DERICK MILTON
MATUKIO ya kupotea watoto wadogo katika mazingira ya kutatanisha kabla ya kukutwa wameuawa, yanayotokea mkoani Njombe, yanaonekana kuingia katika Kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Matukio hayo yameanza kuleta hofu kubwa kwa wakazi wa kata hiyo juu ya watoto wao ambako watoto watatu wasichana na wanafunzi, wameuawa kinyama kwa nyakati tofauti.
Moja ya tukio ambalo limeongeza hofu kwa wananchi wa kata hiyo ni kuuawa kwa Joyce Joseph (8) mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Lukungu mkazi wa Kijiji cha Lukungu katika kata hiyo.
Tukio hilo lilitokea Februari, 08 mwaka huu na mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukiwa umetupwa katika kichaka kijijini hapo, baada ya kupotea kwa siku mbili.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Iseni ‘B’, Julias Baraza siku moja kabla ya tukio hilo, mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani asubuhi kwenda shule lakini hakurejea nyumbani mpaka alipokutwa ameuawa na mwili wake kutupwa kichakani.
Matukio yaliyopita.
Tukio la kwanza lililotokea Oktoba 10, mwaka jana wakati mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Mwabasabi, Susana Shija (9) katika Kijij cha Lamadi, alipokutwa amekufa na mwili wake kutupwa kwenye jumba chakavu huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimeondolewa.
Mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukiwa hauna baadhi ya viungo vyake zikiwemo sehemu zake za siri, mikono yake yote miwili, miguu yote miwili na kuondolewa kwa nywele zake zote za kichwani.
Mama mzazi wa marehemu, Dina Halili, akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, alisema mtoto wake alitoweka nyumba katika mazigira ya kutatanisha wiki mbili zilizopita na akatoa taarifa Kituo cha Polisi Lamadi.
Katika tukio la pili, mtoto wa kike, Milembe Maduhu (12), mwanafunzi wa darasa la saba, naye alikutwa akiwa ameuawa ndani ya jengo linaloendelea na ujenzi maeneo ya Lamadi Desemba 13, 2018.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Deusdedit Nsimeki, mwanafunzi huyo alikuwa akisoma shule moja wilayani bunda (hakuitaja jina) na alipotea siku kadhaa akiwa anauza vitumbua mjini Lamadi, kabla ya mwili wake kupatikana katika jumba hilo.
Hofu kwa wananchi.
Baadhi ya wananchi wakizungumza na Mtanzania mjini Lamadi walisema wameanza kuwakataza watoto wao kwenda kutembea au kwenda kanisani peke yao huku wakilazimika kusindikiza kwenda shule.
Diwani wa Kata hiyo, Laurent Bija alisema bado hajaweza kugundua wahusika wa matukio hayo, licha ya wananchi kuwataja baadhi ya watu ambao wana shaka nao.
“Hofu ni kubwa kwa wananchi wangu, hata mimi mwenyewe, maana nimelazimika kuwakataza watoto wangu wa kike wawili kwenda kanisani au kutembea, lakini shuleni nawasindikiza asubuhi,” alisema Bija.
Mbali na diwani huyo baadhi ya wananchi walilalamikia jeshi la polisi wilayani humo kwa kuwakamata baadhi ya watu ambao walisema niwahusika lakini wameachiwa.
Mmoja wa wananchi ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema kuwa baada ya kufika matukio mawili, kuna baadhi ya watu walitajwa na wananchi kisha kukamatwa na polisi kwa lakini walishangaa kuona siku chache watuhumiwa hao wameachiwa.
Hata hivyo, diwani alisema jeshi la polisi liliwaachia watuhumiwa hao baada ya kukosa ushahidi wa kuwapeleka mahakamani, licha ya kutajawa na wananchi kuwa yawezekana ndiyo wanahusika.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Simiyu , na wajumbe wa kamati hiyo juzi walikuwa na kikao na wananchi kujadili matukio hayo.
Wakizungumza kwa uchungu katika mkutano huo uliochukua saa tano na kumalizika saa 3.00 usiku huku wanawake wakimwaga machozi. wananchi wengi walilitupia lawama kwa jeshi la polisi wilayani humo.
Walisema wahusika wa matukio hayo wamekuwa wakikamatwa na jeshi la polisi lakini huachiwa huru bila ya kufikishwa mahakamani.
Kwa mujibu wa wananchi hao moja ya jambo kubwa linalosababisha watoto wadogo kuuawa ni imani za ushirikina (CHUMA ULETE) ambazo walisema zimekithiri katika kata hiyo na wahusika wote wanafahamika.
Waomba kupiga kura
Baada ya malalamiko hayo wananchi hao walimuomba Mkuu huyo wa Mkoa, awaruhusu wapige kura ya kuwataja wahusika wakuu wa matukio hayo kwa kuwa wanawafahamu vizuri.
Mkuu huyo wa mkoa alikubaliana na ombi la wananchi hao kupiga kura, huku akiagiza mkuu wa upelezi mkoa na kamanda wa polisi mkoa kuwaondoa askari wote wanaotuhumiwa na ambao hawatekelezi kazi ipasavyo.
“Lakini katika hatua ya kura nakubali ifanyike lakini siyo njia sahihi, ila tutafanya kutokana na mazingira yetu, tusipige kura kwa ushabiki, ugomvi wetu mitaani, tuseme ukweli tu,” alisema Mtaka.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa serikali itawachukulia hatua kali wahusika wote ambao watabainika kufanya vitendo hivyo ambavyo alieleza vinaharibu taswira ya mkoa wake.