PATRICIA KIMELEMETA
CHAMA Cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, umemuomba Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuibana Mahakama Kuu kutoa hukumu ya kesi namba 23/2016 inayohusu uhalali wa uenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba kwenye chama hicho.
Kauli hiyo imetolewa wiki moja baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaama, Benhaj Masoud, kuahirisha hukumu ya kesi hiyo hadi Machi 18.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, baadhi ya wabunge wa chama hicho upande wa Maalim Seif, walisema mpaka sasa wanashindwa kuendelea na majukumu ya siasa kutokana na mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho, hali iliyosababisha kufunguliwa kwa kesi mahakamani ikiwamo ya uhalali wa Lipumba.
“Tunaomba Jaji Mkuu, Profesa Juma au Jaji Kiongozi, Dk. Eliezer Felesh, kuingilia kati hukumu ya kesi yetu ambayo inachukua muda mrefu kutosomwa hali inayosababisha shughuli za siasa kushindwa kufanyika kutokana na mgogoro wa uongozi,”alisema Mbunge wa Malind, Ally Saleh ambaye ndiye aliyefungua kesi hiyo.
Alisema mgogoro huo umesabababisha kujitokeza mgawanyiko wa wanachama ambako upande mmoja unamuunga mkono Lipumba na mwingine unamuunga mkono Maalim Seif.
Alisema mpaka sasa hukumu hiyo imeahirishwa mara nnne na mara ya kwanza ilitakiwa kusomwa Oktoba 10, 2018, iliahirishwa hadi Novemba 30, 2018, ikaahirishwa tena hadi Januari 15, 2019, ikiaahirishwa tena hadi Februari 22, 2019 na sasa imeahirishwa hadi Machi 18, 2019.
Alisema kutokana na kujitokeza hali hiyo, wanachama wamepata wasiwasi wa kujua hatma ya uongozi ndani ya chama hicho hali iliyosababisha kumuomba Jaji Mkuu kuingilia kati.
Alisema mahakama ndiyo chombo pekee nchini kinachosimamia haki, hivyo basi wanaamini watatenda haki hukumu hiyo itakapotolewa.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, chama kinahitaji kufanya mikutano ya ndani kuteua viongozi mbalimbali watakaosimamia uchaguzi wa ndani na uchaguzi mkuu kuhakikisha wanashindwa, lakini kuwapo mgogoro huo kumesababisha kushindwa kufanyika mikutano.
Profesa Lipumba alijiuzulu nafasi ya uenyekiti Agosti 6, 2015 wakati chama kinaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais.
Alisema licha ya kupitia changamoto hizo, chama hicho kiliweza kufanya vizuri kwenye uchaguzi huo na kusaidia kupata wabunge wanne kutoka Zanzibar, walioingia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge wa uwakilishi viti 18 kutoka Pemba na viti tisa kutoka Zanzibar.
“Mpaka sasa CUF ina madiwani zaidi ya 300 nchini na inaongoza halmashauri tano ambazo ni Newala, Tandahimba, Mtwara, Kilwa na Liwale,”alisema.
Mbunge wa Nchinga, Hamidu Bobali, alisema mgogoro uliopo ndani ya chama hicho umesababisha wanachama kugawanyika.
Alisema kundi linalomuunga mkono Lipumba linawazuia wabunge wanaomuunga mkono Maalim Sief kufanya shughuli za siasa ndani ya majimbo yao.
“Mimi nipo upande wa Maalim Seif, Mwenyekiti na Katibu wa chama katika Halmashauri ya Nchinga, wapo upande wa Lipumba, kila nikitaka kufanya shughuli za chama wanakwenda polisi kuweka zuio jambo ambalo limeniathiri katika siasa,” alisema Bobali.