TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM
Wanafunzi wa Sekondari zaidi ya 200 wanatarajiwa kuchuana vikali katika maonesho ya kufanya Tafiti za kisayansi kwa wanasayansi chipukizi yatakayofanyika Julai 31 na Agosti mosi Mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 18, Mwanzilishi mwenza wa Taasisi ya Young scientist (YST), Gosbert Kamugisha amesema mpaka sasa wamepokea kazi za wanafunzi zaidi ya 600 ambazo watazichuja na kubaki 200.
“Kwa kushirikiana na wafadhili wetu ambao ni Karimjee Jivanjee Foundation(KJF) na Shell Tanzania tumefanikiwa kutembelea shule mbalimbali na kuwaelekeza wanafunzi namna ya kufanya tafiti na ugunduzi wa teknolojia,” amesema Kamugisha.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Toyota Tanzania ambao ni wadhamini wa Karimjee Jivanjee Foundation, Yusuf Karimjee amesema taasisi hiyo itatoa ufadhili wa masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi watakaofanya vizuri katika maonesho hayo.
“Kuanzia Mwaka 2012 hadi mwaka jana KJF imekuwa ikitoa udhamini kwa wanafunzi wabunifu kupitia YST ambapo jumla ya wanafunzi 27 wamenufaika na ufadhili huo,” amesema Yusuf.