29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Zanzibar yajipanga kukomesha udhalilishaji

KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR

WAZIRI wa Katiba na Sheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Khamis Juma Mwalimu, amewataka wananchi kushirikiana pamoja na Serikali katika kupinga na kuondoa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wananchi na watoto.

Amesema kufanya hivyo kutaweza kuimarisha ustawi wa jamii sambamba na kupata vizazi vilivyo bora.

Hayo aliyasema jana mjini Unguja baada ya kumaliza matembezi ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.

Alisema wananchi wana wajibu wa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupiga vita udhalilishaji ambao hauendani na mila na utamaduni wa Kizanzibari, jambo linalosababisha kuporomoka kwa maadili.

Alisema Serikali imeweka sheria na mikakati madhubuti kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.

“Katika kupambana na vita hii, Serikali imeamua kusimamia sera, mwongozo na sheria ili kuona inaleta uwiano wa kutokomeza vitendo hivi vya ukatili kwa jamii,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mwalimu aliwataka wazazi na walezi kutimiza vyema majukumu yao kwa kuwa karibu na watoto kwa kila hatua kama njia ya kukomesha vitendo vya udhalilishaji kwao kwa kuwajenga mazingira bora ya baadaye.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alizipongeza jumuiya mbalimbali za CCM katika mkoa huo kwa juhudi wanazozichukua ikiwamo kuandaa makongamano na kutoa elimu kwa jamii kuhusu vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na ukatili kwa watoto.

Akisoma risala ya Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Kichama Dimani, Makame Ameir Yussuf, alisema jumuiya hiyo imeandaa matembezi hayo ili kuunga mkono juhudi za Serikali na kuendelea kuikumbusha jamii juu ya kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na kuimarisha ustawi wa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles