Na GRACE SHITUNDU
RAIS Dk. John Magufuli amesema wadau wa maendeleo wasituzuie kuendelea kutunza mazingira kwa kujenga mradi wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji – Stiegler’s Gorge kwa kuwa tusipofanya hivyo hata pori la Selous linaweza kuwa historia kwa sababu wananchi watakata miti kwa kutafuta nishati.
Kiongozi huyo ambaye anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Ruvuma, aliyasema hayo jana wakati akizindua mradi wa kuzalisha umeme wa Makambako hadi Songea wa kilovolti 220.
“Wadau watuelewe sisi ni watunza mazingira kuliko wote duniani, msituzuie kuendelea kutunza mazingira na ninakuomba balozi wa Sweden uendelee kuwaelimisha wengine kwamba huu mradi ni muhimu kwa kutunza mazingira, na tusipouanzisha huu mradi ni vigumu kuyatunza mazingira,” alisema Rais Magufuli ambaye aliishukuru Serikali ya Sweden kwa kuwa marafiki wazuri na kuisaidia Tanzania kwa muda mrefu.
Alisema Tanzania itaendelea kuwaomba waendelee kusapoti kwa miradi mingine ili nchi iweze kuwa na umeme wa uhakika.
“Tuna gesi, makaa ya mawe madini ya kila aina ambayo tunaweza kuzalisha umeme, nina uhakika haya maeneo yote yakifanywa vizuri nchi yetu itaweza kusogea mbele katika suala la nishati.
“Nimeeleza hapa zaidi ya hekta 400,000 za miti zinakatwa, tusipowapelekea umeme hata hilo pori la Selous litakuwa historia, na huo ndio ukweli, siwezi kuwapanga askari polisi wawazuie wananchi kwenda kukata kuni wakati sijawapelekea umeme,” alisema.
Alisema ndiyo maana Serikali ikatumia busara ya kawaida ili kuendelea kutunza hizo hifadhi pamoja na Selous kwa kutoa asilimia mbili ya hifadhi kwa ajili ya kutengeneza umeme wa megawati 2,100 utakaopelekwa kwa wananchi kwa bei nafuu.
Rais Magufuli alirejea kauli yake ambayo amekuwa akiitoa kila mara tangu aamue kutekeleza mradi wa Stiegler’s Gorge kuwa una umuhimu mkubwa katika utunzaji wa mazingira na maendeleo ya wananchi.
Alisema mradi huo utakuwa muhimu na mkubwa kwa kuwa utatoa megawati 2,100 zaidi ya umeme wote uliopo na malengo ni kufikia megawati 5,000 ili nchi ifanye vizuri katika viwanda
“Mradi wa Stiegler’s Gorge na mbuga ya Selous tunatoa kasehemu kadogo tu, Selous ukubwa wake ni zaidi ya nchi ya Ubelgiji.
“Nchi nzima ya Ubelgiji unaiweka kwenye mbuga ya Selous inapotelea humo na tumeendelea kuitunza kwa miaka yote wakati kwa nchi nyingine wameshamaliza maeneo yao ya hifadhi na wameshamaliza wanyama wao, sisi tumetunza.
“Tumetunza Selous, Serengeti, Ngorongoro na maeneo mengine mengi ambayo yameongezwa matano kuwa hifadhi ya Taifa.
“Lakini tunapoongeza maeneo ya kuhifadhi, lazima tunawapa watu wetu adhabu kwa kuwa maeneo hayo ndiyo maeneo yao ya kukata kuni.
“Tulipopata uhuru tulikuwa watu milioni 9 hadi 10, leo watu wako milioni 55, hujawaletea umeme wa bei nafuu unawazuia kukata kuni, wataishije?” alisema.
Akizungumzia nishati hiyo mkoani Ruvuma, alisema lilikuwa tatizo kubwa kwani walitegemea majenereta katika kuzalisha umeme.
“Mradi huu (aliouzindua) utasaidia kuondoa changamoto ya umeme kwenye mikoa ya Njombe na Ruvuma na utaokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.8 ambacho kilikuwa kikitumika kuzalisha umeme wa mafuta.
“Napenda kuipongeza Wizara ya Nishati kwa kufanikisha mradi huu kwa msaada wa Serikali ya Sweden, kwani nchi isipokuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na unaopatikana kwa bei nafuu, shughuli nyingi ni vigumu kufanyika,” alisema.
Alisema ukosefu wa umeme una athari nyingi za kiuchumi akitolea mfano watu wengi kulazimika kutumia mafuta ya taa, mkaa au kuni.
“Nchi yetu kila mwaka hupoteza takribani tani 400,000 za miti kwa ajili ya mkaa na kuni hali inayochangia uharibifu wa mazingira.
“Lakini ni ukweli usiopingika kwamba usipowapa njia mbadala unategemea nini kwa sababu nchi yetu ya Tanzania eneo lipatalo asilimia 32.5 ya eneo lote ni hifadhi, zilizobaki ndio maeneo yanayoweza kutumika kwa shughuli mbalimbali.
“Tangu uhuru eneo liko vile vile, wakati watu wanaongezeka, idadi ya mifugo inaongezeka na mahitaji ya matumizi yanaongezeka,” alisema.
Alisema nchi nzima umeme unaopatikana ni megawati 1,560 na mahitaji ni makubwa na yataendelea kwa sababu nchi imeamua kuwa na uchumi wa viwanda.
“Viwanda huwezi kuviendesha kwa dizeli bali umeme tena wa bei nafuu, kwa bahati mbaya unauzwa uniti moja kwa bei ya juu ukilinganisha na nchi nyingi zilizoendelea, hapa kwetu uniti moja inauzwa dola senti 11 hadi 12, lakini baadhi ya nchi unauzwa dola senti 0.12.
“Ni ukweli usiopingika kwamba sisi hatutaweza kushindana na nchi hizo katika viwanda kwa sababu viwanda vyao vitakuwa vinatengeneza bidhaa za bei nafuu na sisi tutatengeneza za bei ya juu.
“Kwa hali hiyo bidhaa zetu zitakosa soko maana yake tutakuwa tunatengeneza malighafi na kuwapeleka wao, hivyo suala la ajira kwetu tutalisahau na wao tutawatengenezea ajira,” alisema.
Alieleza kwa kuliona hili Serikali imeamua kufanya uwekezaji katika umeme kwa kuwa nchi yoyote inayotaka kujikomboa kiuchumi ni lazima ifanye hivyo.