23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Serikali yaonya rushwa chaguzi za S/Mitaa

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SERIKALI imeonya kuwa haitakuwa na simile kwa mtu au chama cha siasa au kikundi chochote kitakachojihusisha na rushwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akifungua mkutano wa kujadili namna ya kudhibiti rushwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu  jijini Dar es Salaam jana.

Alisema Serikali ya Rais Dk. John Magufuli inataka wananchi watambue kuwa Serikali yao imedhamiria kupambana na rushwa katika nyakati zake zote na sura zake zote.

“Sote tunafahamu mwaka huu tutakuwa na uchaguzi katika ngazi za Serikali za Mitaa, hivyo basi chaguzi hizi zinapaswa kuendeshwa na kusimamiwa kwa uadilifu na umakini mkubwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili haki, usawa, uhuru na demokrasia viweze kustawi, kuendelezwa na kudumishwa, hivyo Takukuru kamwe isiwe na msalie Mtume kwa yeyote atakayejihusisha na masuala ya rushwa,” alisema.

Profesa Kabudi alisema rushwa katika uchaguzi ni zaidi ya udanganyifu wa hesabu za kura, kwa kuwa una madhara kadhaa ikiwemo viongozi kukosa uwajibikaji, waadilifu na  wazalendo.

Alisema pia hali hiyo huchangia uwepo wa vitendo vya uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa, uchumi kudidimia kwa kukosa mipango ya maendeleo na viongozi kufanya maamuzi ya kisera yenye masilahi kwa wachache.

Kutokana na hali hiyo, aliipongeza Takukuru kwa kuandaa warsha hiyo kwa wakati mwafaka, ambapo  pamoja na sheria na kanuni zilizopo, bado kuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha jamii inashirikishwa na kuelimishwa kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna Diwani Athumani, alisema rushwa katika uchaguzi ni hatari na inaweza kuleta madhara kwa Taifa kwani viongozi wala rushwa au watoa rushwa hawataweza kuisimamia nchi kwa misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo.

“Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kutosha na kutoa taarifa bila woga kwa wale wote watakaojihusisha na masuala ya utoaji ama upokeaji rushwa ili sheria ziweze kufuata mkondo wake na baadaye kuwa na Taifa lenye usawa katika nyanja zote,” alisema Diwani.

Warsha hiyo ya wadau kujadili namna ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa, vyama vya kiraia na vyombo vya ulinzi na usalama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,636FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles