33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ateta na Dk. Obasanjo

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amekuwa na  mazungumzo na Rais mstaafu wa Nigeria, Dk. Olusegun Obasanjo Ikulu, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa   na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema baada ya mazungumzo hayo, Dk. Obasanjo alimpongeza Rais Dk.Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika uongozi wake.

Alisema moja ya kazi hizo  ni kupambana na rushwa, kuimarisha utoaji wa elimu, kuimarisha miundombinu, kuongeza nishati ya umeme, kuboresha usafiri wa ardhini na angani na jinsi wadau mbalimbali wa ndani na nje wanavyopaswa kuelewa juhudi zinazofanyika.

Dk. Obasanjo  alisema pia Rais Magufuli amedhihirisha kuwa kiongozi imara wa kusimamia mambo muhimu yenye maslahi kwa nchi yake.

Alisema ingawa maendeleo ya nchi hayapatikani mara moja, lakini kwa muda mfupi amefanya juhudi kubwa za kuimarisha maeneo ya huduma za  jamii, kukiimarisha chama chake cha siasa (Chama Cha Mapinduzi – CCM) na   ameonyesha kuwa anakijua anachokifanya katika maeneo ya uchumi.

“Tusijisahau  ukoloni mamboleo bado upo na mabeberu bado wanaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha wanatunyonya.

“Kiongozi yeyote wa Afrika anayethubutu kuwazui hawezi kuwa rafiki wa hao ambao walikuwa wakinufaika kwa kutunyonya,” alisisitiza  Dk. Obasanjo.

Mapema Rais Magufuli, alipokea hati za utambulisho za mabalozi watatu walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao nchini ambao ni kutoka  Jamhuri ya Korea, Malawi na Brazil,  baada ya waliokuwapo  kumaliza muda wao.

Waliowasilisha hati hizo ni Balozi wa Jamhuri ya Korea  nchini, Cho Tae-ics aliyechukua nafasi ya Song Geum-young,  Balozi wa Malawi nchini, Glad Chembe Munthali aliyechukua nafasi ya  Hawa Olga Ndilowe na Balozi wa Brazil, Antonio Augusto Martins Cesar aliyechukua nafasi ya  Carlos Alfonso Iglesias Puente.

Mabalozi wote walimhakikishia Rais Magufuli kuwa katika kipindi chao watakahakikisha wanaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo na matunda ya uhusiano na ushirikiano huo yanawanufaisha wananchi wa pande zote.

Rais Magufuli alimpongeza Cho Tae-ics kwa kuteuliwa kuiwakilisha Jamhuri ya Korea   nchini na amemtaka apelekee salamu zake za shukrani kwa Rais wa Korea, Moon Jae-in kwa ushirikiano mzuri ambao Tanzania inaupata kutoka Korea ikiwemo kujengwa miundombinu kama vile Daraja la Kikwete kwenye mto Malagarasi mkoani Kigoma, Hospitali ya Mafunzo na Tiba Mloganzila na Daraja la Tanzanite linalounganisha ufukwe wa Aga Khan na Coco Beach, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles