IMEDAIWA kuwa usimamizi mbaya wa zoezi zima la hijja ndio uliosababisha vifo vya mahujaji waliokwenda kuhiji katika mji mtakatifu wa Makka, Saudi Arabia.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na baadhi ya mahujaji ambao wamenusurika kufa katika tukio la kukunyagana lililotokea hivi karibuni katika mji wa Mina.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa mahujaji hao waliorejea nchini, Abdulmalik Almas, alisema utaratibu wa kurusha mawe eneo la ‘Jamarat’, ulivurugwa baada ya kubadilishiwa njia na wanajeshi wa Saudi Arabia.
“Wakati tunarudi kutoka Jamarat kumpiga shetani tulikutana na wanajeshi wa nchi hiyo na kututaka tupite njia tofauti na ile ya kutokea ambayo ilikuwa ni nyembamba sana kiasi cha kubanana,” alisema Almasi.
Alisema yeye aliweza kupenya na kufika katika hema walilofikia, ambapo muda mfupi wanawake walianza kulia kwa madai kuwa waume zao walikuwa hawajulikani walipo.
“Tulifanikiwa kuwatuliza,…baadaye walikuja wanajeshi na kututaka tusiende eneo la tukio kwa kuwa serikali ndio itakayowahudumia majeruhi,” alisema Almas.
Alisema japokuwa binadamu lazima afe, lakini si kwa uzembe unaosababishwa na binadamu wenzake na kuesema kuwa tukio hilo limechangiwa na uzembe wa dhahiri uliofanywa na Serikali ya Saudi Arabia.
“Nakanusha kauli zinazozagaa kuwa sababu ya vifo hivyo ni kusukumana kwa mahujaji wenyewe na chanzo cha kusukumana ni mahujaji wa kiafrika. Si kweli chanzo ni wao kwa sababu ndio waliotubadilishia njia ghafla,” alisema Almas.
Sheikh Saleh
Naye Sheikh Mulaba Saleh aliyeongozana na hujaji huyo aliiomba Serikali ya Tanzania ifanye uchunguzi na kujiridhisha kama hija hiyo ni salama kwa wananchi wake, kabla ya kupeleka mahujaji nchini humo.
Hata hivyo, Saleh alisema taasisi zinazopeleka mahujaji nazo zinapaswa kuchunguzwa, kwani kumekuwapo na taasisi za matapeli wanaokusanya fedha kwa Waislamu bila kuwapeleka Hijja.
Aliiomba Serikali ya Saudi Arabia iunde tume itakayoshirikisha nchi zilizopata misiba hiyo na ikibainika kulikuwa na uzembe, wahusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa Hijja ni ibada takatifu hivyo, Waislamu duniani kote wailinde kwa kuunda muungano wa taasisi itakayosimamia Hijja kwa pamoja.
Amiri
Naye Rais wa Jumuiya ya Aljazira International Hajj Trust, Amiri Seifulah, ameonesha masikitiko yake kutokana na vifo hivyo na kueleza kuwa hadi sasa baadhi ya miili ya mahujaji imeanza kuharibika.
Amiri alisema hayo jana wakati akizungumza na MTANZANIA mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam akitokea Makkah alipokwenda kutekeleza ibada ya hija ambayo ni nguzo ya tano katika dini ya kiislamu.
“Hadi sasa wenzetu waliofariki ni wanne na hali kwa kweli ni mbaya maana maiti zimeanza kuharibika hali inayopelekea washindwe kutambulika kwa urahisi, kwani awali walikuwa wanatumia alama za vidole kuwatambua, lakini sasa inawawia vigumu kutokana na kuharibika,” alisema.
Hujaji huyo alisema Serikali ya Saudi Arabia inaendelea na uchunguzi wa maiti ambazo hazijatambuliwa na kwamba taarifa zote zitakuwa zikitolewa na ubalozi husika.
“Tunamshukuru Mungu kila kitu kilikwenda vizuri lakini wakati tunakwenda kumpiga shetani ndio balaa hilo likatokea, tunawaombea waliotutangulia wapumzike kwa amani,” alisema.
Wakati mahujaji hao walipotangazwa kuwasili uwanjani hapo jana ndugu, jamaa na marafiki walijawa na furaha na kuanza kuomba dua na kuimba kaswida mbalimbali za dini hiyo, huku wengine wakibubujikwa na machozi.
Mahujaji 80 waliwasili jana saa 10.15 jioni na Ndege ya Shirika la Emirate, ambapo kundi jingine la mahujaji lilitarajiwa kuwasili saa 3.30 usiku.
Taarifa ya wizara
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imepokea taarifa za kuwapo kwa mahujaji wawili kutoka Tanzania ambao wamelazwa katika Hospitali ya Moya nchini Saudi Arabia, baada ya kujeruhiwa kutokana na tukio la mkanyagano.
Mahujaji hao ambao wanaendelea kupata matibabu na hali zao zikiendelea vizuri ni Hidaya Mchomvu na Mahjabin Taslim Khan.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo hujaji mwingine anayejulikana kwa jina la Mustafa Ali Mchira amelazwa katika Hospitali ya Ansari Madina, katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa Mchira alipata ugonjwa tangu alipowasili Saudi Arabia na hivyo ugonjwa hauhusiani na ajali iliyotokea Septemba 24 mwaka huu.
Kwa upande wa Serikali ya Saudi Arabia imeanza kutoa taarifa za alama za vidole vya mahujaji waliopata ajali, hivyo ubalozi unazipitia na kuzihakiki taarifa hizo ambazo zitasaidia kuwabaini mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia katika ajali hiyo.
Kutambuliwa kwa mahujaji hao waliolazwa kumetokana na jitahada zilizofanywa na ubalozi wa Tanzania nchini humo kwa kushirikiana na taasisi ya Tanzania Hajj Mission.
Maofisa wa taasisi zilizosafirisha mahujaji walitembelea hospitali mbalimbali katika miji ya Makkah, Mina, Arafat, Muzdalifa, Jeddah na Twaif kwa ajili ya kuwatafuta mahujaj wa Tanzania waliofariki dunia au kulazwa katika hospitali hizo.
Tukio hilo lililotokea Septemba 24, mwaka huu limegharimu maisha ya mahujaji zaidi ya 4,000 ambapo kati ya hao Watanzania sita wamepoteza maisha, huku wengine 50 wakiwa hawajulikani walipo.
Habari hii imeandikwa na Tunu Nassor, Esther Mnyika, Veronica Romwald na Koku David, Dar es Salaam