MAPUTO, Msumbiji
SERIKALI ya hapa imesema maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu katika mji wa Beira yameongezeka maradufu na kufikia wagonjwa 271 katika kipindi cha saa 24 mpaka jana.
Serikali na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wanajaribu kudhibiti kusambaa maradhi hayo wiki mbili tangu kimbunga Idai kilipouukumba mji wa Beira na kusababisha mafuriko makubwa yaliyowaua zaidi ya watu 700 katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.
Akizungumza wakati wa kufungua kituo cha muda cha matibabu ya kipindupindu mjini Beira, Waziri wa Mazingira alisema tayari wagonjwa 138 wanapatiwa matibabu na kwamba hadi sasa hakuna aliyefariki dunia kutokana na maradhi hayo kwenye hospitali zinazotoa huduma.
Maeneo mengi nchini hapa na Zimbabwe ambayo yaliathiriwa vibaya na kimbunga Idai bado hayafikiki kwa njia ya barabara.
Maradhi ya kipindupindu ni tatizo sugu nchini hapa ambayo yameshuhudia milipuko ya mara kwa mara katika miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watu 2000 walikumbwa na kipindupindu wakati mlipuko wa mwaka jana.