29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

‘Farasi’ wa Rais Magufuli wamegoma kunywa maji

Na. M. M. Mwanakijiji

NINA uhakika Rais Dk. John Magufuli, halali vizuri na hata akilala hulala kwa kushtukashtuka. Na kama huwa anaota ndoto basi ndoto zake zimejaa maruweruwe. Zinatisha, zinashtua na zinaumiza. Ni zile ndoto ambazo mtu akishtuka anajikuta amelowa jasho hadi kwenye ndevu na anatamani bilauri ya maji baridi kuzimulia. Ni zile ndoto ambazo mtu huogopa hata kuzisimulia.

Ukimsikiliza Rais Magufuli mara kwa mara akinung’unika na kuhuzunika kuhusu mambo aliyoyakuta ndani ya Serikali utakubaliana na mimi kuwa kuna hatari ya kuwa maji yamezidi shingo. Sipendi tena, sitaki kusikia Rais Magufuli anaanza kuzama. Inapofika mahali hadi Rais anakwenda kufanya mwenyewe ukaguzi wa miradi midogo kama ya kupaka rangi ndege, basi bila ya shaka farasi wake wamegoma kunywa maji.

Nilipokuwa kijana mdogo kule Matimila Songea, babu yangu alinisimulia kisa kimoja ambacho kilikuwa ni cha kunifundisha maadili ya kufanya kazi kwa kujituma, badala ya kusubiri mtu anifuate kila baada ya dakika kuniuliza kama nimefanya nilichotakiwa au la. Kilikuwa ni kisa ambacho baadaye ukubwani nilikuja kusikia hata kwenye nchi nyingine (kimefanana). 

Simulizi la jamaa mmoja aliyekuwa na farasi wake wengi ambao alikuwa anawatumia kwa shughuli zake mbalimbali za nyumbani na kwa usafiri. Alikuwa anawalisha farasi wale vizuri na kuwatunza vizuri. Aliwajengea banda zuri ambamo walikuwa wanalala na zizi lao lilikuwa ni mojawapo ya mazizi bora kabisa ya farasi.

Alikuwa pia anawatumikisha kweli kweli. Farasi – alisema mzee yule – walikuwa ni wanyama wa kazi. Aliwatumia kusafirisha mizigo kwenda sehemu mbalimbali, pia aliwatumia kwa kufanya kazi za kilimo cha maksai. Wakati mwingine mzee alikuwa anajikuta anachanganyiwa katika shughuli zake – labda sababu ya uchovu au mambo mengi kichwani – na kujikuta akiweka mkokoteni mbele ya farasi badala ya nyuma yake na farasi wakashindwa kwenda hadi mtu amshtue kuwa ameuweka mkokoteni vibaya!

Wakati mwingine hata hivyo mzee yule alipata shida ilipokuja zamu ya kuwapa maji farasi wake. Kuna siku moja – alinisimulia babu yangu – mzee alipata shida kuwapa farasi maji ya kunywa. Baada ya safari ndefu porini, mzee alihisi kuwa farasi wana kiu na aliamua kuwapeleka kwenye kijito cha maji. 

Farasi walikwenda vizuri tu hadi kwenye kijito kile, lakini hawakutaka kunywa maji yale. Mzee aliwavuta kwa kutumia rijamu na kuwachapa mijeledi viumbe wale wa Mungu lakini farasi waligoma katakata kunywa maji ya kijito kile. Mzee hadi presha ilianza kumpanda na hakuelewa kwanini hawakutaka kunywa maji yale.

Hakutaka kuendelea na safari bila farasi kunywa maji! Alipita bi kizee mmoja pale na kumkuta anahangaika kuwalazimisha kunywa maji yale. Yule bi kizee kumbe alikuwa anamwangalia kwa muda mzee wa watu anavyohangaika kuwanywesha “maji” farasi wake. 

Bi kizee baada ya masabahiano alimwambia mzee yule “unajua unaweza kuwapeleka farasi kwenye maji lakini huwezi kuwalazimisha kunywa maji!” Alimaanisha tu kuwa farasi wakiwa kweli na kiu hawatahitaji kulazimishwa kunywa maji. 

Wanachohitaji ni kujua maji yapo na wao wakiwa na kiu watakunywa! Mzee alimsikiliza ajuza yule na kuamua kuendelea na safari; na kweli farasi walifika salama walikokuwa wanakwenda na aliwawekea maji bandani na baada ya muda akakuta farasi wamekunywa maji yote ya kwenye ndoo!

Rais Magufuli anakabiliwa na tatizo kama hili. Anajitahidi sana kuwafanya ‘farasi’ wake wanywe maji, lakini inaonekana kama kuna mgomo fulani hivi. Hivi ni viongozi gani hawaelewi matarajio ya Rais ni nini? Kwanini Rais azungumzie mapato ya Uwanja wa Taifa na mgawanyo wake; Kwanini Rais ndiye afikirie kutoa msaada kwa watu kama kina Peter Tino na watu wengine wengi ambao tunaona anawasaidia? Inakuwaje Rais ndiye aende Magomeni kukagua ujenzi wa nyumba na kugundua kuna tatizo? Yaani, inafika mahali Rais anaonekana ni ‘micro manager’ wa aina fulani hivi.

Inawezekana watendaji wake hawajui wanatakiwa kufanya nini? Fikiria kwa mfano mojawapo ya mambo yanayotia aibu sana na kudhalilisha Jeshi la Polisi ni kuwa hawana uwezo, weledi na mbinu za kutoa ulinzi kwenye kijimkutano kidogo cha ACT-Wazalendo! 

Yaani, miaka karibu 60 ya Uhuru bado hatuna chombo kinachoweza kusema “Zitto, mna haki ya kufanya mkutano wenu, tumesikia kuna watu wanataka kufanya vurugu na sisi tupo kuhakikisha mnafanya mkutano wenu salama!” Yaani ikibidi hata kuleta ‘batalioni’ nzima ya FFU kuwapa ulinzi; badala yake farasi wamegoma! Wanatafuta njia ya mkato – futa mkutano!

Labda farasi hawa wanafikiria wanamfurahisha Magufuli. Upande mmoja unaweza kuona ni kama utani, lakini inawezakana ni kweli. Kuna wanaokumbuka wiki chache tu nyuma Rais Magufuli – masikini wa Mungu – alijikuta analalamikia utekwaji wa Mohammed Dewji; alilinyooshea Jeshi la Polisi jinsi gani lilishindwa hata kutoa maelezo nini kimefuatia. Sasa tukifuata mantiki, inawezekana kweli jeshi letu si tu halina uwezo wa kulinda “vimikutano” kama vya kina Zitto, bali halina weledi wa kufuatilia tukio zito kama la kutekwa kwa Mo! Hili hata mimi lingenikosesha usingizi!

Swali kubwa ni Rais Magufuli afanye nini? Kama farasi wake wanamgomea hivi kiasi kwamba inamlazimu yeye mwenyewe, makamu wake au waziri mkuu kwenda kufuatilia? Inanikumbusha kisa kingine – nilichowahi kukisimulia hapa huko nyuma – cha jamaa waliokuwa wamelazimika kulisukuma gari kulitoa kwenye matope. 

Baada ya gari lao zuri kukwama kwenye matope licha ya kuwa ni 4 x 4, walijikuta wanahitaji kulipa nguvu ya ziada ili litoke. Baada ya jitihada zao zote walifanikiwa kulikwamua kwenye matope. Gari lilikuwa limechafuka nyang’anyang’a na harufu ya moshi ilikuwa kila upande. 

Cha kushangaza baada ya kulisafisha dereva akawaambia waendelee kulisukuma! Gari lilikuwa linawaka na mifumo yake mbalimbali ilikuwa inaweza kufanya kazi; lakini dereva kwa sababu hakutaka likwame tena akaamua abiria wake walisukume!

Rais Magufuli asije akajikuta anakosa usingizi na kukabiliwa na matatizo ya moyo au msongo wa mawazo kwa sababu anawaza sana juu ya kulisukuma gari hili la Tanzania. Labda umefika wakati – sijui kwa uhakika – anapaswa kuangalia ni nini kinaweza kufanya gari hili liende bila kupewa maelekezo toka “juu”. Kwamba kila mtu anajua wajibu wake chini ya Katiba na akautekeleza bila kuhofia kutumbuliwa, kuudhi mtu au kuonekana haendani na “juhudi”.

Ngoja niwaulize kitu; wote tushasahau mambo ya ‘madawati’ kwa vile Rais ‘kasahau’! Wote wamesahau masuala ya usafi kwa vile tu Rais hafanyi tena usafi; wote wamesahau mambo mengi ambayo Rais aliyaanzisha na sasa wanasubiria kudakia tu atakachosema Rais. 

Halafu akija kuwatumbua watasema Rais mkali sana! Fikiria hili la kupaka ndege rangi; yaani wapo watu kabisa wanafikiria wanaweza kufanya hili na hadi taarifa zinamwendea Rais Ikulu na yeye apige mkwara! Katibu Mkuu wa Wizara yuko wapi?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles