba shirika la kijasusi la nchi ya kigeni lilikuwa limeripoti kwamba NTJ ilikuwa ikiandaa njama ya kushambulia makanisha na ubalozi wa India.
Hata hivyo hakuna mengi yanayojulikana kuhusu kundi la NTJ, ambalo siku zilizopita lilihusishwa na kufanya uharibifu kwenye sanamu za madhehebu ya Buddha.
Chanzo cha habari kutoka jeshi la polisi kimeeleza kuwa watu 24 waliokwisha kukamatwa wakishukiwa kuhusika na mashambulio ya siku ya Pasaka wana uhusiano na kundi hilo lakini hakufafanua zaidi.
Kutokana na shambulio hilo la umwagaji mkubwa wa damu, Sri Lanka iliifunga mitandao mingi ya jamii, ikiwamo Whatsapp na Facebook, hatua inayodhihirisha kupungua kwa imani katika makampuni hayo mawili makubwa ya Marekani, kuweza kuchuja taarifa za uchochezi.
Mitandao hiyo miwili pamoja na Instagram imeshutumiwa kusambaza habari za uongo. Mtandao wa twitter haukuathiriwa na hatua hiyo.
Ghasia za dini
Serikali ilihofu kuwa kuenea kwa ujumbe wenye hasira kungechochea ghasia zaidi katika kisiwa hiki ambacho wakazi wengi wa Wabuddha, lakini pia yakiwapo makundi ya makubwa ya Waislamu, Wakristo na Wahindu.
Hii si mara ya kwanza kwa Sri Lanka kuifunga mitandao ya jamii. Machi 2018 serikali ya nchi hiyo iliizuia kwa wiki nzima mitandao ya Whatsapp, Facebook na mitandao mingine, kwa hofu kwamba ilikuwa ikiendeleza kampeni ya chuki dhidi ya Waislamu katika jimbo la katikati mwa nchi hiyo