21.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

IBADA YA PASAKA: Maaskofu watuma ujumbe wa amani

*Mfumo wa elimu wachambuliwa, watoa hadhari

WAANDISHI WETU-DAR/MIKOANI        

ASKOFU wa Jimbo la Katoliki la Kayanga, Almachius Rweyongeza amesema amani ni kazi ya haki wala si matokeo ya vita.

Pia amesema amani si kutokuwa na vita bali ni matokeo ya haki, hivyo Serikali ina wajibu wa kuilinda amani hiyo nchini.

Askofu Rweyongeza alitoa kauli hiyo jana wakati akihubiri katika misa ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu George Jimbo Katoliki la Kayanga mkoani Kagera.

Pamoja na mambo mengine, Askofu Rweyongeza alisema ujumbe wa salamu ya Yesu kwa  e wote wanaosherekea Sikukuu ya Pasaka ni amani.

Huku akinukuu baadhi ya vifungu vya biblia, aliwataka waumini kutathimini maisha yao kama yanaendelea kuwa na amani ya Yesu Kristo.

 “Tunaweza kusema Pasaka ni sherehe ya kutakiana amani, Yesu salamu yake ni amani iwe kwenu, tunaposherekea Pasaka mtakie mwenzako amani.

“Amani ni kazi ya haki wala si matokeo ya vita na utawala wa mabavu, amani si kutokuwa na vita. Amani ni matokeo ya haki.

 “Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa, hujengwa siku kwa siku, amani ni hatua endelevu, aidha madam utashi wa binadamu ni dhaifu na umejeruhiwa na dhambi, kuleta amani kunadai siku zote kila mtu azitawale tamaa zake na Serikali ijihusishe katika kulinda amani.

 “Pasaka ni wakati wa kufanya tathimini ya maisha yako, mtu binafsi, familia, jumuiya, kanisa na taifa kwa ujumla, tufanye tathimini juu ya maisha yetu kama yanaendelea kuikumbatia amani ya Kristo ama lah!

“Mti hauli matunda yake wenyewe bali huliwa na wengine. Basi na sisi tujitoe katika kutoa matunda au karama zetu kuwanufaisha wengine. Hizi karama tumepewa bure,”alisema.

Vilevile alisema maendeleo bila dhamira safi huharibiwa na kubomoka kwa muda mfupi sana.

“Maendeleo ya watu hayajengwi kutokana na fedha wala vitu na teknolojia bali kwa dhamira njema ya kuwatumikia watu,”alisema.

Askofu Rweyongeza alizungumzia pia mfumo wa elimu nchini, akisema mtu akitaka kuangamiza taifa lolote hahitaji kutumia nguvu za nyuklia bali atoe elimu duni.

“Kuchezea elimu ni kuangamiza taifa. Watu wangu wameangamia kwa kukosa maarifa (Kitabu cha Hosea).

“Je, mfumo wetu wa elimu ni kama biashara? Kubadilishwabadilishwa kwa sera na mfumo wa elimu bado hatujui tunachokitaka kwamba taifa letu liweje? Mwelekeo wetu ni upi?

“Kila mara tunashuhudia mitaala yetu imekuwa ikibadilishwabadilishwa bila kuwapo umakini wala utafiti wa kina. Msemo wa kilatini wa “Non scholae sed vitae discimus” ni wa maana sana.

“Tunahitaji elimu bora ya kutatua maisha ya kila siku nje ya darasa, tunasoma kwa ajili ya maisha na si kufaulu mtihani.

“Mfumo wetu wa elimu hautayarishi vijana wetu kuwa rasilimali imara katika maisha bali wa kuliangamizi taifa letu. 

“Kulegeza vigezo vya ufaulu kinyume na viwango vya  maitaifa hakuleti tija. Ubora wa elimu si kulegeza ufaulu ili kuongeza idadi ya wafaulu,”alisema.

Alisema hatua ya wanaopata viwango vya chini vya ufaulu ndiyo wanapelekwa katika vyuo vya walimu na kwamba matokeo yake ni kuzalisha wezi, watu wasiokuwa na dira na hatimaye kuchangia kujaza magereza.

“Kama mwalimu ni mbabaishaji akaanza kuchekwa na wanafunzi wenye akili ya kuzaliwa, ataamua kuwachapa viboko.

 “Msemo wa mwanafalsa  Albert Einstein una maana kubwa sana kwamba; ‘Dunia itaharibiwa si na watenda mabaya bali kwa ukimya wa watu wema,”alisema.

Askofu Rweyongeza alihoji somo la dini na maadili yanapewa kipaumbele  huku akisema hakuna kosa kama kupuuza somo la dini.

“Somo la dini  shuleni liende sambamba na masomo dunia mengine ili watoto wetu waendane na tabia njema maishani mwao.

“Mafisadi, wabaguzi, wategeaji na watoro kazini, wauwaji, wezi nk, wanatokana na elimu isiyokwenda sambamba na maadili.

“Wanaoapa eti Mungu nisaidie na huku matendo yao ni kinyume na hayo ndiyo matokeo ya uonevu, ubadhirifu nk,”alisema.

Alishauri mtu aliyeshindwa somo la dini asiajiriwe na kabla ya kuajiriwa adhaminiwe na kiongozi wake wa dini, vinginevyo serikali itaendelea kuwaajiri wahalifu.

“Kutokariri darasa kunazaa watoto wasiokuwa na maarifa. Vijana wanatahiniwa kwa kufanya mitihani ya ‘multiple choice’ ambayo ni ya kubahatisha. Haiwajengei tu kutojua lugha ya kujieleza bali pia kutokuwa na uwezo wa kuchambua mambo.

“Kwa nini serikali inazuia shule ambazo haizigharimikii kutokaririsha wanafunzi ili wakomae katika elimu?

“Hatuna budi kujitathimini upya kuhusu ubora wa elimu, tunahitajika mjadala wa  taifa kuhusu elimu ya vijana. Hili ni jambo lisiloepukika na kwa haraka sana.

“Na Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa alikuwa sahihi kabisa aliposema kunahitajika mjadiliano ya  taifa kuhusu mwenendo wa elimu nchini. Tunamuunga mkono,” alisema Askofu Rweyongeza.

Ibada hiyo ya  taifa  pia ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti na wakuu wa wilaya za mkoa wa Kagera.

ASKOFU SHOO

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, akihubiri katika ibadala ya Pasaka mjini Moshi, alisema duniani leo wapo watu ambao wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kuuficha ukweli, bila kujua kuwa ukweli una asili ya kutofichika.

Aliwataka wakristo kama wafuasi wa Yesu Kristo   kuukumbatia ukweli katika mambo yote.

“Ndugu zangu tunaweza kusema tunaipenda nchi yetu, lakini swali kubwa kwetu ni je, tunayo ujasiri wa kujitoa kweli kweli hata kiasi cha kutoogopa vipingamizi na vikwazo vya hatari?

“Ujasiri peke yake bila upendo unaotoka moyoni, huzaa ukatili na ujasiri usiokuwa na upendo huzaa hofu na inapotokea kusimama kwa ajili ya wengine kwa manufaa ya wengine upendo bila ujasiri unabakia kuwa upendo wa mdomoni tu.

“Hata leo baadhi ya wakristo tunaweza kusema tunampenda Yesu lakini inapokuja saa ya kusimama kama Shahidi wa Kristo, kuitetea familia yako, Kanisa na hata nchi yako unaingia mitini,  kina mama wale hawakusaliti, walisimama kweli kweli na upendo wao huu wa dhati,”alisema Dk. Shoo.

Askofu huyo alisema ujasiri wa kujitoa kwa ajili ya wengine na familia, Kanisa na nchi unahitaji watu kama hawa wenye upendo wenye ujasiri na upendo wa kujitoa kwa ajili ya wengine.

“Wakati wa Yesu, maaskari waliokuwa wakilinda kaburi, walipewa fedha nyingi   kuuficha ukweli lakini haikuwezekana na leo wapo watu ambao wanajaribu kuwazuia wakristo kutangaza habari za Yesu na kulizuia kanisa kufanya kazi ya kitume, bila kujua kuwa tendo hilo ni la Mungu mwenyewe.

“Kulifanyika jitihada nyingi kwa ajili ya kuficha ukweli wa Yesu kufufuka, maaskari walioshuhudia lile tetemeko na kushuhudia Yesu kufufuka walikuwa  na hofu kubwa, walipewa fedha nyingi na wale wakuu wao, ili eti waseme Yesu hakufufuka bali wanafunzi wake walikuja kumuiba usiku wakiwa wamelala.

“Lakini haikuwezekana kuuficha ukweli huo, habari za kufufuka kwa Yesu zikaenea na tena mbaya zaidi hata habari kwamba wakuu waliwapa fedha wale askari ili wanyamaze nazo zikaenea.

“Yamkini duniani wapo leo pia watu waovu wanaotumia nguvu nyingi kuuficha ukweli, wanasahau kuwa ukweli una asili ya kutofichika daima, tujifunze kwa wale kina mama waliokwenda  kaburini.

“Ukweli na upendo wa dhati ndiyo uliyowafanya kina mama waliokwenda kaburini wadiriki hata kuhatarisha maisha yao.

“Leo hii tunapoadhimisha sikukuu hii ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo, tujifunze jambo kwa kina mama hawa waliokwenda kaburini walikuwa na upendo wa kweli, ambao ni tofauti na upendo wa unafiki.

“Upendo wa kweli hutoka moyoni na hutupa ujasiri, hutupa nguvu ya kufanya mambo yale magumu na hata yale yanayoonekana hayawezekani na ya hatari,”alisema Askofu Shoo.

Askofu Shoo pia alisema mapatano ya msingi yaliyomo kwenye Katiba yakionekana ni sawa na kipande cha karatasi huo utakuwa mwanzo wa kuelekea mahali ambako si kuzuri.

“Kuna mapatano ambayo tumewekeana kama nchi, tukisema mapatano haya yatalindwa na Katiba basi ni lazima tuyaheshimu, tuyajenge na kuyalinda kama tunataka kutembea pamoja.”alisema.

ASKOFU NZIGILWA

Akiongoza ibada hiyo ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa aliwakumbusha waumini kwamba kifo si mwisho wa maisha yao bali kuna maisha mengine baada ya   duniani.

Askofu Nzigilwa alisema Sikukuu ya Pasaka ni kumbukumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo ambaye kupitia kifo chake kilichotokea zaidi ya miaka 2000 iliyopita, ulimwengu ulikombolewa.

“Kifo si mwisho wa maisha ya Mkristo na kaburi si nyumba ya milele ya Mkristo kama tunavyoambiwa. Yesu alisema anakwenda kwa baba kuandaa makao ili atakapokuwa nasi tuwepo.

“Sasa yeye hayupo tena kaburini, alifufuka. Alishinda kifo na mauti, ndiyo maana leo tunakumbuka ufufuko wake. Hilo ndiyo fumbo la imani yetu Katoliki,”alisema Askofu Nzigilwa.

Pia aliwataka wakristo kuwa wakarimu kwa watu wenye shida kwa kujitoa kusaidia wengine hata kwa vitu ambavyo wanavihitaji katika maisha yao.

“Pasaka itusaidie kutoka kwenye maisha ya zamani ya dhambi na kuanza maisha mapya yanayompendeza Kristo mfufuka,”alisema.

ASKOFU MALASUSA

Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa akihubiri   katika Usharika wa Azania Front  Dar es Salaam, aliwataka wakristo kuwa mstari wa mbele kuhamasisha amani huku akiwataka viongozi kujali wengi kuliko matakwa yao.

Pia alishauri kuwe na vyombo vya kuleta matumaini kwenye jamii badala ya kukatishana tamaa na kukimbilia mambo yanayoashiria uvunjifu wa amani.

Askofu Malasusa alisema haipendezi kwa wakristo kuwa mawakala wa kusambaza habari mbaya na kuzungumzia kuhusu upungufu pekee wakati yapo mazuri wanayofanyika.

“Wakristo tuna kila sababu ya kuwa vyombo vya kuleta matumaini katika jamii, si kukatishana tamaa wala kuzungumza mambo yasiyofaa, tunapotoka hapa kusherehekea Pasaka tupeleke ujumbe kwenye jamii kwamba Mungu yupo na anaishi.

“Hilo tunatakiwa kulionyesha kwa vitendo kwa kuonyesha upendo kwenye maisha ya wengine kwa kuwasaidia na kuwajali kwa dhati, hii ni sikukuu kubwa kwetu wakristo,”alisema Askofu Malasusa.

Aliwataka viongozi wote nchini kuwa na upendo huku wakitangulia kuwapenda na kuwajali wengine kabla ya kutanguliza matakwa yao.

Askofu Mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Kitete Christian akihubiri katika kanisa hilo  mjini Tabora, alisema  Sikukuu ya Pasaka inawakumbusha wakristo jinsi Yesu alivyokufa na kufufuka.

Alisema kufufuka kwa Yesu Kristo ni ishara tosha kwamba kifo chake ni fidia ya hukumu ya dhambi za wanadamu wote.

Alisema hukumu ya dhambi za wanadamu ilifanywa na Mungu mwenyewe kama Jaji Mkuu na kumtoa mwanawe Yesu Kristo ili afe kwa kumwaga damu yake   msalabani.

Alisema maandiko matakatifu katika kitabu cha Warumi 6:23 yanasema kuwa ‘kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti’,  hivyo mtenda dhambi yeyote alipaswa kuhukumiwa kwa matendo yake maovu.

Alisisitiza kuwa kupitia msalaba na kaburi, Yesu alilipa fidia ya hukumu ya dhambi iliyotolewa na Mungu ila kwa kumwaga damu yake alifuta hukumu hiyo kwa kila mtenda dhambi atakayekubali kumpokea kuwa bwana na mwokozi wa maisha yake.

‘Watanzania na dunia nzima tukubali kumpokea Yesu Kristo, tumwamini na kumpa nafasi katika maisha yetu ili tuwe salama na hata siku ya kuondoka duniani twende mbinguni kwa mlango wa Yesu Kristo,” alisema.

Aliitaka jamii kuendelea kumwabudu, kumtukuza, kumuadhimisha na kushikamana kupitia sikukuu hii ili huyo aliyefufuka ayafufue yote yaliyokufa katika maisha yao, familia zao, huduma zao na maisha yao kwa ujumla.

ASKOFU KINYUNYU

Askofu wa Dayosisi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Dodoma, Amon Kinyunyu aliwataka wakristo kutokana tamaa  wanapokutana na changamoto katika maisha yao.

 “Kila Mkristo anatakiwa kujiuliza afanye nini juu ya changamoto anazokutana nazo, ni nani atakayeniondolea changamoto hizi.

“Ukweli ni kwamba suluhisho la kweli lipo kwa Yesu pekee, ukikabiliwa na changamoto katika maisha yako zikabidhi kwa Yesu kwani alikufa kwa ajili yetu, hivyo Bwana atakuonyesha namna ya kukabiliana nazo,”alisema askofu Kinyunyu.

Alisema Yesu alitimiza ya Mungu ya kuukomboa ulimwengu na kuwa Pasaka ni ukombozi wa dhambi kutoka utumwani walikokuwa wanatumika wanadamu.

“Kufufuka kwake ni sababu ya kutufanya tuamini kuwa tukifa tutafufuka, tusisikitike juu ya kifo, bali tutambue ni kulala na mwishowe tutafufuka kama alivyofufuka Yesu.

“Hivyo tunatakiwa kufanya mambo ya kumpendeza Mungu   tuweze kurithi ufalme wa mbinguni,”alisema.

  Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Theresia Jijini Tanga, Padre Sebastian Mbega aliwataka waumini kuwa na macho ya ufufuo dhidi ya dhambi na umauti kwa  kuendelea kutenda mema   kuweza kumpendeza Mwenyezi Mungu ikiwamo kuacha maovu.

Pia alisisitiza upendo na amani kwa waumini hao kwa vile jambo hilo ni msingi mkubwa wa ukristo  kuhakikisha wanapendana na ndiyo maana kuna amani kubwa.

Padre Sebastian aliyasema hayo jana wakati wa Ibada ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika kwenye kanisa hilo lililopo barabara ya 20 jijini Tanga.

Aliwataka waumini hao kuwa na macho ya ufufuko kwa kuhakikisha wanaendelea kutenda yaliyo mema kwa jamii yatakayokuwa msingi wa kumpendeza Mwenyezi Mungu.

Alisema wakristo lazima wawe macho, uhai na uzima dhidi ya mauti na dhambi   kuweza kuishi maisha ya uzima kwani ukiwa kwenye hali hiyo utaweza kutenda mema kila wakati.

“Ndugu zangu wakristo tuwe macho ufufuko, uhai uzima dhidi ya dhambi kwani ukiwa na hali hii unaweza kutenda mambo mema yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu kwenye maisha ya sala, “alisema.

Hata hivyo aliwakumbusha waumini kuendelea kusali na wamuombe Mungu awape macho ya ufufuko ili watamani yaliyo juu kwa kutafuta maisha   ya kila siku na siyo chini.

ASKOFU CHILONGANI

ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kati, Dk.Dickson Chilongani alisema  licha ya  Serikali kupambana na rushwa lakini hali hiyo bado ipo na kwa kiwango cha juu.

Akihubiri kanisani hapo alisema   ni aibu kwa watumishi wa serikali kuendekeza vitendo vya rushwa licha ya serikali kupiga vita vitendo vya rushwa na ufisadi.

Dk.Chilongani alisema   kwa sasa rushwa inaendelea kufanyika katika ofisi za umma huku jina linalotumika kudai rushwa ni “supporting  document” jambo ambalo linakwamisha utendaji wa kazi kwa ufanisi.

“Hivi karibuni nilisafiri kwenda nje,   cha kusikitisha nilipofika uwanja wa ndege wa Dar es Saalam, nilipokewa na wahudumu ambao ni watumishi wa serikali licha ya kuwa sikuwaomba msaada wowote wa kunisindikiza au kufunga zipu ya begi langu lakini waliniomba hela ya soda ambayo ni rushwa,”alisema Askofu Dk. Chilongani.

Alisema kuwa vita ya rushwa isiwe ya mtu mmoja au serikali pekee bali iwe ya watanzania wote na kama rushwa haitapigwa vita na watu wote ni dhahili  watu wanyonge hawatapata haki zao.

Habari hii imeandaliwa na ELIZABETH HOMBO, OSCAR ASSENGA , Eliya Mbonea, Ramadhan Hassan Na ALLAN VICEN

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,656FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles