Polisi nchini New Zealand imesema mshukiwa wa mashambulizi ya msikiti wa Christchurch atakabiliwa na mashtaka 50 ya mauaji na mashtaka mengine 39 ya kujaribu kuua wakati atakapofikishwa mahakamani leo Ijumaa.
Brenton Harrison Tarrant, ambae ni raia wa Australia, alikamatwa mnamo Machi 15 siku moja baada ya mauaji hayo yaliyofanyika katika misikiti miwili.
Watu 50 waliuawa katika misikiti miwili na wengine kadhaa walipigwa risasi na kujeruhiwa. Tarrant hatolazimika kujibu mashtaka hapo kesho.
Majaji wamesema kufikishwa kwake mahakamani kutahusu zaidi uwakilishi wa kisheria wa Tarrant ambae amesema anataka kujiwakilisha mwenyewe.
New Zealand itazuia kile kinachoweza kuripotiwa juu ya kesi hiyo, ili kuepusha kushawishi uamuzi wa baraza la wazee wa mahakama.