SARAH MOSES -DODOMA
KAMBI ya Upinzani Bungeni, imemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutengua uamuzi wake wa kusimamisha vikao vya kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa ( LAAC ).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Mwakilishi wa Kambi ya Upinzani, John Mnyika alisema kauli aliyoitoa spika siyo ya Bunge, bali ni yake binafsi.
“Haiwezekani mgogoro wa Spika na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Musa Assad, ukasimamisha mambo mengine ya bunge kuendelea.
“Kama kamati tunamtaka spika abadilishe uamuzi wake kwa kamati hizi mbili na awezeshe kamati hizo kukutana kabla ya tarehe 25 mwezi huu,”alisema Mnyika na kuongeza:
“Tumesikia spika amesimamisha kamati hizo kwa kuwa CAG ameitwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Januari 21, mwaka huu kwa kile alichokiita mgogoro wa CAG na Bunge … kauli hiyo siyo ya Bunge ila ni yake binafsi”.
Alisema uamuzi alioutangaza Spika hawakushirikishwa hivyo hilo ni tangazo lake mwenyewe
Alisema tayari Spika ameonyesha Bunge kutoshirikiana na CAG jambo ambalo hawakubaliani nalo wao kama timu pinzani.
“Bunge hili ukiondoa kamati za PAC na LAAC, bado lina wajibu wa kupokea taarifa ya mwaka kuanzia Januari 2018/2019 kwa kamati zote,”alisema.
Alisema Januari 24 na 25, Kamati ya LAAC ilitakiwa kuanza kuwasilisha ripoti za kamati, hivyo kupitia uamuzi wa spika kamati hizo haziwezi kupata fursa ya kukutana na CAG na kuzungumza.
Wakati huo huo, Mnyika alisema Spika asiwalazimishe wabunge kwenda mbele zaidi kutumia kanuni za bunge kumtoa kwenye cheo chake.
“Mbunge mmoja wa upande wowote ule anaweza kutumia kanuni au ibara ya 137 ya kumwondoa spika, hivyo asitulazimishe wabunge na abadilishe uamuzi wake haraka sana”alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Naghenjwa Kaboyoka ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), amesema mapendekezo ya kamati hizo yakikosekana hawataweza kuisimamia serikali kupitia bunge.
“Kamati hizi mbili zinasimamia fedha za umma zinatumikaje na vilevile tumepewa jukumu na watu wa CCM kuweza kusimamia fedha,”alisema Kaboyoka.
Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alisema maoni yaliyotolewa si ya Mnyika bali ya kambi nzima ya upinzani.
“Hili ni tukio la kwanza kutokea nchini kati ya mgogoro wa Bunge na CAG na kauli ya CAG inaleta utata kwa wahisani kwa nchi kukosa fedha kwa kutaka kuonyeshana ubabe,” alisema Silinde.