25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasiasa wa kike wa Afrika wanapigania kuwapo vileleni

OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI

Duniani kote wanasiasa wa kike wanaokamata nyadhifa za juu ni nadra. Katika Afrika hali hiyo imezidi. Pale viongozi mbalimbali wa nchi wanaposimama kupiga picha ya pamoja, wengi wao ni watu waliovaa suti nyeusi, ni taabu kupata sura ya aliyevaa gauni au mtandio.

Lakini kila miaka ikienda hali hiyo inabadilika. Kizazi kipya cha wanawake kinasonga mbele kutaka kukamata nyadhifa za juu katika siasa.

Ni nchi tano tu kati ya zaidi ya 50 katika historia ya Afrika baada ya uhuru kuwa na viongozi wa kike. Katika mabaraza ya mawaziri na mabunge wanawake kwa miongo ya miaka wamebakia kuwa wachache. Hadi sasa katika karibu kila nchi wanawake wanawakilishwa kwa uchache sana.

Mnamo miaka michache iliyopita nyuso za kizazi kipya cha wanasiasa wa kike kimechomoza na kuipunguza kasumba iliyoenea kwamba wanawake hawapendi siasa au labda hawajawiva vya kutosha kwa shughuli hiyo. Peke yake mwaka 2018 tumeshuhudia mishangao. Katika nchi ya Mali, huko Afrika Magharibi, kwa mara ya kwanza baraza la mawaziri lilianza kazi yake likiwa na thuluti moja ya mawaziri wa kike. Muhimu kati yao ni waziri mpya wa mambo ya kigeni, Camissa Kamara, aliye na umri wa miaka 35.

Mwaka huu Rwanda imevunja rekodi yake yenyewe. Shemu ya wanawake bungeni imezidi na kufikia asilimia 68 ya wabunge kutoka asilimia 64 hapo kabla.

Nchini Ethiopia Waziri Mkuu mpya, Abiy Ahmed, alichagua baraza la mawaziri lenye idadi sawa ya wanawake na wanaume, kumi kila upande. Wiki iliyopita Rwanda iliiga mfano wa Ethiopia. Pia muda mfupi kabla, Bunge la Ethiopia lilimchagua Sahle-Work Zawede kuwa rais wa mwanzo wa kike katika nchi hiyo iliyoko Pembe ya Afrika.

Katika Malawi na Jamhuri ya Afrika ya Kati kulikuwapo marais wa kike wa kujishikiza ampao mwaka 2014 na 2016 walifuatwa na wanaume. Ellen Johnson-Sirleaf wa Liberia, Rais wa kwanza wa kike katika Afrika, hajawania tena wadhifa huo baada ya kuwapo madarakani kwa awamu mbili. Machi 2018 Ameenah Gurib-Fakim akawa Rais wa kwanza wa kike katika Kisiwa cha Mauritius kilichopo Afrika.

Licha ya kwamba zaidi ya nusu ya wakaazi wa Afrika ni wanawake, lakini wanawake hivi sasa wamepiga hatua kubwa katika elimu na kuonesha vipaji, licha ya vizingiti vingi wanavyokabiliana navyo, ukilinganisha na wenziwao wanaume.

Rais Sahel-Work Zewde wa Ethiopia, mwenye umri wa miaka 68, ni mfano wa mwanamke aliyepanda juu na kufikia nafasi hiyo kutokana na elimu pamoja na uzoefu wake wa kuongoza.

Alizaliwa Addis Ababa na kusoma Ufaransa. Kazi yake ya kibalozi aliianzia katika enzi ya utawala wa kikoministi wa kijeshi huko Ethiopia katika miaka ya thamanini. Wadhifa wake wa mwanzo kama balozi ulianza mwaka 1989 huko Senegal, akifuata huko Djibouti na baadaye Ufaransa.

Pia alikamata nyadhifa mbalimbali katika Umoja wa Mataifa. Kama Rais wa Ethiopia, shughuli za Sahel-Work Zewde ni za uwakilishi wa nchi tu, madaraka yote yako mikononi mwa waziri mkuu. Lakini kuchaguliwa kwake ni hatua muhimu kwa wanawake wa Ethiopia na wa Afrika, kwa jumla.

Katika hotuba yake ya mwanzo mbele ya Bunge la nchi yake, Sahle-Work Zewde aliwataka Waethiopia waichunge amani, akitaja kwamba wanawake ni watu wa mwanzo wanaoteseka pale inapozuka mizozo. Na akaongeza: Pale mnapoamini kwamba nimezungumza sana juu ya wanawake, basi nakuhakikishieni kwamba: ndio kwanza sasa ninaanza.

Waziri mkuu wa Ethiopia amesisitiza kwamba wanawake huchapa kazi vizuri zaidi ndani ya serikali yake na kwa uchache sana ambapo utawagundua wana madoa ya kula rushwa au kuendesha ufisadi. Kwa hakika, tafiti zinathibitisha jambo hilo.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimarekani ya Utafiti (Thinktanks Council on Foreign Relations) mchango wa wanasiasa wa kike umesababisha athari nzuri katika nchi zinazopitia mizozo. Wanawake wanaposhiriki serikalini, basi vipindi vya amani katika nchi hizo huwa virefu zaidi na uwezekano wa nchi kuangukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe hupungua.

Watafiti wamegundua kwamba kutokana na hali hiyo ya wanawake kukamata nyadhifa za juu za kisiasa serikalini imani ya wananchi kuelekea taasisi za kisiasa huongezeka pale wakaazi wote, wakiwamo wanawake, wakijumishwa serikalini.

Swali: kwanini mnamo miaka iliyopita kumekuwapo mabadiliko ya wizani wa kijinsia katika majukwaa ya siasa katika Afrika? Mabingwa wanasema kwamba mabadiliko hayo yanatokana na mwamko ulioonekana katika miaka ya tisini. Katika wakati huo karibu nchi zote za Kiafrika zilikumbwa sana na mawimbi ya vuguvugu za kudai demokrasia. Mabadiliko ya vizazi katika siasa yamesababisha kupatikana nafasi mpya kwa vijana wa Kiafrika, hasa wanawake. Hiyo ndio maana tukaona idadi ya wabunge wa kike inaongezeka, jambo ambalo pia lilionekana katika mabaraza ya mawaziri.

Wachunguzi wa mambo pia wamegundua kwamba wanawake hufaidika pale si tu wanapokuwa wabunge, lakini pia wanapokuwa mabingwa nje ya Bunge pale wanapohitajika kushika nafasi za uwaziri. Wanawake walio na ujuzi na wachapaji kazi katika uajiri wa namna hiyo huwa hawalazimiki kuvivuka vizingiti vingi na mara nyingi kwa haraka hujikuta wanakamata nyadhifa za uwaziri. Hali kama hiyo imetokea kwa waziri mpya wa mambo ya kigeni wa Mali. Lakini shuruti muhimu ya kutokea hali kama hiyo inategemea vipi anavyofikiri mkuu wa nchi au serikali, kama vile alivyotenda Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, aliyetambua kwamba wanawake ni Bongo thamini kwa Afrika, pindi tu wanapewa nafasi.

Mnamo miaka 18 iliyopita sehemu ya wabunge wa kike katika nchi 49 zilizoko chini ya Jangwa la Sahara imeongezeka zaidi ya mara mbili. Hivi sasa wabunge wa kike wanatimia asilimia 23, idadi kubwa zaidi kuliko ile iliyopo Asia, nchi za Kiarabu na hata katika nchi nyingi za Ulaya Mashariki. Rwanda, Namibia na Afrika Kusini ni kati ya nchi zilizo na idadi kubwa sana ya wabunge wa kike duniani.

Umoja wa Afrika (AU) mwaka 1995- Mwaka wa Mkutano wa Wanawake mjini Peking- uliamua kwamba hali za wanawake na wasichana lazima ziimarishwe. Baadaye ikafuata Itifaki ya Maputo ambayo ilitunga haki za usawa wa kijinsia katika mwenendo wa siasa na kuanza kufanya kazi 2005. Hadi sasa Itifaki hiyo imeidhinishwa na nchi 37 barani Afrika. AU iliitangaza Ajenda 2063 yenye lengo la kutokomeza kabisa kukosekana usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maisha. Pia katika nchi nyingi za Afrika tangu miaka 20 sasa kumetolewa miito na kuwekwa mikakati ya kuwapa usawa wanawake. Mambo yote hayo yamewapa moyo wanawake wa Afrika.

Lakini bado mfumodume haujabadilika katika jamii nyingi za Kiafrika. Kuna tofauti kubwa katika kutoa ubora wa maisha baina ya wanaume na wanawake. Hasa wanawake wa Kiafrika wanakabiliana na vifo wakati wa kuzaa, hawapati nafasi za kutosha za elimu na wanakumbana na mimba za utotoni. Na kwa mwendo wa sasa itachukua miaka 100 kuufikia usawa wa kisiasa na kiuchumi baina ya jinsia barani Afrika.

Kuna wahakiki wanaolaumu kwamba bado marekebisho yanayofanywa sasa Afrika hayatoshi, hayaendi katika mizizi ya matatizo. Inasahaulika kwamba hatua za kuboresha uwakilishi wa wanawake zinakwenda moja kwa moja na mabadiliko ya kijamii na ubora endelevu wa maisha ya wanawake. Mfano wa ilivyo shida kuweza kuleta mabadiliko hayo unaonekana huko Kenya.

Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 inataka kila taasisi ya kisiasa inayochaguliwa katika nchi hiyo angalau iwe si chini ya thuluthi  moja ya wanawake. Lakini Bunge la nchi hiyo hadi leo halijapitisha sheria za kutekeleza jambo hilo. Katika uchaguzi mkuu wa karibuni uwakilishi wa wanasiasa wa kike waliochaguliwa umebakia asilimi 9.2 tu.

Shida ni kwamba  wanawake hawaungwi mkono vilivvyo na vyama vya siasa pale wanapopigania nyadhifa, hawapatiwi msaada wa kifedha na hata hubaguliwa. Shida ni kwamba kumejengeka mawazo potofu miongoni mwa baadhi ya wanaume kwamba kitu kinachotarajiwa kutoka kwa mwanamke na lengo tu ni kuolewa na kuzaa watoto. Mfumodume unaangalia kwamba mahala pa mwanamke ni jikoni tu.

Tangu utotoni, kwa makosa, msichana husomeshwa kwamba jukumu lake ni tu kumsaidia mama kazi za nyumbani, huku mvulana akicheza mpira na kwamba kazi ya kusafisha nyumba ni ya msichana tu. Mabadiliko ya kweli lazima yaanze mapema tunapowalea watoto wetu, tutoe nafasi sawa kwa wote na tuachane na kasumba inayoendelea kubakia miongoni mwa baadhi yetu kwamba mtoto wa kiume ni bora kuliko wa kike katika jamii. Ni hapo tena tunaweza kudai kwamba tumefaulu kuwa na usawa wa kijinsia

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles