24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa kulipa posho wenyeviti wa vijiji

Pg 1FREDY AZZAH, HANANG

MGOMBEA Urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendele (Chadema), Edward Lowassa, amesema akiingia madarakani, Serikali yake itawalipa posho wenyeviti wa Serikali za vijiji, wenyeviti wa mitaa na wenyeviti wa vitongoji kwa kuwa wanafanya kazi kubwa.

Lowassa ambaye jana alifanya mikutano mitano ya kampeni   Magugu, Dongobesh, Bashinet na Haidom, aliyasema hayo akiwa kwenye mkutano wa kampeni Makondeko, Kateshi, wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara.

“Serikali yangu ikiingia madarakani  wenyeviti wa vijiji, vitongoji, mitaa tutawalipa posho. Lazima tugawane keki ya nchi kwa sababu hawa wanafanya kazi kubwa, lazima walipwe,” alisema Lowassa.

Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alimpongeza mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru kwa kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nampongeza Kingunge kwa kukubali mabadiliko,” alisema Lowassa.

Akiwa kwenye mji mdogo wa Magugu, Lowassa alisema Serikali yake itajenga hospitali mpya za kisasa zenye vifaa vyote na wataalamu.

Kuhusu elimu alisema wapo watu wanaokejeli sera ya kutoa elimu bure kuanzia shule za watoto wadogo mpaka chuo kikuu wakihoji atapata wapi  fedha.

Kama nchi ina   gesi, madini na inaweza kununua mashangingi haiwezi kushindwa kutoa elimu bure, alisema.

“Nagombea ili nipambane na umasikini, ninaamini hakuna urithi utakaoweza kumpa mtoto wako kama siyo elimu  ndiyo maana nasema kipaumbele changu cha kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu,” alisema.

Baada ya elimu, alisema atahakikisha anaboresha kilimo ikiwa ni pamoja na kutafuta soko la uhakika kwa bidhaa za wakulima na kuwaruhusu kuuza mazao yao popote penye soko.

Naye  Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, akiwa   Magugu, alisema kuna njama chafu zinaendeshwa za kuwaeleza wananchi siku ya kupiga kura watakuta jina la Ukawa na siyo vyama vinavyounda umoja huo.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.

“Kwenye karatasi ya kura hamtakuta jina la Ukawa, mtakuta majina ya vyama, rais mtampigia anatoka Chadema na wagombea wengine wako kwenye vyama husika,” alisema Sumaye.

Aliwataka  wananchi hao kuhakikisha wanawahi kwenye vituo vya kupigia kura ili wasikose fursa hiyo kutokana na njama za wapinzani wao wa siasa.

Akiwa Kateshi, alisema baadhi ya viongozi wa CCM wanasema wanataka kufuta historia yake ya utendaji, jambo alilosema ni ndoto.

“Hawawezi hawa, mimi nilitoka madarakani nyama ilikuwa ikiuzwa kilo moja Sh 500, sukari kilo Sh 600 na vitu vingine vingi bei ilikuwa chini.

“Kama wanataka kufuta historia yangu, wahakikishe wanashusha bei za bidhaa  viwe kama tulipokuwa sisi madarakani,” alisema Sumaye.

Alisema hata kwenye jimbo la Hanang, aliliacha likiwa na maendeleo ikiwa ni pamoja na hospitali kuwa na dawa lakini kwa sasa hakuna tena hizo huduma.

Akizunguzia hoja za Sumaye, Lowassa alisema wakati kiongozi huyo akiwa CCM alidharauliwa lakini kwa sasa Tanzania nzima inamheshimu.

“Amejenga hoja nzuri ya CCM kutoendelea kubaki madarakani, CCM walimdharau, lakini tangu aje Ukawa, Tanzania nzima inamtambua na kumheshimu,” alisema Lowassa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Wilaya ya Hangang, Idi Kitiyanga, alirudisha kadi ya chama chake na kuchukua ya Chadema.

Kityanga aliyekuwa pia diwani wa Kata ya Masakta, alisema amechukua uamuzi huo kwa kutambua kuwa hakuna mabadiliko yanayoweza kufanywa na CCM.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles