24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

WATEULE WANAPOSHINDWA KUMSAIDIA RAIS

Na LEONARD MANG’OHA

RAIS Dk. John Magufuli, amesema sekta ya madini inakabiliwa na changamoto nyingi na kubwa ikiwamo Tanzania kutoongoza orodha ya nchi zinazouza dhahabu katika ukanda wa Afrika Mashariki licha ya kuwa nchi yenye dhahabu nyingi.

Kutokana na ripoti ya nchi za Afrika Mashariki kutoonesha Tanzania kuwa kinara wa uuzaji dhahabu katika ukanda huu ni wazi kuwa kuna mahali kuna udhaifu ambao Wizara ya Madini haiwezi kukwepa.

Baadhi ya mambo ambayo Rais anadai kuwa ni udhaifu ni pamoja na Bunge kupitisha sheria nzuri za madini na madini yenyewe pia yapo lakini bado wizara haijawahi kuuliza mahali inapouzwa dhahabu inayopatikana nchini.

Pia yako maeneo mengi yalitolewa kwa wachimbaji wadogo na wakubwa wa dhahabu, lakini wizara haijui dhahabu inayochimbwa inauzwa wapi na kama wanauza haijui Serikali inapata asilimia ngapi kutokana na mauzo hayo.

“Kwa kuwa sheria tayari iko wazi, suala hilo ni la wizara na wala halihitaji Bunge au Waziri Mkuu kujiuliza kwa sababu wizara ipo na ina wataalamu, makatibu wakuu, makamishna, Tume ya Madini na watendaji wengi ambao wanatakiwa kusimamia majukumu yao kisawasawa.

“Ukimwambia mtu alime korosho si lazima ujue na soko lake liko wapi? Ukimwambia mtu alime mahindi pia lazima ujue soko lilipo, sasa hawa tumewaambia walime dhahabu, soko lao tunalijua la hao walimaji liko wapi?

Kwa mujibu wa Rais, sheria ya madini imeweka wazi namna ya kuingia mikataba na wawekezaji wakubwa pamoja na nchi nyingine, lakini iliweka pia namna ya kuwashirikisha wachimbaji wadogo katika sekta ya madini, soko la dhahabu na madini mengine, jambo ambalo wizara haijaonesha inashiriki vipi.

Katika hotuba yake Rais anahoji kuhusu uanzishwaji wa vituo vya madini kama sheria inavyoelekeza ambavyo vingesaidia katika ufuatiliaji wa kiasi cha madini kinachozalishwa, kinachouzwa na kuwezesha kupata taarifa ya kila wiki kuhusu kiasi cha dhahabu inayouzwa kwenye vituo husika.

“Ni kitu gani kinachotushinda, kama sheria ilishapitishwa na Bunge, wizara inayohusika imeshindwa kitu gani katika kuanzisha hili? Nimelazimika kuzungumza haya ili ndugu zangu mjue ‘challenge’ (changamoto) tulizonazo kwa sababu inauma unaposikia kilo zaidi ya 300 zimekamatwa zikisafirishwa isivyo kawaida,” anasema Rais.

Kutokana na hilo, Dk. Magufuli, anasadiki kusema Tanzania ina watu wasiojitambua wakiwamo wataalamu kama majiolojia, wahandisi huku akiomba radhi kwa hilo akikiri kuwa si maneno mazuri ya kuwaambia watu.

Na kutokana na hali hiyo, anahisi kuendelea kufanya mabadiliko kila wakati na kila atakayeshindwa kwenda na kasi yake atamwondoa huku akisisitiza kuwa huo ndio ukweli na hawezi kuuficha kwa sababu Serikali inahitaji fedha na rasilimali za Watanzania lazima ziwasaidie masikini katika kupata huduma bora za afya, elimu na nyingine.

Katika kile ninachokitazama kama kukasirishwa na kitendo cha wizara kushindwa kuanzisha vituo, anamwagiza Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko, kuanza na suala la uanzishwaji wa vituo hivyo na ikiwezekana akae na Wizara ya Fedha na Mipango hasa Gavana wa Benki Kuu na kuanzisha utaratibu wa kununua na kuweka akiba ya dhahabu kwa kutumia fedha ilizonazo na kuweka hazina, ambayo inaweza kuhifadhiwa na kusaidia kwa kuwa dhahabu ni fedha.

Vile vile kuhakikisha vituo hivyo vya madini vitakavyoanzishwa kusimamia mali ya Watanzania kwa kujua kiasi cha dhahabu kinachozalishwa, kuhifadhiwa na kuuzwa nchini kwa mwaka na kuitaka wizara husika kuamua pia kuhusu uwezekano wa kuchuja na kuzalisha dhahabu nchini na kuhakikisha inashughulikia masilahi ya Watanzania.

Katika hali inayoonesha kujawa kwake na hali ya uthubutu, anaeleza kuwa ni vyema kufanya kitu hata ukikosea kuliko kuogopa kukosea kwa kulinda kazi yako kwa kuwa kufanya hivyo utashindwa kuilinda hiyo kazi.

“Watendaji fanyeni kazi, mbuni kitu chochote ambacho mnafikiri mkikifanya hiki ni kwa masilahi mapana ya nchi. Hilo ndilo ombi langu. Kwa hiyo waziri wa madini, katibu mkuu na tume ya madini mkafanye kazi, si kazi yenu kutoa leseni tu,” anasema Rais.

Kupitia haya anayoyaeleza Rais nakubaliana na hoja yake kuwa kuna udhaifu miongoni mwa watendaji wake na ninahisi wako baadhi ya wasaidizi wake aidha wanashindwa kumwelewa au wanafanya mambo kwa hofu ya kupoteza nafasi zao hivyo wanashindwa kujiamini na kufanya mambo makubwa yaliyopewa baraka kisheria.

Kama pasingekuwa na udhaifu kasoro hizi ndogo ndogo zingetatuliwa mapema badala ya kumngoja Rais kuzisemea, kitendo cha kushindwa kushughulikia wizara haiwezi kuukwepa udhaifu unaoelezwa kuwapo.

Kwa sababu Rais ameamua kufanya mabadiliko katika wizara hiyo waziri wa sasa Biteko atazishughulikia changamoto hizo alizozitaja Rais ili kuongeza ufanisi katika sekta ya madini na kuliwezesha Taifa kupata mapato yanayoendana na wingi wa madini nchini.

Pamoja na mambo mengine ni imani yangu kuwa migogoro inayotajwa na Rais baina ya watelue wake pia ni kikwazo kwa baadhi yao katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Tutakumbuka kuwa katika hafla ya kuwaapisha mawaziri iliyofanyika ikulu mapema wiki hii, Rais alieleza namna ambavyo baadhi ya watendaji wake serikalini wanavyogombana badala ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika maeneo yao.

Katika kutolea mfano suala hilo, Dk. Magufuli, alieleza namna ambavyo alizinasa meseji za majibizano kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Zainabu Chaula.

Licha ya Rais kukiri kuwa wawili hao wote wanafanya kazi vizuri, bado siamini kama wangeweza kushirikiana vema pale linapokuja jambo ambalo linahusisha wizara zote mbili, kwa kuzingatia kuwa wizara hizo hutegemeana kwa kiasi kikubwa.

Mgogoro mwingine alioutolea mfano ni ule unaomhusisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa na Mkuu wa Wilaya hiyo. Katika hali ya kawaida mahala kama hapa hapawezi kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

Tunafahamu fika kuwa Mkurugenzi ndiye mtendaji mkuu wa shughuli zote za halmashauri na ndiye mwidhinishaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo husika, je, katika hali ya ugomvi kama hii ataweza kuunga mkono jambo lolote linaloanzishwa na Mkuu wa Wilaya hata kama lina tija kwa jamii.

Katika migogoro mingi kama hiyo ambayo imekuwa ikielezwa maeneo mbalimbali nchini ni wazi inatawaliwa na masilahi binafsi ya kila upande jambo linalowafanya kushindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu na kushindwa kumsaidia Rais ambaye amewaamini na kuwapa nafasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles