25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Serengeti Boys ndiyo basi tena Afcon ya vijana

NA MOHAMED MHARIZO

NDOTO ya timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania walio chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kutwaa ubingwa wa Afrika sambamba na kufuzu fainali za  Kombe la Dunia zimefutika rasmi, baada ya jana kuchapwa mabao 4-2 na Angola, mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Serengeti ilizindua kampeni hizo kwa kufungwa mabao 5-4 na Nigeria, kisha kuchapwa mabao 3-0 na Uganda, kabla ya jana kutunguliwa mabao 4-2 na Angola.

 Serengeti Boys iliuanza mchezo jana kwa kasi, ikisaka ushindi, dakika ya 12, Omary Omary aliipatia bao la kuongoza, baada ya kuunganisha kona ya Edmund John.

Kuingia kwa bao hilo kuliizindua Angola, ambayo iliongeza mapambano na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 17, kupitia kwa Telson Tome, aliyefunga kwa kichwa baada ya kuunganisha krosi ya Osvaldo Capemba.

Dakika ya 33, mwamuzi wa mchezo huo, Abdulwahid Huraywida kutoka Libya, alimwonyesha kadi ya njano Omary Omary wa Serengeti Boys, baada ya kumchezea faulo David Nzaanza wa Angola.

Angola iliandika bao la pili  dakika ya 40 kwa mkwaju wa penalti uliofungwa na Capemba, baada ya Omary Omary kumkwatua Zito Luvumba wa Angola ndani ya eneo la hatari.

Dakika ya 43, Serengeti Boys ilisawazisha kupitia kwa Agiri Ngoda.

 Dakika ya 44, Serengeti Boys ilifanya mabadiliko, alitoka Edmund John na kuingia Ladaki Chasambi.

 Timu hizo zilimaliza kipindi cha kwanza zikiwa zimefungana mabao 2-2. 

Kipindi cha pili kilianza huku Serengeti Boys ikijaribu kusaka ushindi.

Dakika ya 61, Serengeti Boys ilifanya mabadiliko, alitoka Morice Abraham na kuingia Salum Milinge.

Angola nayo ilifanya mabadiliko dakika ya 63, alitoka Francisco Junior na kuingia Manuel Miguel.

Dakika ya 68, Angola iliandika bao la tatu lililofungwa na David Nzanza. 

Bao hilo liliichanganya Serengeti Boys, ambayo ilijikuta ikifungwa bao la nne dakika ya 71 kupitia kwa  Capemba. 

Hadi mchezo huo unamalizika Angola walitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 4-2 na kutinga nusu fainali, sambamba na kukata tiketi ya Kombe la Dunia. 

Angola inaungana na Nigeria kutinga nusu fainali ya michuano hiyo na kufuzu Kombe la Dunia.

 Katika mchezo mwingine wa kundi A, Nigeria ilitoka sare ya bao 1-1 na Uganda Uwanja wa Azam Complex. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles