24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Wahamiaji 624 wakamatwa Geita

NA HARRIETH MANDARI- GEITA

OFISA Uhamiaji wa Mkoa wa Geita, Naibu Kamishna, Wilfred Marwa, amesema bado kuna wimbi kubwa la wahamiaji wanaoingia nchini na kwa mwaka jana waliwakamata 624.

Kwa mujibu wa Kamishna Marwa, kati ya wahamiaji hao, walio wengi wanatoka Burundi ambao walikamatwa 229 wote wakiwa ni wafanyakazi katika mashamba.

Alisema wahamiaji wengine walitoka  Kenya, Uganda, Burundi, Misri, Australia, Ethiopia, Sudan, China, Afrika Kusini, Mali, India, Vietnam, Indonesia, Newzeland, Brazil, Ufilipino, Ufaransa na Ghana.

“Hao wote tuliwakamata kwa makosa mbalimbali yakiwemo kuishi nchini bila kibali, pia kuchelewa kuongeza muda wa kuishi nchini.

“Kisheria watu wa aina hii wanatakiwa  kuhalalisha upya ukazi wao na pia huwa tunawapa kibali kama hati maalumu  ambayo wanailipia kama adhabu kwa kukiuka sheria ya kuongeza muda bila kuhakiki upya,” alisema.

Vile vile kati ya wahamiaji hao, 175 ni wale waliokuwa na vibali vya kuishi nchini vilivyoisha muda wake.

Alisema kundi hilo ni la wahamiaji ambao wameajiriwa katika makampuni mbalimbali mkoani hapa ikiwemo migodini na kwamba wapo waliofunguliwa mashtaka.

Akifafanua juu ya wahamiaji haramu wa ‘Kitanzania’, Marwa alisema huingizwa hatiani kutokana na kupatikana na hatia ya kuwasaidia kwa kuwahifadhi, kuwaajiri na pia kuwakaribisha wahamiaji kutoka nje ya nchi.

 Marwa alisema iwapo Mtanzania yeyote  atakutwa na hatia ya kumsaidia au kumhifadhi mhamiaji wa kigeni, adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 au faini ya Sh milioni 20 au adhabu zote mbili.

Kamishna Marwa alitoa wito kwa walowezi walioingia nchini miaka mingi iliyopita ambao wanaishi mkoani hapa  kujitokeza kujiandikisha ili watambulike uraia wao kisheria na kwamba kwa kipindi cha mwaka jana jumla ya familia za walowezi 772 zilitambuliwa.

“Ninatoa wito kwao kuja ofisini ili waweze kusajiliwa kisheria kwa sababu mashine zote za alama za vidole zipo ofisini, bado mwitikio ni mdogo sana,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles