33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa wa ugaidi wafikishwa mahakamani

ugaidi arusha
Watuhumiwa wa kosa la kukutwa na mabomu wakielekea katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha jana kusomewa mashtaka yanayowakabili.

JANETH MUSHI NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

WATUHUMIWA sita wanaodaiwa kufanya ugaidi jijini Arusha, wamefikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya kosa la kurusha bomu katika Mgahawa wa VAMA, Julai 7, mwaka huu na kujeruhi watu wanane.

Wakisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Maahakama ya Mkoa wa Arusha, Rose Ngoka na Wakili wa Serikali, Augustino Temba akisaidiana na Wakili Felix Kwetukia, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shaban Mmasa ambaye ni mlinzi aliyekuwa VAMA siku ya tukio, Athuman Mmasa (38) na Mohamed Nuru (30) ambao ni walinzi wa mgahawa wa Kichina uliopo jirani na VAMA.

Watuhumiwa wengine ni Imam wa Msikiti wa Quba ambaye pia ni Mwalimu wa Shule ya msingi Olturmet, Jaffar Hashim Lema (38), Abdul Salum (31) na Said Temba (42) ambaye ni mfanyabiashara jijini Arusha.

Temba alidai kuwa kosa la kwanza linalowakabili watuhumiwa wanne ambao ni Shaban Athuman, Mohamed na Lema ni kosa la kutenda njama za kufanya ugaidi kinyume na kifungu namba 24(2) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.

Alidai mahakamani hapo kuwa kati ya mwezi Februari na Julai mwaka huu, kwa pamoja walifanya njama ya kufanya ugaidi katika Mgahawa wa VAMA.

Shtaka la pili linalowakabili watuhumiwa wote ni kosa la ugaidi, kinyume na kifungu namba 4(2) c, kifungu cha 3(a,b,c,e) na kifungu cha 27 (a,c,b) na 13 cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 31 cha sheria ya kuzuia ugaidi ya mwaka 2002.

Mwanasheria huyo wa Serikali aliieleza Mahakama kuwa Julai 7, mwaka huu, watuhumiwa wote walifanya kitendo cha kigaidi kwa kurusha bomu la mkono katika mgahawa huo na kujeruhi watu wanane (8).

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa la ugaidi Julai 7, mwaka huu katika Mgahawa wa VAMA na kusababisha madhara.

Katika shtaka la tatu ambalo ni kutoa silaha kinyume na kifungu namba 20(C) cha sheria ya kuzuia ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, kosa linalowakabili Athumani na Lema, ambao wanadaiwa kutoa silaha aina ya bomu la kurushwa kwa mkono kwa Mohamed kati ya Julai 5, hadi 7 mwaka huu.

Kosa la nne linalowakabili Lema, Salum na Temba ni la kutoa ushirikiano katika kufanya ugaidi, ambapo wanadaiwa kwa tarehe tofauti walitoa msaada wa kifedha na kuwezesha kufanyika kwa kosa la ugaidi katika mgahawa wa VAMA.

Temba aliieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakalimilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya kutajwa tena kwa kesi hiyo.

Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Ngoka, aliahirisha shauri hiyo kwa kuwa haina uwezo wa kulisikiliza kwa mujibu wa sheria

“Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili, hivyo mnatakiwa kukaa kimya bila kujibu chochote hadi itakapopelekwa Mahakama Kuu na ninaahirisha kesi hii hadi Agosti 6, mwaka huu itakapotajwa tena,” alisema Hakimu Ngoka.

Katika tukio la bomu ambalo ni la sita kutokea jijini hapa, watalii wanane kutoka nchini India walijeruhiwa vibaya sehemu za miguuni kwa bomu lililorushwa ndani ya mgahawa huo.

Waliojeruhiwa katika tukio hilo ni Deepack Gupla (25) aliyepoteza mguu wake wa kushoto, Mahash Gupta, Manisha Gupta na mtoto wao Mansi Gupta, Manc Gupta (36), Prateek Jaley, Vinod Suresh (37) na Raj Rajin (30).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles