Na BENJAMIN MASESE
WAHITIMU wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Twihulumile Mwanza, wamemuomba Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula (CCM) kukaa na wabunge wa chama hicho kuishauri Serikali kukubali Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HSELB) itoe mikopo kwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Asha Omari kwa niaba ya wahitimu wenzake wakati wa mahafali yao katika risala yao kwa mgeni rasmi, Mabula ambaye aliwakilishwa na Diwani wa Kata ya Nyegezi, Edith Mudogo (CCM).
Walimtaka mbunge huyo kukaa na wabunge wenzake kuishauri Serikali kupitia wizara ya elimu na bodi ya mikopo kuangalia upya mfumo wa utoaji mikopo kuwawezesha wanafunzi waliosoma kwenye shule binafsi kupata fursa hivyo sawa na wahitimu waliosoma shule za umma.
Omari alisema hawafurahishwi kuona namna Serikali inavyowabagua wanafunzi waliosoma kwenye shule binafsi na kuwapa unafuu waliosoma kwenye shule za umma wakati wote ni watanzania.
“Kusoma kwenye shule binafsi hakumaanishi wazazi wao wana uwezo mkubwa wa uchumi bali hujikamua na kujinyima kuwawezesha kupata haki ya elimu baada ya kukosa fursa kwenye shule za serikali.
“Hivyo tunaomba utusaidie kufikisha kilio chetu bungeni kwa waziri wa elimu aone utaratibu unaofaa wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wote wanaojiunga na vyuo vikuu bila kujali shule walizosomea.
“Kama mbunge unayetokana na CCM tunaomba ukae na wabunge wenzako muishauri Serikali na bodi ya mikopo ili na sisi tupate fursa hiyo,” alisema Omari.
Hata hivyo walimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuboresha huduma za jamii zikiwamo elimu bure, afya, maji,umeme na barabara huku utulivu kwa wafanyabiashara wadogo (machinga) ukiiamarika baada ya kuwatetea na kuwatengenezea vitambulisho.
Akijibu risala hiyo, Mudogo alisema maombi yao ya mikopo atayafikisha kwa mhusika kama na kuwataka wahitimu hao kuendeleza nidhamu waliyokuwa nayo shuleni baada ya kuingia uraiani ambako kuna changamoto na tabia mbalimbali.
Aliwashauri kujiepusha kufanya vitendo vya ngono kuepuka kuambukizwa Ukimwi ambao umeendelea kuteketeza nguvukazi ya taifa.
“Elimu ndio kila kitu katika karne hii ambayo itaondoa changamoto mbalimbali na ni ufunguo wa maisha.
“Niwapongeze walimu na wazazi kuona umuhimu wa elimu kwa sababu ni urithi pekee wanaostahili kupewa watoto, utampa vyote mtoto vitakwisha lakini elimu akishaipata haiwezi kutoka kichwani,”alisema.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Buhongwa, Paul Mbinayamaswa alisema serikali ya awamu ya tano ni sikivu, inasikiliza maombi ya wahitimu hao kuhusu utaratibu wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanaochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu.
Awali, Mkuu wa shule hiyo, Michael Boniface alisema licha ya kuwapo na changamoto shule imepata mafanikio makubwa ya taaluma tangu kuanzishwa kwake. Hata hivyo alisema imani yake kwa wahitimu hao 44 ni kupata ufaulu wa daraja la kwanza, pili na tatu kwani wana uwezo mkubwa wa taaluma