CHAMA cha Soka nchini England (FA), kimesema kuwa Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, hakutumia lugha chafu kwa daktari wa timu hiyo, Eva Carneiro, hivyo hataadhibiwa.
Inasemekana kocha huyo alitumia lugha chafu kwa daktari huyo katika mchezo wa awali wa Ligi Kuu nchini England dhidi ya Swansea City, huku timu hizo zikimaliza mchezo huo kwa kutoka sare ya 2-2.
Daktari hiyo alitumia muda mwingi kumtibu mchezaji wao, Eden Hazard na kusababisha malumbano na kocha huyo kisha kusimamishwa kazi, hata hivyo, baada ya muda uongozi wa klabu hiyo ulimtaka daktari huyo kurudi kazini, lakini aligoma na kudai kuwa Mourinho alimdhalilisha.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho cha soka kilifanya uchunguzi juu ya suala hilo na kugundua kwamba Mourinho hakutumia lugha yoyote chafu kwa daktari huyo wa timu, hivyo hawezi kuadhibiwa na kama angekutwa na hatia basi angefungiwa michezo mitano.
Hata hivyo, daktari huyo anaonekana kutoridhishwa na matokeo hayo ambapo yuko mbioni kusaka sheria katika mamlaka husika.