29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mianya ya rushwa ibanwe urasimishaji makazi

SERIKALI imetangaza kupunguza gharama za kurasimisha makazi  kutoka Sh 250,000 hadi 150,000 ili wananchi wa hali ya chini waweze kumudu gharama za urasimishaji.

Uamuzi huu umetangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi ambaye amesisitiza kupunguza gharama hiyo kutasaidia kila mwenye kipande cha ardhi aweze kukilipia.

Lukuvi anasema gharama zilizokuwa zinatozwa hapo awali na kampuni za upimaji ni kubwa ambazo  zilisababisha wananchi wengi kushindwa kuzimudu.

Kwa mujibu wa Lukuvi, wananchi wengi wa hali ya chini wengi pia wameshindwa kununua viwanja vilivyopimwa na Serikali vyenye hati kutokana na uduni wa vipato.

Tunakubaliana na uamuzi huu, kwa sababu kiwango hiki ni kikubwa kutokana na hali halisi ya uchumi ilivyobana, lakini busara hii inaweza kupunguza tatizo hili na kila mwenye kustahili kulipa atalipa kwa wakati.

Kutoza kiwango hicho kikubwa ilikuwa ni kuwabebesha mzigo wananchi wa kawaida ambao bado wana wanatamani wafikie malengo. Lakini pia hali hii  imechangiwa na Serikali kushindwa kuweka mikakati ya aina hii mapema.

Tunasema hivyo kwa sababu kuna maeneo iliacha maeneo mengi bila kupimwa na wananchi wakaamua kujenga majengo yao na kupelekewa huduma za maji, umeme na nyinginezo.

Kosa hili  ni kubwa ambalo linasababisha leo hii wananchi wabebeshwe mzigo huu, wakati watu wa mipango  miji wapo na wanalipwa mishahara.

Mipango miji ndiyo wanapaswa kutupiwa lawama zote hizi kwa sababu wapo wanaoishi maeneo hayo lakini hawakuchukua hatua za kuzuia.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Lukuvi bado ana kazi ya ziada ya kuhakikisha wananchi hawabebeshwi mzigo mkubwa, kama alivyosema kuwa amefanya utafiti na kubaini kuna kampuni za upimaji zinapata fedha nyingi.

Kuhusu uwajibikaji ni muhimu Serikali ikasimamia suala hilo kwa dhati. Hii ni kutokana na maelezo ya waziri, ambapo hadi sasa kampuni zilizosajiliwa kwa upimaji ni zaidi ya 70, lakini zinazofanya vizuri ni chache.

Inasikitisha kuona Waziri Lukuvi anasema wameshindwa kuchukua hatua kwa muda mrefu kuwafutia wapimaji wanaofanyakazi chini ya kiwango kwa sababu mkurugenzi wa upimaji alikuwa hajateuliwa.

Huku ni kuhalalisha wapimaji hawa waendelee kuwaumiza Watanzania, jambo ambalo halikubaliki.

Tunapenda kuona wapimaji wanafanya kazi zao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakamilisha hatua zote za upimaji hadi utoaji wa leseni za makazi kama sheria inavyowataka.

Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya msingi, huku kampuni ambazo zinafanya kazi chini ya kiwango zinachukuliwa hatua kali za kisheria.

Katika hili, tunapenda kuwatahadharisha watumishi wa Serikali wanaomiliki kampuni za upimaji wasiwe mabingwa wa kukimbilia kupewa tenda, kwani wataanza hata kutumia vifaa vya ofisi kwa ajili ya masilahi yao binafsi.

Tunasisitiza  hili kwa sababu wapo watumishi wasiokuwa waadilifu watatumia mwanya huo kujitajirisha mamilioni ya fedha kwa kutumia vifaa vya serikali hadi tenda hizi zitakapokamilika.

Pia kwa kuwa kazi hii ni endelevu nchi nzima, inapaswa kusimamiwa na halmashauri zetu vizuri ili mwisho wa siku kila mwananchi aweze kupimiwa eneo lake ambalo litasaidia serikali kukusanya kodi kwa maendeleo ya taifa.

Ni ukweli kwamba asilimia 70 ya wananchi wa kawaida hawalipi kodi,  hivyo urasimishaji na utoaji wa leseni za makazi utasaidia kuwatambua wamiliki wa vipande vya ardhi na mwisho wa siku Serikali itaongeza makusanyo ya kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles