32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wawekezaji watakiwa kujenga hoteli maeneo ya hifadhi

Na Aziza Masoud – Dar es Salaam

WAKALA wa Misitu (TFS) imewataka wawekezaji kujenga hoteli, nyumba za starehe na maeneo ya kuchezea watoto katika maeneo yenye vivutio vya utalii ili kuongeza mvuto utakaoongeza watalii.

Akizungumza katika Msitu wa Pugu, Dar es Salaam jana wakati wa ziara ya utalii wa ndani kwa ajili ya wananchi na wanafunzi, Meneja Masoko wa TFS, Mariam Kobelo, alisema ipo haja ya wawekezaji kuanza kuwekeza kwa kujenga hoteli na maeneo mengine ya kupumzika katika misitu ya kitalii na maporomoko ili kuongeza mvuto wa maeneo hayo.

“Tuna vivutio vingi kama Msitu wa Pugu, Msitu wa Amani, maporomoko ya maji na vinginevyo, lakini nadhani watu wengi wanashindwa kufika kwa sababu ya maeneo hayo kutokuwa na sehemu rasmi za kupumzikia.

“Kutokana na hali hiyo, natoa wito kwa wawekezaji kujenga hoteli za kitalii, kumbi za starehe na maeneo ya kuchezea watoto ili kuongeza mvuto wa maeneo hayo na kuongeza idadi ya watalii, hasa wa ndani,” alisema Kobelo.

Pia aliwataka wazazi na walimu kuwa na utaratibu wa kuwatembeza wanafunzi katika vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo ya karibu ili waweze kupata ufahamu wa masuala ya uhifadhi.

Alisema ziara za mara kwa mara katika maeneo hayo pia zitawasaidia kupata elimu itakayowafanya wafahamu vitu na viumbe vilivyopo katika misitu na kuvitangaza.

“Mfano hapa katika Msitu wa Pugu, waliofika hapa watapata fursa ya kuona mti wa Mpugupugu ambao ndiyo chanzo cha jina la eneo hili pamoja na Bwawa la Minaki, mapango ya popo, hivyo tunaamini wao watakuwa mabalozi wa kuvitangaza,” alisema Kobelo.

Kwa upande wake, Hashim Mbita, ambaye ni mmoja wa wananchi waliofika kufanya utalii huo, alisema kitendo cha TFS kuweka utaratibu wa kutangaza utalii wa ndani kupitia wanafunzi na wananchi ni kizuri kwa kuwa kinaisadia jamii kuwa na uelewa mpana wa masuala ya utalii.

“Mimi ni mmoja wa watu wanaopenda  utalii wa ndani, nina utaratibu wa kwenda katika vivutio vya utalii mara kwa mara, lakini utaratibu huu wa TFS unatukutanisha watu tunaopenda utalii na kuzuru maeneo ya utalii,” alisema Mbita.

Pia alizitaka idara zinazosimamia vivutio vya utalii kuyatangaza maeneo hayo kwa Watanzania ili yajulikane kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles