KINSHASA, DRC
MUUNGANO wa vyama vya upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa kauli moja umekubaliana kupinga matokeo ya urais yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, Ceni ambayo ilimtangaza mgombea wa chama cha UDPS, Felix Tshisekedi, kushinda kinyang’anyiro hicho dhidi ya wagombea wengine wa muungano wa upinzani, Martin Fayulu na wa chama tawala, Emmanuel Shadary, kufuatia uchaguzi uliofanyika Desemba 30, mwaka jana.
Akizungumza na vyombo vya habari nchini humo, Fayulu, amesema kuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanastahili kufahamu ukweli wa uchaguzi, ambao ameutaja kuwa ni kama ‘mapinduzi’.
Tume ya Uchaguzi nchini humo, Ceni Januari 6, mwaka huu ilimtangaza mgombea mwingine wa upinzani, Felix Tshisekedi, kuwa mshindi katika kinyang’anyiro hicho, lakini kumekuwa na tuhuma kuwa mshindi huyo ameingia makubaliano ya kisiasa na rais anayeondoka madarakani, Joseph Kabila.
Mshindi alipata kura ngapi?
Tume hiyo ilisema matokeo yaliyotangazwa na Ceni, Tshisekedi, alipata kura 7,051,013 akiwa na asilimia 38.57, Fayulu, alijikusanyia kura 6,366,732 sawa na asilimia 34.83, huku mgombea wa chama tawala, Shadary, akipata kura 4,357,359 sawa na asilimia 23.84. Ceni imesema jumla ya asilimia 48 ya wapigakura waliojiandikisha walijitokeza kupiga kura.
Tangu kutangazwa matokeo hayo, watu kadhaa wanaripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa. Uchaguzi huo unakamilisha safari ya miaka 18 madarakani ya Joseph Kabila.
Matokeo hayo, endapo yatathibitishwa, yataweka historia ya makabidhiano ya amani ya hatamu za uongozi toka nchi hiyo ilipopata uhuru wake toka kwa wakoloni wa Ubelgiji mwaka 1960.
Kanisa lenye ushawishi mkubwa la Katoliki ambalo lilikuwa na waangalizi wa uchaguzi 40,000, limesema matokeo yaliyotangazwa hayaendani na matokeo waliyonayo.
Fayulu amesema nini?
Akizungumza na Shirika la utangazaji la BBC, Fayulu, amesema atayapinga matokeo hayo kwenye mahakama ya katiba.
“Nitafanya kila liwezekanalo kwangu kufanya ukweli udhihiri sababu wananchi wa Congo wanataka mabadiliko. Kambi iliyoshinda imeundwa na watu wa Kabila. Felix Tshisekedi ameteuliwa na Joseph Kabila ili kutekeleza matakwa ya utawala wa Kabila. Kabila ndiye bosi,” amedai Fayulu.
Aliongeza kuwa: “Kabila hawezi kubaki na kusuka mpango na mtu ambaye hatakuwa na mamlaka yoyote… Tshisekedi anajijua kwamba hakushinda uchaguzi.”
Hata hivyo, Fayulu alisema hataki kuwapa kisingizio wapinzani wake kuwa hakufuata sheria. Pia ameweka wazi kuwa kuna uwezekano mdogo wa kushinda kesi hiyo sababu mahakama zinadhibitiwa na Serikali.
Fayulu alisema pia ana hofu kuwa kutatokea vurumai kama tume ya uchaguzi (Ceni) haitatoa takwimu sahihi za kituo kimoja kimoja cha kupigia kura na kusisitiza kuwa ni haki ya kila Mkongomani kuandamana kwa mujibu wa sheria.
Muungano wa upinzani ulishinda?
Kwa mujibu wa muungano wa upinzani wa Lamuka, Fayulu, ameshinda uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 61 ya kura dhidi ya 18% alizopata Felix Tshisekedi katika uchaguzi huo.
Lamuka ulinukuu takwimu zilizotolewa na maofisa wake 220,000 walitumwa katika vituo mbalimbali wakati wa uchaguzi mkuu huo.
Takwimu hizo zilitolewa na Fidele Babala, mmoja wa makada wa Lamuka, mbele ya mamia ya wafuasi wa muungano Lamuka katika makao makuu ya chama cha MLC, mjini Kinshasa. Babala alitangaza matokeo ya uchaguzi mkoa kwa mkoa.
Je, kumetokea vurumai zozote?
Maelfu ya mashabiki wa Tshisekedi waliingia mitaani kwa furaha kusherehekea ushindi walioupata, lakini upande wa pili wafuasi wa Fayulu wamejitokeza mitaani kupinga matokeo hayo.
Matukio ya ghasia yameripotiwa katika eneo la Kikwit, ambapo polisi wawili na raia 11 wanasemakana kuuawa.
Kuna ripoti pia mamia ya wanafunzi wamekuwa wakipinga matokeo hayo kwa kuandamana na kutimuliwa na mabomu ya machozi katika mji wa Mbandaka.
Maandamano pia yameripotiwa katika mji wa Kisangani, lakini Kusini ambapo Tshisekedi anaungwa mkono kwa wingi kumekuwa na sherehe.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, amezitaka pande zote kujizuia kufanya ghasia.
Wagombea wenye dukuduku na matokeo wanatakiwa kuwasilisha hoja zao mahakamani saa 48 toka kutangazwa kwa matokeo ya awali. Majaji itawachukua siku saba kupitia kesi na kutoa maamuzi.
Wataalamu wa masuala ya Katiba wanasema kuwa kuna matokeo ya aina tatu yanayotarajiwa; mosi mahakama inaweza kuthibitisha ushindi wa Tshisekedi, pili kuamuru kura zihesabiwe upya na tatu kufuta matokeo yote na kuamuru kura zipigwe upya.
Mahakama ya Katiba haijawahi kubatilisha matokeo kabla na wengi wanawaona majaji wake kuwa washirika wakubwa wa chama tawala. Iwapo ushindi wa Tshisekedi utathibitishwa basi ataapishwa ndani ya siku 10.
Salamu za viongozi wa nje ya DRC
Mkuu wa Kamisheni ya Afrika, Moussa Faki Mahamat, katika taarifa yake kuhusu matokeo ya uchaguzi huo, alisema: “Ni muhimu kwa mtanziko wowote wa matokeo, hususani kuwa hayajaakisi matakwa ya wananchi, inabidi utatuliwe kwa njia ya amani kwa kutumia sheria na makubaliano ya kisiasa kwa pande zinazohusika.”
Kwa upande wake, Marekani imewasifu wapiga kura kwa kuwaita mashujaa na kutaka maswali yote tata kuhusu kura na matokeo yapatiwe majibu sahihi.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Yves, katika taarifa yake iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters ameomba kuwepo na ufafanuzi kuhusu matokeo hayo akisema ushindi wa Tshisekedi unaenda kinyume na uhalisia wa mashindano.
“Kanisa Katoliki la Congo lilifanya hesabu yake na kutoa matokeo tofauti kabisa,” amenukuliwa na shirika hilo.
Nayo Ubelgiji ambayo iliitawala DRC wakati wa ukoloni imeungana na Ufaransa katika kutilia mashaka matokeo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje, Didier Reynders, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akiiambia redio ya taifa RTBF kuwa Ubelgiji itatumia nafasi yake ya muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka taarifa rasmi ya kilichotokea.
“Tuna mashaka na inabidi tuhakikishe na kujadiliana suala hili katika vikao vya Baraza la Usalama,” amesema Reynders.
‘Kabila kulidhibiti bunge’
Katika hatua nyingine muungano wa vyama vinavyounda Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, umepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa ubunge uliofanyika sambamba na uchaguzi wa rais Desemba 30, mwaka jana.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi ya nchi hiyo, Ceni baada ya kupata viti 288 kati ya 429 vya bunge vilivyotangazwa hadi jana, upinzani ukipata viti 141.
Ceni imesema kulikuwa na wagombea zaidi ya 15,000 katika nafasi za ubunge kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Hatua hiyo inapunguza nguvu za aliyetangazwa mshindi wa urais, Felix Tshisekedi.