Arodia Peter na Asifiwe George, Dar es Salaam
NI mtikisiko, ndivyo tunavyoweza kusema kwa mmoja wa wanachama wa mwanzo wa chama cha TANU na ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale-Mwiru, aliyetangaza kujiondoa katika chama hicho.
Kingunge ambaye alikuwa mwanachama namba nane wa CCM, alitangaza hatua hiyo Dar es Salaam jana, akisisitiza kuwa chama hicho hivi sasa kimekiuka misingi na dhamira ya uanzishwaji wake na hivyo kuendelea kukaa katika chama hicho ni kusaliti nafsi yake.
Hata hivyo aliweka wazi msimamo wake wa kuunga mkono mabadiliko wanayoyataka Watanzania wengi ambayo alisema yako bayana kutokea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
“Nimefikia uamuzi huo kwa kuwa uongozi wa sasa wa CCM umeamua kukibinafsisha chama na kufanya yale wanayoyataka wao kwa maslahi ambayo sina hakika ni ya nani.
“Mambo yanafanyika ya ajabu, vijana wanatumika kudhalilisha watu, mavuvuzela wanaajiriwa i kutukana watu, sikubaliani na hilo, chama ni nidhamu na nidhamu hiyo ni kuheshimu Katiba.
“Hiki si chama tulichokubaliana kukijenga, sasa nasema kuanzia sasa najitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM)… siwezi kuendelea na chama kisichoheshimu Katiba,” alisema Mzee Kingunge na kuendelea:
“Nawaachia chama, sikusudii kujiunga na chama chochote cha siasa kwa kuwa mimi ni mwanaharakati, nimeshiriki kujenga demokrasia ndani ya chama na ni mwanzilishi wa kutafuta uhuru na kujenga Tanzania mpya. Siwezi kuvumilia kuona demokrasia inapigwa mateke lakini wakubwa wanasimama na kusema kila kitu kimeenda sawa”.
Kingunge ambaye pia alikumbushia jinsi mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka huu ulivyovurugwa, alisema anajua lazima uamuzi wake huo utawasumbua baadhi ya makada ndani ya CCM, wazee, vijana na watu wengine nje ya chama hicho, lakini ni uamuzi ambao lazima aufanye vinginevyo atakuwa anajisaliti mwenyewe.
Alisema ingawa amejitoa CCM lakini bado ni raia huru na ana haki zake za raia, siasa na jamii na kwamba ataendelea kuwa na msimamo juu ya nchi yake na yupo tayari kuungana na wapenda mabadiliko.
Mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya CCM mwaka huu ulivurugwa kwa makusudi huku majina matano yaliyochomolewa kutoka Kamati ya Maadili ambayo iko chini ya Katibu Mkuu yakipitishwa kinyume cha utaratibu wa chama, alisema.
Alisema utaratibu uliotumika wakati Rais Ali Hassan Mwinyi akiwa Mwenyekiti wa CCM mwaka 1995 na ule wakati wa Benjamin Mkapa mwaka 2005 ni tofauti na uliotumia katika uongozi Jakaya Kikwete mwaka huu, jambo ambalo alisema ni la historia katika nchi hii.
CCM IMELEWA MADARAKA
Kingunge alisema hivi sasa nchi ina makundi mawili ambayo ni wale wanaoimba ‘kidumu chama tawala’ na wale wanaotaka mabadiliko ambao ni wengi.
“Vijana wengi wanataka mabadiliko tukiondoa kakundi ka UVCCM (Umoja wa Vijana wa CCM). Kila ninapopita watu wanataka mabadiliko, wakulima, wavuvi, wafanyakazi wachimbaji migodini, wanafunzi wa elimu ya juu, vyuo vikuu na wasomi wanataka mabadiliko.
“Ninachotaka kusema ni kundi lipi kubwa, hali ikoje, kwa jinsi ninavyotazama vijana walio wengi wanahitaji mabadiliko kwa sababu kila ninapopita ninasikia hivyo.
“Mwalimu alitufundisha jambo moja kwamba sikilizeni wananchi wanasema nini mnapotaka kuteua kiongozi wa nchi kwa sababu huyu si sawa na katibu kata, alituambia tuchague mgombea anayekubalika ndani na nje ya CCM.
“Katika hili niko upande wa mabadiliko na ninaona yamechelewa kwa sababu ni asili yetu wapigania uhuru ni watu wa mabadiliko, tuliiua TANU na ASP ili kuunda CCM, hayo ni mabadiliko.
“Kimsingi CCM iliendeshwa kwa misingi ya vikao, hata miaka ile ya 1990 wakati tunaamua nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi, tulitumia vikao vya katiba, ambavyo sasa vinakiukwa,” alisema.
Kingunge aliendelea kukishutumu CCM kuwa kimefikia hatua ya kubadili kibwagizo chake cha asili kisemacho “Kidumu Chama Cha Mapinduzi, badala yake kimebadilishwa na kuwa ‘Kidumu chama tawala’.
Alisema hatua hiyo ni ulevi wa madaraka na inaonyesha jinsi chama hicho kinavyotaka kidumu milele. Aliponda lugha zinazotumiwa na chama hicho dhidi ya upinzani akisema zinaonyesha ni za uhasama.
Watu wakubwa wanaokaa kwenye chama na kusema upinzani hauwezi kuchukua nchi ni dalili mbaya ya ‘ulevi wa madaraka’ kwa chama hicho kilichoongoza kwa zaidi ya nusu karne, hivyo kinafaa kupumzika, alisema.
Alisema ukongwe wa CCM wa kukaa muda mrefu mdarakani umekifanya kujisahau na hakiwezi kamwe kutekeleza ahadi nyingine mpya.
“Mtu anasimama jukwaani anasema hao ‘maadui’ zetu, ninaomba tuheshimu heshima ya nchi yetu iliyonayo duniani, tufanye uchaguzi wa haki, watu wakimtaka mtu mwacheni kwa sababu Tanzania ni nchi yetu sote, kila raia ana haki, tufanye mchezo ulio sawa.
“Tunakwenda kwenye kampeni, kiongozi wa chama Nape (Nnauye) anasema tutashinda hata kwa goli la mkono, goli la mkono ni faulo. Maana yake CCM ishinde hata kwa kuvunja sheria.
“Naamini huo ndiyo msimamo wa chama kwamba lazima washinde hata kwa mtutu wa bunduki! Je, mimi niendelee kubaki humu? Hiki si chama changu, labda kama nimepotea njia alisema na kuongeza:
“Madaraka hulevya, hata chama tawala cha Mexico kilitawala miaka 65 lakini baadaye wananchi walikiangusha. CCM kimekaa muda mrefu, nusu karne ya CCM ni muda mrefu sana kuongoza nchi, hii ni sawa na kupanda mlima unafika mahala pumzi zinakwishia, huwezi kuendelea mbele, CCM kimeishiwa pumzi.
“Ndiyo maana nasema mabadiliko ni muhimu kwelikweli, tupate watu wengine wenye pumzi mpya, mimi sitaki chama changu kifutike, bali kiwekwe benchi kidogo ili kijifunze na kujisahihisha”.
AKOSOA SERIKALI YA JK
Katika mkutano huo ambao ulirushwa moja kwa moja na luninga ya ITV, kada huyo wa zamani wa CCM alikosoa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwamba imeshindwa kuchangamsha na kukuza uchumi wa nchi.
Alimsifu Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa kwamba katika kipindi chake alifanya kazi nzuri ya kuboresha uchumi. Alisema Mkapa alimkabidhi nchi Kikwete uchumi ukiwa unakua kwa asilimia saba lakini miaka 10 baadaye kiwango hicho kimebaki kilekile.
“Hii maana yake tumebaki palepale kwa miaka 10, sasa tunataka mabadiliko ili uchumi ukue na kufikia asilimia 10 na hata 15. Sasa hii CCM inaweza kutufikisha huko?” alihoji na kuongeza:
“Tatizo la wananchi ili wapate ajira umasikini uondolewe ili nchi iwe na uchumi bora na uliochangamka. China inakuza uchumi wake kwa asilimia 15 hadi 30, Tanzania inaweza ndani ya miaka mitano kufika asilimia 10 kama tutafanya mabadiliko,”alisema Kingunge.
Amnanga Dk. Magufuli
Kingunge pia aligusia suala la uzoefu wa wagombea urais ndani ya CCM akisema Magufuli hana uzoefu wowote katika chama na hata katika mambo ya ulinzi na usalama.
“Nilipoamua kumuunga mkono Edward Lowassa nilitazama majina yote nikaona ndiye pekee anaweza kuipeleka nchi pazuri zaidi.
“Edward ana uzoefu na historia ya uongozi ndani ya chama, hao wanaomzungumza hawajawahi kufika huko alikofika yeye. Mathalani Edward amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kwa kipindi kirefu.
“Huyu mdogo wangu Magufuli (Dk. John)… miaka hii mnakwenda mnamchukua tu, nendeni huko kwao muulize alikuwa nani,” alisema Kingunge.