24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugu wa vigogo kesi ya Nida waangua vilio mahakamani

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

VILIO kutoka kwa ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake watano jana vilitawala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kukosa nafasi ya kuingia katika chumba cha Mahakama.

Vilio hivyo vilitokea wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kesi hiyo kuamuliwa kusikilizwa katika chumba cha hakimu badala ya mahakama ya wazi kama walivyotarajia wao.

“Kwa nini kesi hii haikusomwa katika mahakama ya wazi badala yake ikasomwa katika mahakama ya ndani (Chamber), tunashindwa kuingia kusikiliza chumba kidogo.

“Tumetoka mbali sana, wapo waliotoka Mbeya wengine Kibamba, Mbezi yote hiyo ni kwa ajili ya kutaka kusikiliza kesi ya ndugu zetu ila tunashangaa kuona imeitwa chamber. Wanatuficha nini, jambo hili limetusikitisha na kutuumiza,” alisikika mmoja wa ndugu hao akilalamika.

Hata hivyo askari polisi wa mahakamani hapo waliwataka ndugu, rafiki na jamaa hao kutawanyika eneo hilo kwa sababu shughuli za mahakama zilikuwa zikiendelea ambapo walitii agizo hilo na kuondoka.

Awali Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Leornad Swai, aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kutolewa maelezo ya mashahidi na kwamba wapo katika hatua za mwisho za kuwasilisha taarifa kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao.

Pia ameiomba mahakama imruhusu kumchukua mshtakiwa wa tano, Xavery Kayombo, kwa ajili ya kuhojiwa chini ya uchunguzi kuhusiana na tuhuma ambazo hajawahi kuhojiwa zinazochunguzwa.

Wakili wa Utetezi, Benjamin Mwakagamba, alipinga hoja hiyo akidai kuwa tayari rekodi za mahakama zinaonesha kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika ambao ni pamoja na kuwahoji washtakiwa.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Ally alisema amezisikia hoja za pande zote mbili na anakubali kuwa hatua ilipofikia kesi hiyo washtakiwa wameshahojiwa na kutoa maelezo yao.

Alisema kwa kuwa upande wa mashtaka umesema bado wapo katika hatua za mwisho za kuwasilisha taarifa mahakama kuu haoni sababu ya kuzuia mshtakiwa wa tano kuhojiwa na Takukuru hivyo, alitaka hatua hiyo ifanyike jana kabla ya muda wa washtakiwa kurudi gerezani kumalizika.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 19 mwaka huu.
Mbali na Maimu na Kayombo washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa (NIDA), Aveln Momburi, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima na Sabina Raymond.


Wanakabiliwa na mashtaka 22 ya kughushi, mashtaka 43 ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, mashtaka mawili ya kula njama, mashtaka 25 ya kutakatisha fedha na mashtaka matano ya kuisababishia hasara NIDA.

Pia wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la matumizi mabaya ya madara ambalo linamkabili Maimu na Sabina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles