23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kangi atengua uteuzi makamanda wa polisi

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametengua uteuzi wa makanda watatu wa polisi kutokana na kushindwa kutii maagizo yake pamoja na rushwa.

Waliotenguliwa kuwa makamanda wa polisi wa mikoa ni makamanda wa polisi wa mikoa ya polisi ya Ilala (Salum Hamduni) na Temeke (Emmanuel Lukula) na Kamanda wa Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’azi.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dodoma jana, Waziri Lugola alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo, juzi alikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama  ambao waliwapa maelekezo ya nini wanatakiwa kufanya kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Alisema   suala la makamanda wa polisi ambao wamesimamishwa imetokana na kushindwa kusimamia suala la rushwa jambo ambalo wameshindwa kulifanyia kazi eti kwa sababu yeye (aliyetoa agizo) ni mwanasiasa.

“Kuna maelekezo nilitoa lakini kuna mikoa inabeza maelekezo hayo na maagizo hayafanyiwi kazi na mrejesho ninaopata ni kwamba maelekezo haya  hayafanyiwi kazi kwa sababu anaeyatoa ni mwanasiasa.

“Eti kwamba mwanasiasa anapita tu, sisi tupo na atatuacha, sasa baada ya kubaini hali hiyo nikafanya tathmini kwa mikoa na  kuona ma-RPC wa mikoa gani ni vinara wa kutotekeleza maagizo ninayotoa.

“Maagizo ya kufyeka moto na kuteketeza vichaka vyote vinavyotengeneza mazingira ya rushwa nikajiridhisha kwamba maagizo yangu hayafuatwi.

“Ili kutuma salamu kwa ma-RPC wa mikoa mingine kwamba mimi siyo mwanasiasa na siasa yangu naifanya Mwibara (jimboni) na nje ya mipaka ya Mwibara.

“Kangi Lugola siyo mwanasiasa bali ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi aliyeaminiwa na Rais Dk. John Magufuli. Sasa nimeamua kula vichwa, vichwa vya vinara wawili ambao wanahusika kutotii na kutekeleza maagizo ninayoyatoa,” alisema Lugola.

Waziri Lugola alisema kinara wa kwanza ni aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Polisi Ilala, Salum Hamduni na mwenzake wa Temeke, Emmanuel Lukula.

“Na kwa maana hiyo mimi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi nimetengua uteuzi wa ma-RPC hao wawili kwa kushindwa ama kukaidi kutekeleza maagizo na kushindwa kusimamia askari, kushindwa kupambana   na rushwa ndani ya Jeshi la Polisi,” alisema.

Akitaja sababu za kumsimamisha kazi Kamanda wa Polisi wa Arusha, Ramadhan Ng’azi  kuwa ni kutokana na kushindwa kusimamia dawa za kulevya mkoani humo.

Waziri Lugola alisema kuna baadhi ya viongozi, askari wanapotoa  taarifa za kuwapo  wafanyabishara wa magendo, mirungi na dawa ya kulevya, lakini askari hao hujikuta kwenye misukosuko.

“Nitolee mfano, Mkoa wa Arusha juzi juzi hapa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alifanya ziara mkoani humo, alipata fursa ya kufanya mkutano na polisi.

“Katika mkutano ule aliwaomba askari wawe huru waeleze kero zao na mambo yanayoleta shida.

“Katika mkutano ule yupo askari mmoja ambaye ni mzalendo akamwambia Naibu Waziri nakukabidhi orodha ya askari wenzetu ambao wanajihusisha na mirungi, bangi na  kusindikiza wafanyabiashara ambao siyo waaminifu.

“Lakini siku chache hizi baada ya askari huyo kufanya uzalendo wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha akamwadhibu.

“Kwa hivyo mimi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kitendo alichokifanya RPC wa Arusha na yeye kichwa chake halali yangu kinatafunwa, nimetengua uteuzi wake,” alisema Lugola.

Alisema kumekuwa na baadhi ya askari ndani ya Jeshi la Polisi ambao wanashirikiana na wafanyabiashara wa magendo na madawa ya kulevya nao wanatakiwa kujitafakari.

MUSLIM  NA TAFAKARI

  Waziri Lugolapia  alimtaka Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim, kujitafakari kutokana na rushwa kuzidi barabarani.

“Kikosi hicho kina makamnda ambao wanasimamia… kuna makamanda wa mikoa lakini rushwa ipo pale pale wanatakiwa kujitafakari.

“Yamekuwapo malalamiko mengi barabarani, baadhi ya askari wanachukua rushwa na madereva hasa wa mabasi wanapokataa kutoa rushwa wanaandamwa kweli kweli na kubambikizwa kesi mpaka waufyate.

“Kwenye kikosi cha usalama barabarani kumekuwa na uonevu siyo wa kawaida katika kushughulikia makosa ya vijana wa bodaboda, nimesoma ibara ya nne ya Katiba na inasema kuna tatizo la ajira,” alisema.

Katika hatua ningine, Waziri Lugola amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu, kuunda timu ya kuchunguza ni kwa nini rushwa haiishi barabarani.

Alitoa miezi mitatu majibu ya kueleweka yawe yamepatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles