30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Spika: Tumesitisha kufanya kazi na CAG

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SPIKA wa Bunge Job Ndugai, amesema kwa sasa Bunge limesitisha kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Kutokana na hali hiyo, amewatawanya wajumbe wa Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Tawala za Mikoa na Mitaa (LAAC) kufanya kazi katika kamati nyingine.

Hatua ya usitishaji huo inatokana na kauli ya Profesa Assad aliyoitoa Desemba mwaka jana katika mahojiano na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda.

Mtangazaji huyo alimuuliza CAG kuwa ni vipi ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonesha kuna ubadhirifu, lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

Katika majibu yake CAG alisema; “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge.

“Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

 “Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika, ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”

KAULI YA NDUGAI

Akizungumza na MTANZANIA jana, Spika Ndugai alisema suala hilo si la utani kama baadhi ya wanasiasa wanavyolichukulia.

“Hili jambo sio la utani utani kama hao kina Zitto (Mbunge wa Kigoma Mjini) wanacheza huko Dar es Salaam, sisi hili jambo lililotokea limetusikitisha sana kiukweli.

“Huwezi kutuita sisi dhaifu halafu wewe ni mtu unatakiwa kufanya kazi na sisi.

“Sisi hatutegemei utuite dhaifu yaani kama mazezeta, hiyo ni kuonyesha kwamba si kwamba tumevunja hizo kamati. Ila kwa sasa tumesitisha kazi ya hizo kamati kwa muda. Kwa hiyo wabunge kama wabunge watafanya kazi kupitia kamati nyingine.

“Tumesitisha kwa muda ili hili jambo la huyu ambaye ni mshirika wetu (CAG Profesa Assad) katika kufanya kazi, kwanza afike mbele ya Kamati ya Bunge aeleze kama sisi ni wadhaifu ama laa. Vinginevyo hatuna haja ya kufanya naye kazi ili atafute hao ambao ni ‘strong’ (wenye nguvu) afanye nao kazi.

“Yaani hili si suala la magazeti kama mnavyoandika ushabiki, hatuwezi kujenga nchi ya watu wa kudharaulianauliana, ‘no’ (hapana), haiwezekani.

“Haiwezekani watu mnafanya kazi zenu, watu na heshima zenu mnajitahidi kufanya mnavyoweza, lakini kwa hili acha aje kwanza tumsikilize nini atajibu kwenye kamati, na majibu yake ndani ya kamati mapendekezo yao tutayatoa kwa umma.

“Na kuhusu kamati, ningependa kwanza tubakie huko   maana hili sasa tayari lipo kwenye Kamati ya Maadili, sipendi sana kulirudiarudia, tunataka afike tarehe 21 (Januari) na baada ya hapo mapendekezo yao tutayatoa ‘public’ (kwa umma).

“Kiuweli kuhusu hili la kamati za Bunge tumesitisha kwa sasa shughuli za kamati hizo mbili (PAC na LAAC) mpaka jambo hili litakapokaa vizuri,” alisema Spika Ndugai.

KUITWA KUJIELEZA

Januari 7, mwaka huu Spika Ndugai alieleza kusikitishwa na kauli ya CAG Assad na kumwagiza afike mbele ya Kamati ya Bunge ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge kujieleza kutokana na kauli hiyo aliyodai amedhalilisha Bunge.

Ndugai alimtaka CAG afike mbele ya kamati hiyo kwa hiari yake Januari 21 ili akahojiwe, vinginevyo atafikishwa kwa pingu.

Licha ya CAG, pia Ndugai alisema Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) naye anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 22.

Alisema CAG akiwa nje ya Tanzania wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili Redio ya Umoja wa Mataifa (UN), alisema Bunge la Tanzania ni dhaifu.

“Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndio wapotoshaji, huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” alisema Ndugai.

Alisema kitendo hicho kimemkasirisha kwani hakutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu uhuru.

Baada ya agizo hilo la Spika Ndugai, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliiandika katika mtandao wa kijamii kwamba hakubaliani na hatua hiyo na kudai kwamba hana mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria.

Januari 13, mwaka huu pia Zitto na wabunge wengine wanne walitangaza kufungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania kumzuia CAG kuitikia wito wa Spika wa Bunge.

Wabunge wengine ni Saed Kubenea (Ubungo), Salome Makamba (Viti Maalumu), Hamidu Bobali (Mchinga) na Anthony Komu (Moshi Vijijini).

Zitto alisema wameona watu wengi wametoa maoni tofauti ndiyo maana wameona ni muhimu waende mahakamani kupata tafsiri ya kisheria.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Zitto kuandika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) akimuomba kuingilia kati mgogoro unaoendelea baina ya Spika Ndugai na CAG.

Januari 9, mwaka huu Zitto alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CPA, Akbar Khan, akimwarifu kuhusu hatua ya Spika Ndugai kumwagiza CAG aripoti kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge kuhojiwa kwa madai ya kulidhalilisha Bunge.

Wito huo wa Spika uliwaibua pia wadau mbalimbali waliopinga hatua ya kuitwa kwa Profesa Assad kuhojiwa, huku wakieleza kuna kuvunjwa kwa katiba ya nchi katika suala hili hasa kwa kuzingiatia mamlaka yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles