KAMPALA, Uganda
MBUNGE wa Jimbo la Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, amekamatwa tena baada ya mashabiki wake kupambana na polisi wakipinga kufutwa matamasha yake ya Pasaka yaliyokuwa yafanyike mjini hapa na katika miji ya Arua na Lira.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, hali ya taharuki ilianza baada ya polisi kuzuia msafara uliokuwa ukiongozwa na mbunge huyo kwenda katika ufukwe wa One Love uliopo eneo la Busabala.
Taarifa za gazeti hilo zilieleza kuwa baada ya Bobi Wine kukamatwa alitumbukizwa ndani ya gari la polisi na kupelekwa mahali kusikojulikana .
Mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa kabla ya ya mbunge huyo kukamatwa polisi wa kutuliza ghasia walivunja kioo cha gari lake na kumvuta nje, lakini mwimbaji Nubian Li ambaye alikuwa naye hakukamatwa.
Mbali na mbunge huyo, waandaaji mashuhuri wa matamasha ya muziki Andrew Mukasa na Abbey Musinguzi maarufu kama Abtex ambao waliandaa tamasha hilo la Bobi Wine nao walikamatwa jana.
Taarifa zinaeleza kuwa wawili hao walikamatwa mapema jana na kuzuiliwa katika gari moja la maofisa wa polisi kabla gari hilo kuondoka nao.
Kukamatwa kwa mbunge huyo ni baada ya Rais Yoweri Museveni kusema kuwa hatakubali matamasha ya muziki uliojaa siasa na kuonya kwamba katika siku zijazo hakuna mtu atakayefidiwa kwa matamasha ambayo yamefutiliwa mbali kutokana na siasa.
Rais huyo alitoa onyo hilo wakati wa mkutano na wanachama na waandaaji matamasha ya muziki nchini hapa na wamiliki wa maeneo ya kumbi za muziki katika Ikulu ambako alitoa Sh bilioni mbili za Uganda kama fidia ya hasara waliyopata baada ya maofisa wa polisi kufutilia mbali matamasha ya muziki wa Bobi Wine.